MWANAUME WA NDOTO ZANGU
SEHEMU YA 06
Mamdogo baada ya kutufokea aliondoka kwa hasira, alituacha tukiwa tumezubaa kama mazombi vile. Kama kawaida mama alianza kulia, nilimchukua nilimlaza mapajani kwangu kisha nilimbembeleza, nilimwambia kwamba tusichoke kumuomba Mungu kwa sababu Mungu hamtupi mja wake, penye nia pana njia, hakuna marefu yasiyo na ncha, baada ya dhiki ni faraja, CHA MUHIMU NI UHAI.
Licha ya vitisho vyake lakini hatukuwa tayari kurudi kwake. Kutokana na mamdogo kubeba unga na mchele ilibidi tuishi kwa kula mihogo, maboga na matunda mwitu. Mwanzoni tulendelea kuomba chumvi kwa majirani lakini baadae hata majirani walituchoka, walituambia kuwa wameishiwa. Hapo sasa tulianza kula vyakula visivyo na chumvi. Pia matunda nayo yalianza kuadimika, maboga yalianza kwisha na tuliyachoka, mihogo nayo tulikula ilimradi tu.
Kukosekana kwa chumvi kulifanya vyakula visiwe vitamu, ilifikia hatua tulikosa hamu ya kula chakula, hasa hasa mama yangu kila alichokula kilimkataa, alianza kutapika, mara aliumwa tumbo, vidonda vya tumbo vilianza kumsumbua, tumbo liliwaka moto, muda wote alihisi njaa lakini hakupata hamu ya kula chakula. Kifua chake kilianza kubana, taratibu alianza kukohoa, alibanja makohozi ya kawaida na hatimaye alikohoa damu, alitapika damu, KWAKWELI NILICHANGANYIKIWA SANA,
nilivurugwa.
“Mwanangu nakufa” Mama aliongea akiwa anapumua kwa kasi
“Mama pliizii usifee…”
“Nakufa… Mwili wangu wote hauna nguvu, naona giza tu, nimeumwa sana, nimeteseka kwa muda mrefu, hivi vidonda vimenisumbua sana, kwa sasa naomba nikapumzike, tutaonana Mungu akipenda” Alimaliza kuongea
SEHEMU YA 07
kisha alifumba macho moja kwa moja
“Jamani sasa mimi nitabaki na nani mimii… Mama… We mamaa… Mama ndo umekufa kweli… Mama amkaaa… Jamani mama usifeeeee” Nilianza kulia kwa kasi ya ajabu, nilisimama nikiwa nimevurugwa, mara nilienda pale, mara kule, mara nilidondoka, mara nilimkumbatia mama yangu ambaye muda huo alikauka kabisa, hakutikisika wala nini.
Nguvu zote ziliniishia, akili yangi ilipoteana, kutokana na kuchanganyikiwa nilishindwa kujua nichukue maamuzi gani. Nilizungusha macho huku na huko sikuona mtu hata mmoja, watu wote walikuwa mashambani kwao wakilima.
Niliwaza nimchukue mama nimpeleke zahanati kijijini, ishu ni kwamba nitamchukuaje? Kwa nguvu gani nilizonazo? Kwa usafiri gani?
Nilikosa majibu nilibaki nalia tu.
Sasa nikiwa sielewi nifanye nini mara
nilishtushwa na honi ya gari kubwa ya mizigo (Kenta). Nyuma ya gari kulijaa roba nyingi za mkaa. Mbele walikaa watu wawili, dereva na boss wake ambaye alivalia suti nyeusi. Yule boss baada ya kuniona fasta alifungua mlango kisha moja kwa moja alimfuata mama yangu, pasipo hata kunisalimia wala kuniuliza chochote alimnyanyua mama alimpeleka mbele kwenye siti nyingine ambayo ilikuwa nyuma ya devera (siti ya katikati). Alimlaza mama kwenye siti hiyo kisha alinigeukia mimi.
“Binti twende, fanya haraka tumuwahishe mama hospitali” Aliniambia akiwa ameonyesha sura ya kuchanganyikiwa. Kilio changu kilikata bila kutarajia. Haraka haraka nilikimbia hadi kwenye gari, nilizama ndani kisha nilikaa pembeni ya mama.
Safari ilianza, kutokana na mzigo wa mkaa kuwa mwingi gari ilitembea taratibu. Yule boss
hakupendezwa na spidi ya gari, aliona kama dereva anazingua sana, fasta alimwambia hasimamishe gari kisha walibadilishana majukumu, bosi alishikilia usukani, kilichofuata hapo ni balaa zito, gari iliendeshwa kwa fujo hadi nilihisi labda anataka kutuua atutoe kafara. Baada ya dakika chache tulifika kwenye zahanati ya kijijini.
Tulikuta wagonjwa wamejazana pale zahanati, manesi wenyewe walikuwa ni wachache, huduma zilifanyika polepole, na hili tuhudumiwe tulitakiwa tupange foleni nyuma ya wale waliotangulia. Boss wa gari hakupenda suala la kupanga foleni, hakutaka kabisa kufuata utaratibu, alafu hakuogopa mtu, moja kwa moja alipitiliza alielekea ofisini kwa daktari. Sijui walizungmza jambo gani huko, bila shaka alitoa rushwa kwa sababu kabla sijakaa sawa nilishangaa manesi wakikimbizana kuja kwenye gari, walimchukua mama walimlaza kwenye kitanda cha mgonjwa (machela) kisha
SEHEMU YA 08
walimbeba kuelekea ndani.
Nikiwa pale hospitali licha ya kwamba mimi ndiye mwenye mgonjwa lakini sikuhusika kwa jambo hata moja. Mambo yote alisimamia yule boss ambaye hadi muda huo sikumfahamu jina lake wala sikujua anatokea wapi. Nikiwa nimekaa kwenye benchi nilimshuhudia akihangaika; mara alitoka nje, mara aliongea na daktari, mara aliongea na manesi, mara alichukua fomu kisha alijaza alafu alimpa daktari, baada ya muda alinifuata mimi.
“Binti” Aliniita
“Abee, vipi mama yangu anaendeleaje” Nilimuuliza nikiwa nasimama, macho yangu yaliutazama uso wake, alionekana kulia kiume, nilihisi labda ni kweli mama yangu kafariki.
“Hali ya mama haieleweki, hata madaktari wa hapa wameshindwa kutambua kama mama yetu kafa au ni mzima. Wameshindwa kujua kwa sababu viungo vyote vya mama
vimesimama, havionyeshi dalili ya kufanya kazi.”
“Aaahaah jamani kwahiyo mama kafa kwelii… Mama yangu amekufaaa” Nilianza kulia kwa sauti kiasi kwamba kila mtu alinitazama mimi, watu walinionea huruma. Yule bossi aliniziba mdomo kisha alinivuta pembeni
“Usilie, nani kakuambia kuwa mama amekufa? Kwanini nyie wanawake mna roho ndogo hivi?? Nimekuambia hali ya mama haieleweki, sijasema kwamba amekufa. Hivyo basi inabidi tupate uhakika, nimejaza fomu ya kuomba gari ya zahanati ili itupeleke Tanga mjini kwenye hospital ya wilaya au mkoa, huko tutakwenda kupata uhakika” Bosi alinifokea kwa sauti ya msisitizo na hasira, hakupendezwa na kitendo changu cha kulialia hovyo.
Alinifokea hadi niliogopa, kilio kilikata, nilitulia kimya. Mara gari ya zahanati iliwasili, yeye
aliondoka alielekea ofisini kisha baada ya muda alirudi akiwa ameongozana na manesi ambao walibeba mwili wa mama waliupakiza kwenye gari kisha nami niliambiwa niingie. Nilidhani yule boss nae ataingia kwenye gari ya kituo cha afya lakini hakuingia, aliniambia tutakutana hospitali. Dereva aliwasha gari tuliondoka kwa kasi, huo mwendo wake sasa hadi nilihisi kizunguzungu.
Baada ya mwendo wa masaa kadhaa hatimaye tulifika hospitali ya wilaya ya muheza, nilishtuka kumkuta yule boss akiwa tayari kashafika, tena alionyesha kwamba alikuwa anatusubiri sisi.
Haraka haraka walikimbizana walimchukua mama walimpeleka ndani, kilichoendelea huko wala sikukifahamu, nilitulia kimya nilimuomba Mungu atende miujiza kwa mama yangu.
Sekunde zilipita, dakika ziliondoka, Masaa yalikatika lakini hali hali ya mama bado haikueleweka. Siku ya kwanza ilipita, siku iliyofuata madokta walitoa taarifa kwamba
wameshindwa kumtibu mama, walitushauri tumpeleke hospitali ya rufaa ya mkoa. Kama ilivyokuwa mwanzo mimi na mama tulikaa kwenye gari ya hospital alafu yule boss alitumia gari yake. Yeye aliwahi kufika kabla yetu, alitupokea kisha matibabu yalianza Mara moja. Alisimamia matibabu ya mama ambaye ni mara chache sana niliruhusiwa nikamuone, kila nilivyoenda kumuona nilimkuta kafumba macho. Kuna muda niliwaza ni kweli mama kafa ila madaktari wananificha, hata hivyo sikutaka kukubaliana na mawazo yangu, niliendelea kumuomba Mungu.
Sasa siku hiyo usiku nikiwa sina hili wala lile mara nilishtushwa na sauti ya bosi ambaye aliniita akitaka kuniambia jambo.
“Binti”
“Ah-a- beee”
“Kumbe mama alikuwa anasumbuliwa na vidonda vya tumbo?”
“Ndiyo”
“Poleni sana, pia tumshukuru Mungu kwa sababu tayari mama ameamka, anaongea, anatabasam, na anakuita anataka akakuone”
SEHEMU YA 09
“We umesemaje? Mama angu Mimi ni mzima kaamka? Awe sio kweli…” Niliongea nikiwa nimekodoa macho, fasta nilisimama nilikimbia kuelekea chumbani kwa mama, ni kweli nilimkuta kakaa kitandani, Mama baada ya kuniona alitabasam kisha alicheka kwa furaha. Nilimrukia nae alinikumbatia, madaktari walihisi raha, bosi tajiri nae alikuja akiwa amebeba chakula; alifurahi kuona tunafurahi, alinikabidhi chakula alinambia nimlishe mama.
Nilipokea chakula kisha nilianza kumlisha mama ambaye kwa muda huu hakuwa na nguvu za kuweza kula yeye mwenyewe. Baada ya kula tulipiga story mbalimbali, nilimueleza
mama kilichotokea shambani, tulicheka kimbea hadi sio poa. Kila nilivyomtazama mama yangu sikuamini kama kweli ni mzima, aisee nilifurahi sana. Yule bosi alituletea maji na matunda kisha alinipa pesa, aliniambia anapeleka mzigo wa mkaa store kisha atarudi Siku inayofuata.
“Kwanza Huyo mtu ni nani? Mbona mkarimu sana?” Mama aliniuliza baada ya jamaa kuondoka.
“Hata mi simjui, ila yeye ndiye alitusaidia tangu shambani wakati umezimia. Anaonekana ni mfanyabiashara wa mkaa, ila sijui anaishi wapi”
“Ana utu sana, pia anajua kujali. Ni wanaume wachache sana wenye mioyo hiyo. Angekuwa mwingine angetuleta hospital alafu angetuacha, lakini yeye ametusimamia hadi nimepona.”
Nilitulia kimya, nilikosa cha kujibu kwa sababu mimi mwenyewe nilikubali kuwa Bosi tajiri ana utu mkubwa sana. Mama aliendelea kupatiwa matibabu ya kawaida, kile kikohozi kilikata,
hakutapika tena, hata zile damu hatukuziona tena. Tulilala hospitali kwa siku ya kwanza, siku iliyofuata tulidhani yule boss angerudi lakini hakurudi. Tulikaa siku ya pili, ya tatu, yule boss hakuonekana.
Siku ya nne mama aliruhusiwa kuondoka, ila kabla hajaondoka tulitakiwa tulipe baadhi ya gharama za kulazwa na matibabu ya mgonjwa. Tulipewa fomu ya malipo, tulitakiwa tulipe laki 3 taslimu. Kwanza nilishtuka, hata mama alikodoa macho, na ukicheki yule boss hakuonekana, tulichanganyikiwa.
“Sasa mwanangu hapa tunafayaje? Tutatoka kweli humu ndani? Na kadri tunavyokaa ndivyo gharama zinaongezeka”
“Mi hata sielewi, nilidhani yule boss ametulipia kumbe bado… Na mtu mwenyewe ndo haonekani, tangu alivyoondoka, au ametukimbia?”
“Hapana sijawakimbia, nipo kwaajili yenu” Boss
aliongea akiwa anaingia ndani, tulishtuka kidogo, nilipata wenge.
“Aah baba karibu… Karibu” Mama nae aliweweseka
“Nimekaribia mama. Msijali kuhusu malipo, nitalipia… Na vipi kuhusu nyinyi? Mkitoka hapa mnaelekea wapi?” Alituuliza swali ambalo lilikosa majibu, hatukujua tumjibu nini, niliogopa kumjibu kwamba tunaishi shambani.
“Mbona kimya? Au hamtaki nipafahamu kwenu?”
“Aah hapana baba angu…. Sisi… Sisi hatuna ma- ma-ma…. Sisi tunaishi kule kule sha-sha-shaa… ” Mama alishindwa kumalizia.
“Mh mnaishi shambani? Poleni sana. Basi kama itawezekana naomba niwaombe kitu kimoja”
“Tuombe tu baba angu” Mama aliitikia haraka haraka
“Naomba mkaishi nyumbani kwangu. Mama
yangu najua bado hujapona vizuri, unahitaji uangalizi, virutubisho na lishe nzuri kwaajili ya kuponya vidonda vyako vya tumbo. Mimi sina mama, naomba niishi na wewe kama mama yangu. Sijui kama upo tayari!!” Aliuliza akiwa anamtazama mama usoni
“Haina shida baba, nipo tayari” Mama alijibu kwa furaha akiwa haamini. Na baada ya jibu hilo yule jamaa alinigeukia mimi.
” Na kuhusu wewe binti kwa umri wako unatakiwa uwepo shuleni. Kwani uliishia level gani?”
“Niliishia kidato cha tatu”
“Mtaani maisha ni magumu sana, hata nikisema nikupe biashara inaweza ikakusumbua kwa sababu sio kila mtu atafanikiwa kupitia biashara. Inawezekana mafanikio yako yapo kupitia elimu ya darasani, wacha nikupeleke shule”
“Mimi narudi shulee? Jamani mi hata siamini..
Nashukuru sanaaa, Mungu akubariki” Niliongea kwa furaha nikiwa narukaruka, nilitamani kupaa, furaha yangu ilifanya mama yangu atabasam kwa raha, hata yule bosi alifarijika na aliinjoy kuona nafurahi.
Tulikumbatiana kwa furaha kisha alichukua fomu ya malipo alienda kulipia. Baada ya malipo alituchukua hadi kwenye gari, alituuliza kama kuna vitu vya msingi tumeacha kijijini, tulimwambia kuwa tumeacha magodoro, vitanda, nguo na baadhi ya vyombo vyetu.
Alituambia hakuna haja ya kuvifuata kwa sababu tukifika kwake tutakuta vingine, pia kuhusu nguo alisema atatununulia zingine. Baada ya mazungumzo mafupi tulianza safari kuelekea nyumbani kwake.
*****
Baada ya safari ya muda mchache hatimaye tulifika mjengoni. Tulianza maisha mapya ndani
ya jumba kubwa la kifahari. Ukubwa na uzuri wa nyumba ile ulifanya muda wote niwe nazungusha macho kila kona, sio mmi tu hata mama yangu alionyesha ushamba mwingi tu.
Kwa mara ya kwanza tulikaa kwenye nyumba yenye sofa nyingi, kiyoyozi kikubwa, baada ya muda mwenye nyumba akiwasha Tv kubwa, hapo sasa macho yetu yaliganda kwenye Flatscreen, kiukweli nilihisi kama niko peponi vile.
Yule boss alikaa kwenye sofa jingine, alitukaribisha nyumbani kwake kisha alijitambulisha kuwa anaitwa Nasri Rajun. Hapo sasa nilitambua kuwa kumbe yeye ni muislamu. Alitueleza kuwa yeye ni Afsa misitu na wanyama pori, na ni mjasiriamali mkubwa wa mkaa ambao anausambaza maeneo mbalimbali ya Tanga. Mimi na mama Kazi yetu ilikuwa ni kuitikia tu. Nasi tulijitambulisha kwa kumueleza historia fupi ya maisha yetu, jinsi baba alivyofariki na namna tulivyoishi maisha
magumu baada ha kifo cha baba.
Alitupatia pole kisha alituambia tujisikie tupo nyumbani. Siku hiyo kila kitu alitufanyia yeye, alitupikia, alituandalia msosi, tulikula, aliondoa vyombo, tulioga kisha alituonyesha vyumba vya kulala, kila mtu na chumba chake. Vyumba vilikuwa vizurii, kitanda kizurii, magodoro mazuri, kila.chumba kina Tv na choo humo humo, aisee maisha haya, nyie kuna watu wanaishi jamani kah. Baada ya ukaribisho na utambulisho tuliagana na kila mmoja alielekea chumbani kwake kulala.
*****
Siku iliyofuata nilikuwa wa kwanza kuamka. Kwakuwa niliishi nyumba ya watu nilitakiwa nionyeshe tabia njema. Hivyo basi baada ya kuamka nilianza kufanya usafi wa nyumba nzima, madirisha, nje ya nyumba, vyombo na kila kitu. Mama aliamka alikuta namalizia
kufanya kazi, kutokana na afya yake hakutakiwa kufanya kazi yoyote ngumu. Alioga kisha alinisaidia kuandaa chai. Bosi Nasri baada ya kuamka alikuta nyumba imependeza, chai iliwekwa mezani, alibaki anashangaa tu, kutoka moyoni alijivunia na alifurahia uwepo wetu nyumbani kwake.
“Jamani kwani nyie watu mliamka usiku wa manane au?” Aliongea akiwa anatabasam
“Ah ah ah hapana, mi niliamka saa 12 tu” Mama alijibu akiwa anacheka
“Mmh mnanishangaza kwakweli. Hongereni sana kwa kunisaidia kufanya usafi wa nyumba nzima, mimi mwenyewe ni mvivu sana kufanya usafi. Ila mama yangu hutakiwi kujitesa, afya yako bado haijakaa sawa.”
“Najua, kwanza mimi hata sijafanya kazi. Aliyefanya hii miujiza ni Gensu, yeye ndiye aliamka saa 11 kisha alifanya usafi.”
“Wow! Hongera Gensu”
“Asante” Nilijibu nikitabasam kwa furaha, bichwa langu lilivimba kinoma, nilijiona kama queen wa usafi dunia nzima.
“Ok sasa inabidi tujiandae ili tuelekee shopping ya nguo zenu na vitu vya nyumbani. Pia Gensu tayari nimepata shule ambayo utaenda kusoma. Kwa muda huu mfupi uliobaki itabidi uanzie tena kidato cha tatu kisha mwakani uingie kidato cha nne”
“Sawa haina shida” Nilijibu kwa raha jamani nusura nilale chini nigalegale
“Ni shule ya bording kwahiyo utahamia huko huko. Na kuhusu mama kubaki hapa itabidi nimletee dada wa kazi ambaye atamsaidia kwa shughuli mbalimbali. Nadhani tumeelewana”
“Ndiyo tumeelewa” Mimi na mama tulijibu kwa pamoja
“Sawa. Tujiandae, tunywe chai kisha tuondoke” Haraka haraka tulijiandaa, tulipiga misosi ya
SEHEMU YA 10
asubuhi, tulizama kwenye gari kisha tuliondoka kuelekea madukani. Mama alinunuliwa magauni, vitenge, kanga, begi, vijora, madela, sendo,
ndala na viatu kama vyote. Mimi nilinunuliwa sare za shule, mabegi ya nguo na daftari, vifaa vya shule, nguo za kuvaa nyumbani, mazoezini na vinginevyo. Tulinunua vyombo vya nyumbani, mboga na vifaa vingine kisha tulirudi.
Siku iliyofuata tulimpokea dada wa kazi ambaye ni binti mdogo tu, umri wake ni kama miaka 15 hivi. Binti huyo licha ya kwamba nilimzidi umri lakini pia nilimzidi mwili. Mwenzangu alikuwa mwembama, mimi umbo langu ni la saizi ya kati, sio mnene wala sio mwembamba. Mwenye nyumba alitutambulisha upya, alimtambulisha dada wa kazi ambaye jina lake ni Rahabu kisha alimsisitiza dada huyo atuheshim sisi na zaidi zaidi amuheshimu mama ambaye atakuwa anakaa nae muda mwingi.
****
Tulianza maisha ya watu wanne ndani ya nyumba. Tuliishi kwa furaha, amani na upendo wa hali ya juu. Kwa namna tulivyoishi unaweza sema sisi ni familia ya mama na watoto wake. Kiumri mama yangu alikuwa ana miaka 50.
Boss nasri yeye alikuwa ana 32. Mimi miaka 18 na Rahabu 15. Kwahiyo mama angu alionekana kama mama yetu sote, licha ya kwamba ni mama wa mimi tu lakini wote tulimuheshim kama mama yetu mzazi. Pia mimi na Rahabu tulimuita Nasri Kaka. Rahabu aliniita mimi Dada. Namna ambavyo tulikuwa tunaishi ilifikia hatua nilisahau kama niliwahi kupitia shida na matatizo, nilijiona toto la kishua.
Mama alipendeza sana, ule uzee ulianza kuondoka ghalfa, akipiga pamba zake unaweza sema ni binti wa 35 kumbe 50. Nasri yeye muda wote ni suti tu, muda mwingi alikuwa anashinda kazini kwake, kumuona ni jioni au usiku, kimuonekano yeye ni mrefu, mweupe, ana mwili wa unene lakini sio bonge, pia ana kitambi cha
saizi kati. Mavazi yake yalifanya aonekane ni mtu wa heshima sana. Na kuhusu mimi ungeweza kunikataa kwamba ni yule wa kijijini. Guu lilichomoza, upaja kama wote, unywele ulirefuka, tako sio sana ila lilisimama, mafuta yangu ni losheni tupu!!! Mtoto niling’aa, nilikuwa mzuri zaidi ya white house. Rahabu nae unaweza sema sio dada wa kazi, licha ya wembamba wake lakini mwenzangu alinizidi tako. Sura na shepu nilimzidi lakini mwenzangu alikuwa mtoto kipotabo!! Basi ndo hivyo maisha yetu yalikuwa mazuri tu, chakula tulichagua tule nini, siku nyingine hatukupika kila mtu alinunua anachokitaka yeye, tuliinjoy sana.
****
Muda wa shuleni ulifika, Kaka Nasri alinilipia ada zote. Tena nakumbuka ada ilikuwa ni million 1.3 pamoja na hostel. Kwa mara ya kwanza nilianza masomo kwenye shule ya mtu
binafsi, pia kwa mara ya kwanza niliishi bwenini. Kutoka shuleni hadi nyumbani palikuwa na umbali mrefu, ilikuwa ngumu kwangu kurudi nyumbani, uzuri ni kwamba nilinunuliwa sim kiswaswadu ambacho nilikitumia kuwasiliana na mama, Rahabu na kaka Nasri.
Uzuri wa ile shule ni kwamba ilikuwa ya wanawake tupu, hata waalimu walijaa wakike tupu, hivyo basi hakukuwa na usumbufu wowote kutoka kwa wanaume. Ilikuwa ni shule yenye ulinzi mkali, kila kitu kilifanyika ndani ya fensi la shule, kutoka nje ni hadi likizo ifike. Pia muda mwingi sana ulitumika kwaajili ya vipindi vya darasani, kujisomea na michezo. Hakukuwa na muda wa mwanafunzi kupumzika bila kazi, labda iwe usiku muda wa kulala tu!. Mwanzoni ratiba hizo nilikuwa sizipendi, niliona kama zinanibana kwa sababu nilikuwa mvivu wa kusoma muda wote.
Sio kwamba sikuipenda shule au sikupenda kusoma, ila nilikuwa mvivu tu. Mara nyingi
nilipenda kujitenga na wenzangu. Wapo ambao walitaka kutengezeza urafiki na mimi lakini nilikuwa nawakwepa kwa sababu walikuwa wanapenda sana kusoma, niliogopa wakiwa marafiki zangu watanisumbua muda wote nisome nao jambo ambalo sikulitaka. Kwenye vipindi niliingia lakini nilikuwa sielewi kitu, walimu wakiniuliza kama nimeelewa nilijibu ndio. Balaa lilikuja wakati wa mitihani, kila somo nilishikilia mkia, ni kiswahili tu nilipata D, masomo mengine yote ni F-F-F.
INAENDELEA