MWANAUME WA NDOTO ZANGU
SEHEMU YA 51
“Hivi mume wangu siku hizi pesa zako unazipeleka wapi? Mshahara mbona sihuoni? “
“Mke wangu we acha tu, haya madeni haya yatakuja kuniua. Si unakumbuka kipindi kile nimewajengea nyumba wewe na mama yako?”
“Eeh nakumbuka”
“Zile pesa nilikopa. Hata ile gari yako ni pesa za mkopo. Biashara yangu ya mkaa imekufa kwa sababu serikali imeingilia kati, imekataza watu
kuchoma mkaa. Na mshahara wangu wote unaishia kulipa madeni”
“Mh pole mume!! Kwahiyo tunafanyaje sasa? Mana maisha yamekuwa magumu, duka langu ndo kama hivyo halina kitu chochote nimeamua kulifunga, kwa sasa hata Mimi sina pesa”
“Lakini usijali, Mimi ni mwanaume sitoshindwa kutafuta pesa zingine kwaajili yenu. Kwa sasa wewe utakaa hapa nyumbani, kama pesa za matumizi nitakupa”
Ni kweli tangu nianze kuwa mama wa nyumbani kila siku aliniachia pesa za matumizi bila shida yoyote. Vipesa vidogovidogo havikukosekana, shida ndogondogo zilikwisha, sikujua pesa anapata wapi ila nilishukuru kuona nakula na kulala bila shida. Uzuri ni kwamba nilikuwa mvumilivu. Nilikubaliana na hali ya mume wangu. Japo hakunipeleka shopping, hakunipa pesa za kusuka lakini nilimpenda.
****
Pia kwa kipindi chote hicho sikupata taarifa zozote kuhusu Rahabu, sikujua yupo kijijiji kwao au yupo wapi, ila tu niliamini huko aliko atakuwa anaishi maisha magumu sana. Japo sikumuombea mabaya lakini sikutamani kabisa nimuone machoni kwangu, sikutamani awe karibu yangu, bado nilimchukia kwa mambo aliyonifanyia.
Sasa siku hiyo katika pitapita zangu mara ghafla nilimuona Rahabu akielekea kwenye kigari kidogo aina ya IST, kama kawaida yake alikuwa amependeza kinoma. Tena alipendeza kuliko hata alivyokuwa anapendeza wakati anaishi nyumbani kwangu. Pia kitu kingine kilichonishtua ni ukubwa wa tumbo lake, alionekana kuwa mjamzito.
“Hivi ni yeye au namfananisha?…. Kama ni yeye mbona amekuwa mzuri kuliko mwanzo? Na
hiyo gari ni ya nani? Alafu mbona kama ana
mimba???…. Ile mimba kaipata lini? Ni mimba ya nani? Au baada ya kumfukuza alipata mwanaume ambaye anamlea?”
Nikiwa bado natafakari wenzangu aliwasha gari aliondoka pasipo kuniona. Aliniachia maswali mazito sana. Nilidhani baada ya kumfukuza angepata shida lakini ni kama nilimpiga teke chura. Ama kweli maisha ni kama gwaride.
Niliwaza yaani leo hii Mimi na familia yangu tunaishi maisha ya kubangaiza alafu Rahabu kawa bosslady? Duh dunia ina mambo hii.
Sio hivyo tu bali majirani zangu waliniambia kwamba ile frame ya duka langu ambalo lilifirisika kuna mdada mwenye pesa kaichukua alafu anauza nguo zile zile kama ambazo nilikuwa nauza Mimi. Japo ilikuwa in taarifa ya kushangaza lakini sikushtuka sana, niliona in jambo kawaida tu.
Sasa siku hiyo mume wangu sijui alilalia upande upi, sijui alishawishiwa na malaika gani,
alinipatia pesa laki 2 aliniambia nikafanye shopping. Kwanza nilishangaa, nilijiuliza kama hana pesa anawezaje kunipa laki mbili nikapoteze kwenye kununua nguo??.
Nilimuuliza pesa kapata wapi?… alinijibu aliniambia niache maswali nitumie pesa.
Basi bwana kwanza nilinunua mafuta nilijaza kwenye kigari changu ambacho kilikuwa kinazimazima, nilikipeleka gereji kilipigwa service kisha nilielekea madukani. Nilinunua vinguo vyangu, nilimnunulia na mwanangu, nilijaza vitu kwenye mfuko kisha nilipiga hatua kuelekea kwenye gari yangu nikitaka kurudi nyumbani.
Sasa wakati naelekea kwenye gari macho yangu yalitua kwenye frame yangu ya zamani. Wateja wengi walijazana wakiingia na kutoka kwenye frame hiyo. Nilitazama kwa makini, juu ya kibao paliandikwa maandishi ambayo yaliushtua moyo wangu. Macho yangu hayakuamini mara baada ya kukutana na jina la
duka ambalo lilisomeka hivi “RAHABU SHOPPING CENTER”
Nilijiuliza ni Rahabu huyu huyu ninayemjua mimi au kuna mwingine?… Ghafla nilipandwa na umbea wa kutamani kujua zaidi. Nilipeleka mizigo kwenye gari, niliseti mtandio wangu vizuri ili nisitambulike kirahisi kisha nilipiga hatua kuelekea dukani ili nikajihakikishie vizuri zaidi. Nilikuwa makini kwelikweli, nilifika dukani nilijibana pembeni ya wateja, macho yangu yalitazama ndani ya duka, nilishtuka kuona wahudumu ni wengi. Wahudumu walikuwa watatu, wawili wakike walikuwa wanauza nguo, mmoja wa kiume alikuwa anatoa huduma za kifedha (Mpesa, Tigo pesa, nk) kwenye duka hilo hilo, alafu boss wao alikaa kwenye kiti cha kuzunguka akihesabu pesa, pia akiwa anaandika vitu mbalimbali kwenye daftari.
Umbea niliutamani ila tumbo la kuhara nalo lilinisumbua, Presha iliniandama, nilitamani niondoke haraka Ila niliona hasara kuondoka
SEHEMU YA 52
pasipo kumtambua boss wa duka hilo. Mara ghafla boss alisimama kisha aligeukia upande wangu, weuwee! Nilishtuka nilijibana nyuma ya mlango, kwa macho yangu mawili nilimuona Rahabu ninayemjua akiwa amekamata pesa nyingi mkononi. Alimuita mfanyakazi wake wa kiume kisha alimwambia apeleke pesa benki.
Nilikosa pozi, niliishiwa swaga. Niliganda kwa sekunde chache nikiwa natafakari, sikuwa na namna ya kufanya, taratibu niligeuka nyuma kisha kinyonge nilielekea kwenye gari yangu.
Niliondoka nilirudi nyumbani nikiwa bado siamini nilichokiona. Nilifika nyumbani nilishangaa kumkuta mume wangu kasharudi toka kazini kwake, alafu alikaa kinyonge sana.
“Vipi mume mbona kama una mawazo?”
Nilimuuliza
“Yani maisha haya we acha tu. Nilikamatwa na polisi”
“We acha utani baba Masoud, ulikamatwa muda
gani?”
“Leo asubuhi baada ya kufika kazini nilikutana na polisi, walinipa kesi ya kuhujumu uchumi kwa kuharibu misitu kupitia biashara ya mkaa ambayo nilikuwa naifanya”
“Eeh jamani kwahiyo ilikuwaje sasa?”
“Nimeambiwa nilipe faini million 14, au jela miaka miwili… Nimekubali kulipa faini.
Nimepewa mwezi mmoja nilipe deni, lasivyo nitapelekwa jela.”
“Mmh jamani pole mume wangu, sasa hiyo million 19 tutailipaje jamani” niliongea kwa uchungu.
“Mi hata sielewi, na hapa nilipo sina hata 100 mbovu… Kadi yangu ya mshahara imeshikiliwa hadi nilipe deni. Serikali imenifungia imeniambia siruhusiwi kufanya Biashara yoyote kwa sasa hadi nilipe deni… Na hata kazi kwa sasa nimesimamishwa, siruhusiwi kwenda kazini hadi nilipe deni. Yani mke wangu huu
mwaka nisipokufa kwa presha sijui…” Nae aliongea akiwa anatoa machozi
Nilimtazana nilimuonea huruma, pia machozi yake yalifanya nichanganyikiwe. Niliwaza ndani ya mwezi mmoja tutapataje million 19?
Tutakula nini? Tutaishije? Nilipagawa!!! Nilitamani hata ile laki 2 aliyonipa nisingeitumia. Kutokana na kuvurugwa tulibaki tumekaushiana tu, kila mmoja alitazama upande wake.
“Mke wangu mimi nina wazo” “Wazo gani?”
“Unaonaje tuuze gari yako na ya mama hata kwa million 8 zote mbili ili tupunguze deni?”
“Sawa mume haina shida. Ilimradi hii kesi iishe tu, gari sio kitu” nilijibu kwa moyo mkunjufu
Mume wangu baada ya kusikia hivyo alitabasam kwa furaha, aliacha kulia. Alidhani ningekataa gari yangu iuzwe kumbe mie sikuwa na kinyongo chochote. Kwanza tulimpigia
mama tulimuelekeza alikubali gari yake iuzwe, aliileta nyumbani. Mume wangu aliongea na watu wasiojulikana ambao baada ya muda mchache walikuja nyumbani walilipa pesa million 9 kisha waliondoka na gari zote mbili.
Mambo yalifanyika chapchap hadi nilishangaa lakini sikuuliza chochote, nilikausha kimya.
Mume wangu alitushukuru mimi na mama, mama yangu aliondoka alirudi nyumbani kwake.Tulibaki wenye nyumba. Baba Masoud nae aliniaga alisema anaelekea kituo cha polisi kupunguza deni. Baada ya kulipa alirudi nyumbani kisha tuliendelea kuwaza namna ambavyo tutapata million 10 iliyobaki. Hapo sasa vichwa viliuma. Nilimshauri nae auze gari yake lakini alikataa. Siku ya kwanza ilipita, wiki ya kwanza ilikatika, wiki ya pili iliondoka lakini million 10 haikupatikana.
Na tangu hasimamishwe kwenda kazini muda wote tulikuwa tunashinda nyumbani tukitazamana tu. Uzuri ni kwamba mama yangu
alikuwa anatunza vijipesa, yeye ndiye mara nyingi alikuwa ananipa vijisenti vya kununua dagaa na mboga za majani. Tulifulia kiasi kwamba tuliacha kabisa kunywa chai asubuhi. Chakula chetu kililiwa mchana na usiku tu.
Wiki tatu zilikwisha, tulianza kuhesabu siku zilizobaki ili tukamilishe mwezi mmoja.
Mwenzangu alionyesha kutojali sana, kila nikimuuliza tunafanyaje alinijibu kama ni kufungwa na afungwe. Maneno yake yaliniumiza lakini sikutaka kumkatia tamaa, niliwapigia mashoga zangu wanikopeshe lakini hawakuwa na pesa, nilipita kukopa kwenye vikundi vya wajasiriamali lakini walishindwa kunikopesha kwakuwa sikuwa mwanachama wa vikundi hivyo!! Harakati zangu zote zilifeli, nami sikuwa na namna, nilimwomba tu Mungu atufanyie miujiza.
Na hatimaye mwezi mmoja ulitimia, kwa mujibu wa polisi ni kwamba mume wangu alitakiwa alipoti kituo cha polisi tarehe 31 lakini
hakwenda kwa sababu hakuwa na pesa. Siku iliyofuata asubuhi na mapema tuligongewa mlango, tulitoka nje tulikutana na migambo wawili wakiwa wameshika virungu. Kabla hatujakaa sawa mume wangu alikula mtama wa Nguvu alidondokea chini, walimuweka chini ya ulinzi.
“Unashindana na jeshi la polisi? Kwanini Jana hukuripoti kituoni?” Mlinzi mmoja aliongea kwa hasira kisha alimlamba Kofi la kichwa mume wangu
“Jamani msameheni mume wangu, msimpige hivyoo” Nilianza kulia kwa uchungu, nilichanganyikiwa, nilihisi kuzimia sio kuzimia, kufa sio kufa, kwakweli nilivurugwa.
“We Dada kaaa mbali, tumeagizwa tuje tumkamate huyu mumeo muhujumu uchumi. Na leo ataenda kunyea debe!! Haiwezekani watu wapande miti alafu yeye aikate na kuuza mkaa, serikali inahangaika kulinda misitu na
maliasili ya taifa kumbe kuna hawa majangiri wanatuhujumu… We jangiri si umeshindwa kumaliza deni la million 10? Haya simama twende kituoni…”
“Hey muacheni… Muacheni haraka… Eti deniii deni, kwani pesa kitu gani…” Hiyo sasa ilikuwa ni sauti ya Mrembo mkali ambaye aliongea kwa dharau na kujishaua kutokana na pesa alizonazo. Sote kwa pamoja tuligeuza macho ili tumuone Mrembo huyo ni nani, aisee sikuamini, hakuwa mwingine bali ni RAHABU.
SEHEMU YA 53
Alifika pale tulipo kisha alifungua mkoba wake, alichomoa vibunda vingi vya noti za Tsh elfu 10, alizihesabu pale pale zilikuwa ni million 10 kisha akiwa anatabasam alimkabidhi baba Masoud. Mume wangu hakuamini kabisa, alitaka kupiga magoti ili ashukuru lakini
alizuiliwa na Rahabu; aliambiwa hasiwe na wasiwasi, aliambiwa awahi kituo cha polisi akalipe deni.
Muda huo Mimi nilibaki nimeganda tu, nilikosa maneno. Kiukweli sikupenda msaada wa Rahabu ila nilishindwa kumzuia kwa sababu sikuwa na njia nyingine ya kumsaidia mume wangu. Baada ya kupokea pesa mume wangu aliondoka pamoja na migambo walielekea kituoni. Rahabu alinigeukia Mimi, alinitazama kwa macho ya huruma na upole, alionekana mtakatifu kwelikweli.
“Pole sana dada Nairath (Gensuda), unapitia kipindi kigumu sana. Nilisikia kuhusu kesi ya Shem, kiukweli nisingeweza kukubali Shem afungwe wakati Mimi nipo. Nyie watu mlinisaidia mambo mengi, tuliishi kwa amani, licha ya kwamba nilikuwa dada wa kazi lakini mlinichukulia kama ndugu yenu. Na ndio maana leo hii nami nimeamua kuja kuwasaidia!! sina maneno mengi, kwaheri na niwatakie maisha
mema” Aligeuka kisha aliondoka.
Mimi bado niliganda tu nikimtazama, nilishindwa hata kumshukuru kwa sababu roho yake ilinishangaza sana. Nilidhani angekuwa ananichukia kutokana na kumfukuza nyumbani kwangu, kumbe ndo kwanza alizidi kutupenda na kutujali kwenye shida na Raha!! Tabia yake ilifanya nami nipunguze hasira juu yake, licha ya kwamba aliwahi kuniibia mume wangu lakini ghafla nilianza kumpenda, nilipunguza kumchukia.
Baada ya kulipa deni mume wangu alirudi nyumbani akiwa mwenye furaha. Aliniambia tumshukuru sana Rahabu, nilikubaliana na yeye kwa moyo mkunjufu kabisa, sikuwa na kinyongo chochote.
****
Siku chache mbele mume wangu alipokea barua ya kurudi kazini, mshahara wake ulifunguliwa, aliruhusiwa kufanya Biashara,
alifunguliwa vikwazo vyote. Kiukweli nilifurahi sana, nilifurahi kwa sababu mshahara wake ulitusaidia kuondoa dhiki ndogondogo ambazo zilikuwa zinatuandama.
Maisha yaliendelea bila shida. Hata hivyo sikupenda suala la kuendelea kuwa mama wa nyumbani, nilichoka kumtegemea mume wangu kwa kila kitu. Nilitamani nianzishe Biashara nyingine ili nitengeneze pesa zangu ambazo zingeweza kutusaidia muda ambao mume wangu aliishiwa au alikosa. Nilimshirikisha baba Masoud wazo hilo lakini alikataa, alisema hataki kuniona nahangaika kutafuta wateja, alitaka kuniona natulia nyumbani tu.
Pia aliniambia hataki kuona nasumbuliwa na wanaume ndio maana alitaka niwe mama wa nyumbani tu. Kwakuwa mume wangu hakupenda Mimi niwe mjasiriamali, nisingeweza kubishana nae. Pia uzuri ni kwamba tangu arudi kazini pesa za matumizi aliniachia, hivyo basi sikuona sababu ya
kung’ang’ania kuanzisha biashara yangu, niliamua kutii amri zake za kutaka niwe mama wa nyumbani. Kwa ufupi ni kwamba alinitumia katika matumizi ya kulea familia, kupika, kufanya kazi za nyumbani na kumpa starehe ya chumbani tu.
****
Ulipita mwezi mmoja tukiwa hatuna shida wala changamoto yoyote. Sasa siku hiyo mchana tukiwa tunakula mara tulishtushwa na ugeni mzito wa maofsa wawili wa taasisi (kampuni) binafsi ya kutoa mikopo. Maofsa hao ambao walivalia sare maalumu walijitambulisha kwa kutuonyesha vitambulisho vyao kisha walitueleza kilichowaleta kama ifuatavyo.
“Bwana Nasri nadhani sisi unatufahamu” “Ndiyo ndiyo wakuu wangu”
“Ni miaka 12 imepita tangu tukukopeshe mkopo
wa fedha za ujenzi wa nyumba yako ambayo ni hii unayoishi. Tulikubaliana mkopo ulipwe ndani ya miaka 10 lakini hadi sasa miaka 12 bado hujalipa. Kila siku umekuwa ukituambia utalipa kesho, kesho, Kesho! Simu zetu hupokei na ndio maana tumeamua kuja hapa kwako. Na tumekuja hapa kwa jambo moja tu. Ulipe deni letu la million 40 au tuipige mnada hii nyumba yako pamoja na mali zote.”
Baada ya maelezo hayo nilishindwa hata kula, tayari nilivurugwa, yaani kila siku shida tu, likitoka hili linakuja lile. Nilidhani nyumba alijenga kwa pesa zake kumbe alikopa!!
Nilidhani nimeolewa na mume mwenye pesa zake za halali kumbe ni pesa za michongo tu. Ilifikia hatua nilitamani kulia mbele ya maofsa mikopo lakini nilivumilia.
“Mr Nasri hatuna muda wa kupoteza, gari yetu ya mnada ipo hapo nje kwaajili ya matangazo”
“Eeh jamani yaani mmeamua kuja na gari ya
matangazo? Kweli kabisa mnataka kuuza nyumba yangu??… Naombeni niongezeeni hata mwaka mmoja, mwakani nitawalipa pesa zenu zote” mume wangu aliongea kwa uchungu
“Tumesema hivi, tumekuja hapa kuchukua pesa au kupiga mnada… Kama huna pesa hii nyumba tunauza leo.. Ngoja niwaambie watu wa matangazo waanze kutangaza” Aliongea kama utani vile, alichukua simu yake kisha alianza kuchati na mtu wa matangazo. Baada ya sekunde chache tulisikia “TANGAZO TANGAZOOOOO….” Mume wangu alishtuka, alisimama akiwa amechanganyikiwa.
“Jamani basi basi msitangaze. Kwa sasa sina pesa ila naomba mtoke nje mara moja, kuna jambo nataka niongee na mke wangu kuhusu kulipa deni leo hii”
Wale maofsa baada ya kusikia hivyo hawakuwa wabishi, walitoka nje. Mume wangu alinigeukia Mimi, alifungua mdomo akitaka kuongea kitu
lakini mara alifunga, alishindwa kuongea. Nilimshangaa kwa sababu sikujua anataka kuongea nini.
“Vipi mbona kama kuna kitu unashindwa kuniambia?… We niambie tu”
“Mmh mke wangu sijui nianzie wapi Ebu
fikiria mwanzo tuliuza gari yako na ya mama yako, alafu leo nataka tuwape ile nyumba yenu wapige mnada; je utakubali mke wangu kunisaidia kwa hilo?” Aliongea kwa unyenyekevu akiwa ananitazama kwa macho ya huruma. Niliwaza kama yeye ndiye alitujengea nyumba, yeye ndiye mume wangu, sasa nitaanzaje kumkatalia?
“Haina shida, japo mama yangu atanung’unika ila ndo hivyo haina jinsi”
“Msijali nitawajengea nyingine, kuhusu mama itabidi arudi aje aishi hapa. Ile nyumba ngoja tuwakabidhi hawa watu waipige tu mnada”
Japo roho iliniuma ila nilikubali pasipo kinyongo
chochote. Kwanza tulimpigia mama tulimpa taarifa, ilikuwa kasheshe kumuelewesha. Nae hakuwa na pingamizi, alikubali nyumba ipigwe mnada ili kumnusuru mkwe wake. Baada ya makubaliano tuliondoka pamoja na maofsa mikopo tulielekea mjengoni, waliitazama nyumba pamoja na vitu vya ndani, walijiridhisha kuwa vinawafaa, tuliwakabidhi hati zao na maandikishano yalifanyika. Japo nilishangaa hakukuwa na mashaidi lakini nilishindwa kuhoji.
Muda ule ule walibandika mabango yaliyosomeka “NYUMBA INAUZWA”. Pia walianza kufanya matangazo kwa kutumia vipaza sauti. Mimi, mama na mume wangu tulirudi nyumbani mikono mitupu, dada wa kazi tulimrudisha nyumbani kwao.
SEHEMU YA 54
Tayari nilipoteza gari, nyumba na biashara yangu kwaajili ya kulipa madeni ya mume
wangu. Bora hata gari na biashara havikuniuma sana, lakini nyumba iliniuma vibaya mno.
Kilichoniuma zaidi ni kwamba tulipoteza nyumba pamoja na vitu vyote vya ndani ikiwemo sofa, vitanda na magodoro, friji na makabati, meza na viti, watu wa mikopo hawakutuachia kitu hata kimoja. Moyoni nilimuonea wivu mtu ambaye alibahatika kununua nyumba yetu yenye thamani kubwa kwa bei ya mnada.
Lakini pia kupoteza biashara nako bado kuliniuma sana, kwa maisha ya sasa mwanamke kukosa kipato chako inakuwa sio vizuri. Wanaume wa siku hizi wanapenda mwanamke mwenye pesa ambazo anazitengeneza yeye mwenyewe, pia ukiwa tegemezi wa kila kitu ni rahisi kuchokwa.
Mama yangu mzazi kurudi kuja kuishi na mimi kwenye nyumba ya mume wangu hiyo wala haikuniuma, lakini kitendo cha mimi na mama kushinda nyumbani kuanzia asubuhi hadi jioni
tukitegemea kila kitu kutoka kwa mume wangu kilininyima raha kwa sababu nilihisi ipo siku baba Masoud atatuchoka kisha ataanza kutuendesha atakavyo kwakuwa yeye ndiye anatulisha na kutuhudumia kwa kila kitu.
SEHEMU YA 55
“Nimeimiss nyumba yetu, sahizi ningekuwa kwangu ningekuwa nimekunja nne najichekia Tv…. Sijui nani anamiliki mjumba wetu kwa sasa, namuonea wivu sana” Mama aliongea kwa Manung’uniko. Muda huo tulikaa kwenye mkeka nje ya nyumba
“Kumbe nawe unasikitika kama mimi. Yani hapa natamani niende nikachungulie ili nikamuone huyo anayemiliki mjengo na mali zetu”
“Ebu twende wote, twende tukamsalimie tukampe hongera zake”
Tulikuwa tuna mawenge kwelikweli, nyumba ilitukondesha. Kuna muda niliona nilikosea sana kumruhusu mume wangu aiuze, bora hata tungeuza vitu vya ndani na gari yake kuliko
nyumba yangu. Tatizo la mume wangu ni mbishi na mjanja, yeye kila akidaiwa
alinishawishi tuuze mali zangu tu, zake hakuuza. Na sijui kwanini alinifanyia hivyo.
Basi bwana mimi na mama tuliondoka tulielekea mahala iliko nyumba yetu ili tukaone inamilikiwa na nani. Baada ya nusu saa tulifika, kwanza tulishtuka kukuta ulinzi mkali getini.
Ilibidi tugande nje, tuliogopa kuingia ndani. Tulihisi labda mmiliki wa nyumba hiyo ni kigogo wa serikali mwenye mapesa mengi ndio maana kaweka mlinzi. Tuliganda tukiwa tunashangaa shangaa!!
Tukiwa bado tumezubaa mara tulishtushwa na honi ya gari ambalo lilitaka kuingia ndani, fasta mimi na mama tulikimbizana tulikaa pembeni, tulikuwa kama machizi vile. Baada ya kusogea pembeni tuligeuza macho ili tuione gari ya boss mwenye nyumba, aisee tulishtuka!! Hasa hasa mimi nilishtuka, macho yalinitoka, nilishindwa kuamini hata kidogo mara baada ya kuiona gari
yangu ya zamani ambayo niliiuza.
Nilidhani naota, nilihisi labda naifananisha. Uzuri ni kwamba mwenye gari baada ya kutuona alisimamisha gari kisha alifungua vioo, alifungua mlango kisha alishuka chini akiwa anatabasam!! Hapo sasa sio mimi tu, hata mama yangu nusura aanguke kwa mshtuko!!
Tulikodoa macho kisha tulimtazama Rahabu ambaye alishuka kutoka kwenye gari yangu ya zamani, kama kawaida yake alipendeza kinoma; alivaa kama BOSSLADY, mkononi alishika kipochi cha pesa.
 INAENDELEA