MWANAUME WA NDOTO ZANGU
SEHEMU YA 61
Kutoka moyoni sikupenda kabisa kumuandalia chai shetani, ila nilishindwa kubisha kwa sababu yeye ndiye kanioa na naishi kwenye nyumba yake. Niliingia jikoni, niliandaa chapchap kisha nilipeleka mezani. Baada ya sekunde chache mume wangu alitoka nje akiwa ameambatana na mkewe Rahabu, walipendeza kwelikweli, alafu walishikana mikono, funguo za magari zilitikisika tu, walitembea taratibu hadi mezani kisha wote wawili walikunywa chai yangu. Niliumia sana kuona mwanamke mwenzangu, mke mwenzangu, shetani nisiyempenda anakunywa chai iliyoandaliwa na mimi.
“Alafu we Gensu ebu njoo kwanza” Rahabu aliniita kwa dharau, niliumia sana. Yaani wazi wazi alianza kunikosea adabu mbele ya mume wangu ambaye hakushtuka wala hakushangaa.
“Hivi wewe Rahabu hizo jeuri unazitoa wapi? Unaniita mimi kama mdogo wako vile!!”
Niliamua kufunguka
“We nae si utulie, kwani unajua nimekuitia nini au unaropoka tu?…. Njoo nikuachie pesa ya matumizi, sisi tunataka kwenda kazini “
“Unipe pesa ya matumizi kwani wewe ndiye umenioa?”
“Kah!! Wabongo bwana, sasa kama huyo aliyekuoa hana pesa unataka upewe na nani? Watu hamna pesa lakini hamtaki kusaidiwa, mnataka mfe njaa?”
“Kama nimeolewa nimewekwa ndani, siwezi kufa njaa. Huyo aliyeniweka ndani atanipa chakula”
“Ooh kumbe una jeuri? Sasa ngoja tuone kama huyo mmeo atawapa pesa, ngoja tuone” Aliongea kwa hasira akiwa anarudisha pesa zake kwenye begi.
Walisimama kisha waliondoka, mume wangu hata kunitazama hakunitazama. Niligeuka pembeni nilimuona mama akinitazama tu, alinionea huruma, alinisisitiza niwe mvumilivu labda kuna siku mume wangu atabadilika.
*****
Nilijiua mume wangu hatosikiliza maneno ya Rahabu kuhusu kuacha pesa za matumizi, lakini haikuwa hivyo. Kwanza alimuhamisha mwanae Masoud alimpeleka akaishi na Rahabu. Alafu baada ya hapo roho mbaya zilianza. Siku ya kwanza hakutuachia pesa, tulitumia viakiba vilivyobaki. Siku ya pili hakuacha pesa, pia alianza kurudi usiku wa manane. Siku ya tatu hakuacha pesa, ilibidi mimi na mama turudi kwenye utaratibu wa mwanzo wa kula mlo mmoja au miwili. Uzuri ni kwamba unga ulikuwa wa kutosha, ila shughuli ilikuwa kwenye mboga. Kila siku ilinibidi nizunguke majumbani kwa
majirani zangu kuomba mboga za majani ambazo walilima nje ya nyumba zao.
Niliomba sana mboga ilifikia hatua hata majirani walinichoka, wengine walininyima na wengine walitaka kuniuzia, mfukoni sikuwa na kitu, hapo sasa misoto ya njaa ilizidi kukolea.
Nakumbuka siku hiyo kuanzia asubuhi hadi usiku hatukuingiza chochote tumboni zaidi ya maji ya kunywa tu. Mume wangu alikuwa kwa mke mdogo, alilala hukohuko. Simu nilimpigia sana lakini hakupokea, meseji hakujibu. Siku iliyofuata asubuhi mama yangu alihisi homa, ghafla alizidiwa!! Licha ya kwamba sikuwa na pesa ila nilikodi bajaji tulimpeleka hospitali.
Uzuri ni kwamba alipokelewa alianza kupewa matibabu kisha waliniandikia gharama zote ambazo nilitakiwa nilipe, gharama zilikuwa elfu
54. Sikuwaza sana, nilijua mume wangu atalipa. Nilitoka nje nilimkuta dereva bajaji akiwa amekasirika kwa kumchelewesha, aliniambia nimpe pesa yake ili aondoke. Haraka haraka
SEHEMU YA 62
nilimpigia mume wangu ili nimfahamishe, simu iliita ilipokelewa.
“Hallo mume wangu umeamkaje?” niliongea kwa upole
“Eleza shida” Alinijibu kwa sauti ya usingizi
“Niko hospitali hapa mama amezidiwa asubuhi hii”
“Sasa unaniambia kwani mi inanihusu nini? Kwani huyo ni mama yangu au mama yako?”
“Ni mama yangu. Ila nimekupigia ili uje hospitali kumuona, uje muda huu”
“Sina muda, kwanza nina usingizi. Na nikiamka nawahi kazini… “
“Mh sawa mume. Basi naomba nitumie pesa ya nauli ya bajaji elfu 10 pamoja na pesa ya matibabu elfu 54”
“Mimi sina pesa, labda mpigie Rahabu ongea nae, yeye ndiye boss wangu….. Na Rahabu anasema hawezi kukupa pesa kwa sababu una
jeuri… Hivyo basi tunaomba tafuta namna nyingine, sisi hatuna, tukutakie asubuhi njema” Alikata simu alafu aliizima, hakupatikana kabisa.
Nilichanganyikiwa, boda boda nae hakutaka kunisikiliza wala kunionea huruma; alinijia juu alinambia nimpe pesa yake aondoke la sivyo anaongeza bei iwe elfu 20. Nilivurugwa kiasi kwamba nilitamani kujikojolea…. Mara niliingia ndani, mara nilitoka nje, sikueleweka hata kidogo. Sasa nikiwa katika harakati za kuzunguka zunguka mara ghafla niligongana kibega na mtu ambaye alidondosha makaratasi yake. Kwanza niliogopa, niligeuza macho ili nimuone mtu huyo, nilishtuka kukutana na Genson akiwa amevalia mavazi ya kidaktari.
“Gensu, kumbe upo hapa? Unaumwa wewe au una mgonjwa?” Aliniuliza akiwa anaokota vitu vyake ambavyo vilidondoka
“Ni mama ndiye anaumwa” “Anasumbuliwa na nini?”
“Presha na vidonda vya tumbo”
“Ooh pole sana, yupo wapi nikamuone? Na mbona kama unalia? Kuna tatizo lingine zaidi ya kuumwa?” Aliniuliza swali zuri ila niliogopa kumjibu. Na kabla sijamjibu mara aliingia dereva bajaji
“Hivi we dada ni mwizi au ni tapeli? Yaani nimekusaidia nimemleta mama yako, umenikalisha tangu saa 3 hadi sasa saa 5, si unilipe pesa yangu!! Au unataka nipige kelele watu wajae?” Mwenye chake alidai chake, nilikuwa mpolee. Genson alinitazama mimi kisha alimtazama Dereva bajaji
“Kwani unamdai shilling ngapi?”
“Elfu 10 ila anipe 20 kwa kunichelewesha, amenikosesha wateja wengi sana”
“Msamehe sana, amekosa. Shika hii pesa…” Genson alihesabu elfu 30 alimkabidhi Dereva ambaye alichekelea kisha aliondoka.
“Gensu naomba nipeleke kwa mama nikamuone”
Huwezi amini alibadili safari aliungana na mimi tulienda chumbani kwa mama, kuanzia hapo matibabu yote ya mama aliyashughulikia yeye. Mama alilazwa hospital siku 3 lakini mume wangu hakuonekana, hakutupigia simu wala hakututumia pesa. Gharama za matibabu ziliongezeka, zilifikia laki 2.1 lakini zote zililipwa na Genson. Tukiwa pale hospitali yeye ndiye alituhudumia chakula, nilimueleza kila kitu kuhusu maisha nayopitia, alinipa pole, tulipeana namba kwaajili ya mawasiliano zaidi, hata muda ambao tuliruhusiwa kuondoka yeye ndiye alitupakiza kwenye gari yake, aliturudisha nyumbani kisha alinipatia pesa laki 2 za matumizi. Aliniambia zikiisha nisiogope kumtaarifu.
Tangu siku hiyo urafiki wangu na Genson ulianza rasmi na kwa kasi kubwa. Muda wote alikuwa ananitumia meseji za kunifariji na
kunipa matumaini. Aliniambia kwamba hata kama nina shida nyingi nisikubali kuumizwa na mtu ambaye hanisaidii kwa chochote. Tulichati asubuhi, mchana na usiku; nilihisi raha sana.
Kuna muda alinipigia alinifundisha mambo mengi kuhusu maisha. Sio mimi tu, bali hata mama yangu alimpigia, alimsalimia, alimtumia vocha na pesa ndogo ndogo.
Na tangu tumzoee Genson hatukulala njaa tena, mama yangu aliendelea vizuri, niliacha kabisa kumsumbua baba Masoud anitumie pesa zake za matumizi. Niliamua kumuacha afanye mambo yake kama anavyotaka. Sio hivyo tu bali niliacha kuwa ombaomba kwa majirani.
Mume wangu aliendeleza tabia zake za kurudi usiku, pia aliendeleza harakati zake za kutukaushia akidhani anatukomoa. Hakutaka kumjulia hali mama yangu na wala hakuna siku aliniuliza kuhusu homa ya mama.
*****
Siku hiyo mume wangu alirudi nyumbani alitukuta tukila kuku wa kukaanga, samaki losti, maini yalijaa kwenye bakuli, aliganda alitazama meza alishindwa kuelewa. Mimi na mama tulikuwa bize na misosi, tulifokonyoa minofu tu. Baba Masoud alipitiliza alielekea chumbani, baada ya sekunde chache alirudi akiwa amekasirika. Mkononi alishika pochi yangu ya kutunzia pesa.
“Kwanza nimewakuta mnakula minyama, nimeshangaa kwa sababu ni muda mrefu nimekuwa siwaachii pesa za matumizi, naingia chumbani nakuta pesa nyingi kwenye mkoba wako. Haya niambie hizi elfu 92 kakupa nani?
Nani huyo anawapa pesa za kula?”
SEHEMU YA 63
“Kwahiyo wewe ulitaka tusile ili tufe njaa?” Nilimjibu kwa kumtandika swali
“We mwanamke sitaki maswali, nimekuuliza pesa umepata wapi?”
“Nimeokota” Safari hii nlijibu kwa jeuri nikiwa naendelea kukandamiza misosi.
“Yaani nakuuliza alafu unaendelea kula, unanijibu ukiwa unatafuna tonge mdomoni….
Alafu wewe kumbe hunijui… Ngoja nikufunze adabu” Alinifuata kisha alirusha kofi akitaka kunipiga lakini nilizuia, nilimshika mkono kisha nilimkazia sura.
“Hivi wewe baba Masoud ni mwanamke gani anayeweza kuvumilia mateso unayonipa? Yaani mtu unatutelekeza alafu unashangaa sisi kula chakula, ina maana lengo lenu kutuua na njaa?…
Sikiliza nikuambie, sisi tuna watu, hatuwezi kufa njaa”
“Nilijua tu una mchepuko wewe. Na ndo huyo anayewapa kiburi. Haya sasa kama una watu naomba ondoka nenda kwa hao watu wako….
Ondoka haraka nenda kalale kwa mchepuko
wako… Toka nyumbani kwangu kabla sijakutoa roho” Alinishikia kisu alinitishia kunichoma.
Nilikimbia nilienda kukaa nje, alinifuata alinifukuza aliniambia nisikae karibu na nyumba yake.
Ili kuondoa shari niliamua kuondoka. Nilijizungusha mitaani, nilidhurula kuanzia mchana hadi usiku kisha niliamua kurudi nyumbani. Nilimkuta mama pekee akipika chakula cha usiku. Nilimuuliza kuhusu baba Masoud alinijibu hajui aliko. Basi tuliungana kwenye mapishi, tuliandaa vyakula mezani, sasa wakati tunataka tuanze kula mara mume wangu aliingia!! Yaani ile kuniona tu alinifuata kwa kasi akitaka kuja kunipiga, fasta nilisimama nilikimbilia nje. Alinitolea maneno makali aliniambia nisirudi tena nyumbani kwake, nitafute makazi mengine.
Licha ya kunifukuza lakini sikwenda mbali, nilikaa nje ya fensi; nyuma ya nyumba yake nikiwa nalia. Niliwaza nifanyaje? Nilale nje au
nikalale wapi?… Niliamua kumpigia mume wangu ili nimuombe msamaha lakini hakupokea simu. Nilitumia meseji nilimsisitiza kuwa sina mchepuko, nilimuomba anisamehe lakini niliambulia matusi tu, kupitia meseji alinitukana matusi makubwa makubwa ambayo hayafai kuandikwa au kusemwa.
Masaa nayo yalizidi kukatika. Ilifika saa 3, ikaja saa nne. Mbu walinisumbua lakini sikujali, nilikomaa nao. Mume wangu alijua kuwa nipo nje ya nyumba yake lakini hakutoka kuja kunichukua.
Nikiwa pale nje mara simu yangu iliita, nilitazama nilikuta ni Genson. Nilipokea tulisalimiana kisha aliniuliza kama nimekula, sikupepesa macho nilimjibu sijala. Pia nilimueleza kila kitu kilichotokea kati yangu na mume wangu, jinsi alivyokuta pesa kwenye pochi na jinsi alivyonifukuza.
“Kwahiyo muda huu umelala wapi sasa?”
Genson aliniuliza
“Nipo nje ya nyumba yake, siwezi kwenda kokote. Sina ndugu yoyote, nitalala hapa hapa nje”
“Mh ebu acha utani, nakuja hapo kukuchukua”
Simu ilikatwa. Baada ya dakika chache Genson alikuja kunichukua na gari yake, nilizama ndani kisha tuliondoka. Alinipeleka nyumbani kwa wazazi wake, nilipokelewa na mama na dada yake. Alinitambulisha kwao, aliwaambia kuwa mimi ni rafiki yake nimetokea mikoani. Alinipa msosi nilikula kisha alimpa maelekezo dada yake alimwambia alale na mimi na ahakikishe nakuwa na furaha. Baada ya kunikabidhi kwa dada yake aliaga kwamba anaondoka, alisema anaenda kazini (hospitali) kwenye zamu.
Tulikubaliana kukutana asubuhi ya siku inayofuata.
Mama yake alienda kulala, nilibaki na dada yake ambaye ni mpenda season. Ni muongeaji balaa!!
SEHEMU YA 64
Licha ya kwamba hatukuzoeana lakini muda wote alinisimulia kuhusu movie ambayo alikuwa anaitazama, mara alijitambulisha kuwa anaitwa Canisia, mara aliniambia nikaoge, na hakutamani kabisa niende kulala, alitaka tutazame season pamoja lakini mwenzie nilianza kusinzia! Alizima Tv tulienda kulala, tena nililala kwa uhuru wote! Nilijiachia kama kwangu vile. Nilimpigia mama mzazi nilimuambia kuwa hasijali nipo sehemu salama, alishukuru kusikia nimepata sehemu ya kulala.
***
Asubuhi kulipokucha sikusita kuungana na Canisia kwenye kufanya usafi. Nilipiga kazi kiasi kwamba mama yake alinisifia sana, alisema nafaa sana kuwa mkwewe. Sio mama tu, hata Can kuna muda alinitania aliniita wifi wa mchongo. Tulimaliza usafi, tulipika, tulikula, tulihamia kwenye seasons!
Mida ya saa nne asubuhi Genson aliwasili,
alifurahi kunikuta nimechangamka. Alileta zawadi nyingi kwaajili yangu jambo ambalo lilifanya Dada yake agunegune muda wote. Pia alituachia mboga na pesa za matumizi.
“Na naomba mchana apike Gensuda mana nitakuja kula hapa hapa” Genson alimwambia mama yake na Dada yake.
“Mmmh maajabu, yaani leo kaka utakuja kula hapa nyumbani?”
“Ndiyo, kwani vipi?” Alijibu akicheka
“Ama kweli wifi katuletea baraka ndani ya nyumba yetu”
“Wifi gani? Ushaanza maneno yako”
“Jamani si huyu hapa wifi yangu wa mchongo!! Ah ah ah nakutania bwana kaka…. We nenda, mchana atakupikia, Na usiku atapika ili uje kula hapa hapa”
Tulicheka Kwa pamoja, Genson alifurahi sana; aliaga kisha aliondoka. Tulibaki wenye nyumba
ambao tuliendelea kucheki movie na kupiga story mbalimbali. Mchana kama alivyoahidi Genson alirudi alikula chakula ambacho nilipika Mimi, alinisifia kuwa najua kupika kumzidi Dada yake. Sote kwa pamoja tulicheka kwa furaha.
Kiukweli nilitokea kuipenda sana ile familia, kwa namna tulivyozoeana unaweza sema tulijuana miaka 10 iliyopita kumbe ndo kwanza siku ya kwanza.
SEHEMU YA 65
Baada ya chakula mimi na Genson tulienda kukaa nje ya nyumba kisha tulifahamiana kiundani zaidi. Nilimueleza story yangu ya maisha tangu kufiwa na baba kijijini, kusaidiwa na Nasri, kupelekwa shule kisha kuachishwa shule baada ya kupewa mimba. Kubadili dini, kuolewa na Nasri kisha mateso ya ndoa. Alinipa pole kisha nae alinipa story yake kwa ufupi, aliniambia kwamba yeye ni muajiriwa mpya (daktari) wa hospitali ya wilaya. Na kuhusu mahusiano aliniambia yupo singo (hana mpenzi), anaishi na mama na dada yake baada
ya baba yao kufariki.
“Sasa kwanini husioe?” nilimtania
“Mh kuoa sio mchezo.. Ila ntaoa tu nikipata mtu sahihi…. Sitaki nipate shida za mahusiano kama unazopitia wewe. Hivi unajua kwanini unateseka sana kwenye ndoa yako?”
“Sijui”
“Ni kwa sababu uliolewa na mtu ambaye sio sahihi.”
“Mh! Bila shaka ni kweli kwa sababu nilikubali anioe kwakuwa tu alinipa mimba”
“Nakumbuka baba yangu aliwahi kuniambia kwamba SIO LAZMA NIMUOE MWANAMKE NILIYEMPA MIMBA AU ALIYENIZALIA MTOTO.
Pia hata nyie wanawake sio lazma uolewe na mwanaume aliyekupa mimba au aliyekuzalisha. Unatakiwa uoe au uolewe na mtu sahihi ambaye mnaendana kwenye shida na raha, tena muwe mnapendana kweli kweli. Ukimuoa
mwanamke sababu umempa mimba, mwisho wa siku atakukera au utamtesa tu mtoto wa watu. Vile vile ukiolewa na mwanaume eti kwakuwa amekupa mimba au amekuzalisha mwisho wa siku atakutesa, atakusaliti na atakufanyia mambo mabaya. Tunapaswa kutambua kuwa mapenzi na ndoa ni vitu viwili tofauti. Sio kila mpenzi wako anafaa kuwa mkeo au mumeo!! Ndoa sio mapenzi, ndoa ni maisha! Unapaswa kuchagua mtu kwa kuangalia vigezo vingi.”
“Ni kweli Genson lakini ndio hivyo ishatokea”
“Unajua nini Gensuda, yule mumeo na yule mke wake Rahabu wote lengo lao ni moja, kukukandamiza, kukutesa, kukudharau na kukufanya uwe mdogo kwao. Hivi unajua kuwa zile kesi zote za mmeo ni za uongo?”
INAENDELEA