MWANAUME WA NDOTO ZANGU
SEHEMU YA 46
Kiukweli yule mkaka (Genson) alinichanganya sana, alinivuruga kichwa, aliniacha njia panda. Bora hata angeniambia kuna hivi na vile kuliko maelezo aliyoniachia. Nilitulia niliwaza nifuate ushauri wake au nipotezee? Niliamua kupotezea, nilipiga kazi zangu hadi jioni, nilifunga duka nilirudi nyumbani.
Nilimkuta mume wangu kasharudi, Kwa mahaba mazito alinikimbilia alikuja kunipokea. Alinipeleka chumbani, tulienda bafuni tulioga, aliingia jikoni alipika chakula cha watu watatu tu
ambao ni Mimi, yeye na mtoto wetu Masoud. Nilimuuliza vipi kuhusu Rahabu, alinijibu kwamba Rahabu atajipikia mwenyewe. Kama mwanamke sikupenda suala lile, nilichukua chakula nilikipeleka chumbani kwa Rahabu, nilimkuta akilia machozi tepetepe.
“Pole mdogoangu, usilie sana. Chukua chakula ule” nilimwambia
“Mimi hii nyumba yenu siiwezi, bora nirudi nyumbani. Tangu ile siku umesema natoka na shem, shem ananichukia sana, ananitesa, ananiambia nimekonda nimekuwa kama ufagio wa chelewa, mshahara hanilipi, chakula mnaninyima… Sasa ndo maisha gani haya?
Nirudisheni nyumbaniiiii” alizidi kulia
“Nisamehe mimi dada yako, nisamehe kwa sababu mimi ndiye chanzo cha matatizo yote, nilikuhisi vibaya kumbe haupo hivyo. Nisamehe sana, sitaki kabisa uondoke hapa kwangu kwa sababu ni ngumu sana kumpata dada wa kazi
mwenye tabia njema kama zako! Nakupenda sana mdogoangu” Maneno yangu yalifanya aache kulia. Nilimshawishi ale chakula alikubali, nilifurahi kuona ametulia.
Nilirudi sebuleni niliungana na mume wangu na mwanangu, tulikula kisha tulienda kulala. Usiku sikupata usingizi mzuri, muda mwingi niliwaza sana maneno ya Genson. Nilitamani kufuata maagizo yake ila niliona kama nitajisumbua tu, nilimpuuzia nilimuona anataka kunibabaisha tu, hana lolote wala nini. Nilijifunika shuka nililala.
***
Siku iliyofuata ilikuwa ni jumamosi. Siku hiyo mume wangu alinipeleka kazini, muda wote tuligandana kama ruba. Sasa tukiwa kazini mara alikuja yule mkaka Genson, muda huo mume wangu alikuwa bize akichezea laptop. Genson aliulizia bei za vitu lakini hakununua. Ila kwa siri alinipatia kikaratasi ambacho sikujua kimeandikwa nini. Baada ya kunikabidhi
aliondoka, kwa hofu nilimtazama mume wangu nilishukuru hakuniona, bado alikuwa bize na laptop. Kimya kimya nilisoma ujumbe wa kwenye karatasi, uliandikwa hivi. “Jana nilikuambia nini? Mbona hukufuata maagizo?.
Hivi unajua kuwa mumeo na Rahabu hawana ugomvi? Wanakuzunguka wewe tu!
Wanakuzuga ili usielewe chochote kuhusu wao. Je unajua wao wana siri gani?… Ukitaka kujua basi naomba asubuhi hii muage mumeo mwambie umepata dharula ya wiki moja, kisha utaondoka alafu jioni utarudi nyumbani na utaingia ndani kisha ujifiche ndani ya nyumba yako”. Ujumbe uliishia hapo. Mwili wangu ulianza kupamba moto!! Kwa mara nyingine nilimtazama mume wangu nilimkuta kakomaa na laptop. Nilitafakari mwanzo nilimdharau Genson, je nimpotezee tena???… Safari hii niliona hapana!!
” Mume wangu”
“Naam kipenzi changu” Aliacha kuchezea PC
SEHEMU YA 47 & 48
kisha alinitazama
“Nimepata dharula hapa. Nimetumiwa meseji natakiwa leo niende kijijini kuna msiba wa shangazi…. Nimewaambia kuwa nina mimba kubwa siwezi kwenda lakini wamekataa, wameniambia nahitajika leo hii… Nimeongea na mama lakini anasema anaumwa hawezi kwenda, kwahiyo ni lazma niende mimi Yani
hapa sijui nifanyaje, na nimeambiwa kule nitakaa siku 3…. Leo, kesho na kesho kutwa….
Ah mi siendi”
“Mh mke wangu kwanini husiende? Sio tabia nzuri, itabidi uende. Kwani nauli shilling ngapi?….
Tena bora umeniambia mapema ili nami nikupe lambilambi yangu… Nenda kaniwakilishe na mimi”
“Mh jamani kwahiyo niende pekeyangu? Mi nilidhani utanisindikiza.. Basi itabidi niongee na Rahabu anipeleke”
“Rahabu hawezi kwenda kwa sababu mimi
mwenyewe nimepata simu ya dharula, leo hii inabidi niende dodoma kwenye kikao, nitarudi kesho mchana. Rahabu itabidi abaki na Masoud pale nyumbani”
“Sawa mume, mi ngoja niende nyumbani nikajiandae kisha niondoke”
“Twende wote tukajiandae ili tupelekane stendi, nikuache unaelekea kijijini kisha nami niende Dodoma”
Kauli yake ya kunipeleka stendi iliniogopesha. iliniogopesha kwa sababu sikuwa na mpango wa kusafiri. Hata hivyo niliamua kutulia, tulifunga duka tulirudi nyumbani, tulijiandaa, kila mmoja alikusanya vitu vyake kwenye begi, tulimuaga Rahabu kisha tuliondoka.
Tulifika stendi, mume wangu ndiye alinikatia ticket, nilizama kwenye gari ya kijijini kwetu, alihakikisha gari yetu inaondoka kisha nae aliendelea na harakati zake. Sikujua kama ni kweli alitaka kwenda Dodoma au alikuwa
anizuga tu.
Nikiwa kwenye gari nilihesabu kituo cha kwanza, kituo cha pili, kabla sijafika mbali nilisimamisha gari niliwaambia kuwa kuna kitu nimesahau hivyo basi natakiwa nirudi nyumbani. Sikudai nauli, nilishuka kwenye gari; wao waliendelea na safari lakini mimi niligeuza njia, nilirudi mjini, nilielekea nyumbani kwa mama kisha nilitulia kimya.
Masaa yalikatika, jioni kama nilivyoelekezwa nilirudi nyumbani kwa mume wangu. Kwakuwa mazingira niliyatambua wala sikuhofia sana.
Nilikuwa makini kwelikweli. Nilibahatika kukuta mlango ukiwa wazi. Nilichungulia ndani sikumuona mtu yeyote. Nilinyata taratibu kuelekea sebuleni, mara nilisikia mazungumzo toka jikoni, yalikuwa ni mazungumzo kati ya mume wangu na Rahabu, walisikika kama ifuatavyo.
“Hawezi kurudi, nimempeleka mwenyewe hadi
stendi, nimehakikisha gari yao inaondoka kisha nimerudi. Yeye anadhani naenda Dodoma kumbe nilimdanganya tu”
“Kwahiyo unataka kuniambia sipaswi kuogopa? Leo ni kujiachia tu ndani ya mjengo au sio?”
“Sasa je. Na uzuri ni kwamba anajua kuwa mimi na wewe tumegombana kumbe wala… Hiyo kesho kutwa akirudi atatukuta tushafaidi sana”
“Ah ah ah! Kama nakuona vile jinsi ulivyonipania, tusuburi Masoud alale”
Maneno yao tu yalinivuruga, yalifanya nipatwe na tumbo la kuhara. Nilitamani niwafuate huko huko jikoni lakini niliogopa nitaharibu maelekezo ya Genson. Nilipiga mahesabu nikajifiche wapi? Niliamua kwenda stoo ambako huwa hakuingiliki mara kwa mara.
Ndani ya stoo kulikuwa na gunia nyingi za mkaa na mahindi, nami nilijipachika katikati ya gunia hizo, nilitulia kimya.
Nikiwa stoo kuna muda hewa ilikuwa nzito,
nilitamani kukohoa lakini nilijibana, nilitamani kubanja lakini nilimeza makohozi, mkojo uliniuma lakini niliubana ilimradi nitimize maagizo. Wakiwa jikoni kwa mbali niliwasikia wakikimbizana, mara walitaniana, mambo yalikuwa moto kweli kweli.
Saa moja na nusu walimaliza kupika, vyakula viliandaliwa mezani, walikula kisha walimlazimisha mwanangu Masoud aende kulala. Rahabu ndiye alimpeleka Masoud chumbani, alimlaza kisha alielekea sebuleni kwa mume wangu!! Nilishindwa kuona wanachofanya ila sauti zao nilizisikia, walikuwa bado wananijadili mimi kwamba siwezi kurudi.
Mara nilisikia wakifunga madirisha na milango kisha walielekea chumbani kwangu. Hapo sasa nilizidi kuumia, sikutegemea kama Rahabu nae angeweza kuingia chumbani kwangu na kulala kwenye godoro langu. Japo sikujua wanafanya nini ila nilikuwa makini na sauti zao. Kuna muda waliongea kwa sauti kubwa, mara walipunguza
sauti na ghafla sauti zilikata. Nilianza kusikia miguno, mara kitanda kilipiga kelele na hatimaye kwa masikio yangu mawili nilimsikia Rahabu akilalamika kimahaba!!
“Bebiii hapo hapoo…. Taratibu basi tusije tukamuamsha mtoto”
“Hawezi kusikia, na hata akisikia hatojua chochote. Wewe jiachie, niache nifanye kazi yangu, leo ni mwendo wa mundende tuu!!”
“Aaah jamaniii… Ila sasa usije ukanichezea, kumbuka kuwa hata mimi natamani kuwa mke wa mtu na natamani kuwa kwenye nafasi kama ya mkeo… Isije ikawa unanichezea tu..”
“Kwani una wasiwasi gani? Wewe na yule nguchiru nani mzuri?… Alafu nilishakuambia kuwa napenda wanawake vimodo kama wewe, si unaona navyokumudu. Sasa yule andunje na ule mwili wake nitaufanyia nini mimi?
Mwanamke akinikalia juu nusura anivunje, lakini wewe kiuno unacho, mzigo unao, shepu unayo,
vichuchu unavyo, mtoto mashallah!! Walahi nakuambia kuwa wewe kwangu ni namba 1 alafu yule Tembo simpi namba yoyote” Walinisimanga wakiwa wanaendelea na michezo yao
Aisee nilivumilia nilichoka, niliona liwalo na liwe, kama noma na iwe noma. Nilitoka stoo kwenye maroba kisha moja kwa moja niliwafuata huko huko chumbani!!
SEHEMU YA 49
Mambo niliyoyaona nashindwa hata kuelezea. Kwa macho yangu mawili niliwakuta wakiwa watupu kama walivyozaliwa, walikuwa katikati ya ushenzi wao!! Walishtuka baada ya kuona nimeingia, walikurupuka kila mmoja alijirusha upande wake, walivuta mashuka walijifunika.
Kwa muda huo sikutaka kupambana na mume wangu, nilitaka kwanza nipambane na mwanamke mwenzangu tuonyeshane makali.
Niliokota kiatu changu kimoja nilikirusha usoni kwa Rahabu, nusura nimtoe jicho! Kwa bahati nzuri kilitua shavuni kwake, damu zilichuruzika. Nilimrukia pale pale kitandani kisha nilianza kumshushia kipigo, nilimtwanga ngumi za pua, za uso, za tumbo na za kichwa.
Mume wangu nae alivyo bwege eti alikuja kumsaidia Rahabu. Alinishika mimi kisha alinisimamisha, alinitazama kwa jicho la hasira kisha alinitwanga bonge la kofi, kwa bahati mbaya nilihisi kizunguzungu nilidondokea tumbo la mimba!! Pale pale Damu zilianza kuvuja kutoka sehemu zangu za siri!! Nguvu nazo ziliniishia, ghafla nilifumba macho alafu nilitulia kimya!! Sikujua nini kilifuata.
*****
Nilikuja kushtuka nipo hospitali, mwili wangu ulipambwa na maumivu kila kona, hasa hasa sehemu za siri, muda wote nilihisi kuna kitu kitu
kinataka kutoka. Pembeni alikaa mume wangu ambaye alinitazama usoni mara moja kisha alitazama pembeni; alinionea aibu kutokana na kile kilichotokea. Mara aliingia daktari ambaye alinipima kisha alimtazama mume wangu;
“Ulisema mkeo alianguka si ndiyo?” “Ndiyo dokta”
“Pole sana. Baada ya kuanguka alipata madhara makubwa kwenye mfuko wa uzazi ambao mwanzo ulitoboka. Mimba imeharibika baada ya damu nyingi kuvuja”
“Imeharibika? Imeharibikaje tena dokta? Mimba ya miezi sita inaharibikaga kweli?”
“Ndiyo. Kwa sasa naomba utupishe kwa sababu tuna kazi ya kuhakikisha anaondoa kiumbe cha tumboni ili kisije kikamletea madhara makubwa”
Mume wangu alichanganyikiwa baada ya kusikia mimba imeharibika, alitoka nje akiwa
bado haamini. Mimi muda wote nilikuwa nalia tu, sikutegemea kama ningepoteza ujauzito wangu kirahisi namna hiyo. Sikuwa na namna, nilitulia nilisubiri maelekezo ya dokta. Kwanza nilihamishwa wodi nilipelekwa wodi ya uzazi, nilichomwa sindano za uchungu kisha nilizalishwa kiumbe kilichokufa.
Hayo yote yalifanyika pasipo mama yangu kujua. Nililazwa hospital kwa wiki nzima nikipewa dawa za kusafisha uzazi, kuziba matundu yaliyotoboka kwenye mfuko wa uzazi na kuondoa maumivu. Baada ya kupata nafuu niliruhusiwa kuondoka. Mume wangu alitaka kunichukua kunirudisha nyumbani kwake lakini nilikataa, sikutamani tena kwenda kuishi pamoja na watoa roho!! nilielekea nyumbani
kwa mama ili nikapumzike kwanza.
Ilipita siku ya kwanza sikuona simu wala meseji ya mume wangu, tulikaushiana. Siku ya pili alinipigia sikupokea. Meseji zake za kuniomba nirudi nyumbani sikuzijibu. Siku tano nzima
zilikatika nikiwa kwa mama. Mama alianza kupata wasiwasi, aliniuliza kama kuna tatizo niliamua kumsimulia kila kitu. Kwa hasira nilimueleza kuanzia namna ambavyo kaka Nasri alinipa mimba nikiwa shule, jinsi nilivyofukuzwa shule, alivyonishawishi kunioa, nilivyomfumania na Rahabu na jinsi alivyonipiga kofi lililonidondosha chini hadi nikapoteza ujauzito.
“Eeh kwahyo hapo huna mimba?” “Sina..”
“Mi nilijua tu nyie mnanificha mambo mengi. Nilitaka kushangaa eti wanafunzi wote mfukuzwe shule? tangu lini?… Kumbe mlipeana mimba mkiwa shulee…. Kwahiyo hapo mmegombana? Hutaki kwenda kwako?”
“Unataka niende wakanitoe roho au? Mi siwezi kwenda”
Mama alisikitika kisha alinipa pole. Lakini pia aliogopa endapo nisiporudi kwa mume wangu naweza kuachika alafu tukaanza kupata shida
tena. Alinishauri nirudi nyumbani kwangu, nilikataa katakata. Hata kama mume wangu alikuwa ni kila kitu kwenye maisha yetu lakini sikutaka kukubaliana na matendo yake kwenye ndoa yetu. Hata kama amenisaliti lakini sio kwa kulala na mchepuko wake ndani ya nyumba yangu, kwenye godoro lile lile ambalo mimi na yeye huwa tunalalia.
Siku iliyofuata asubuhi nikiwa nimelala; mama alikuja kuniamsha, aliniambia kuna ugeni mzito. Niliamka nilivaa vizuri kisha nilitoka nje, nilishtuka kumkuta mume wangu akiwa amevalia kanzu na barakashea. Kwa kumtazama unaweza sema mtu kumbe ni shetani mkubwa. Nilitamani nirudi chumbani nikaendelee kulala lakini mama yangu alinizuia, alinipa ishara nikae chini nimsikilize.
Taratibu nilikaa chini kwenye sofa kisha nilitazama pembeni kwenye ukuta, sikutaka kutazamana na gaidi. Usoni nilivimba kwa hasira, moyoni niliwaza kumkatalia chochote
SEHEMU YA 50
ambacho alitaka kuniambia. Niliwaza jinsi nilivyowakuta uchi wakifanya uasherati, namna nilivyopoteza mimba kwa upumbavu wake wa kumtetea Rahabu! Aisee hasira zangu zilizidi kupanda, nilianza kulia pale pale kisha nilinyanyuka nilikimbilia chumbani kwangu, nilijifungia mlango.
Walikuja kuniita, waliniomba sana, walinipigia magoti nitoke nje lakini sikuwasikiliza. Nilidhani mume wangu angeondoka lakini hakuondoka.
Alichukua nyundo aliniambia kama sifungui mlango anaharibu kwa nyundo. Nilidhani anatania, ghafla nilisikia “tiiih, tiih, tiih” alianza kugonga nyundo kwenye mlango. Nilienda kumfungulia, alizama ndani kisha aliamua kutumia nguvu, alinivuta alinipeleka sebuleni kwa mama.
“Mke wangu nisamehe sana, mama mkwe pia naomba nisamehe mimi mwanao nimekosa… “
“Sawa baba nakusikiliza” Mama alijibu, mimi
nilitulia kimya
“Najua mwanao kakueleza kila kitu. Nakiri kuwa ni kweli nilimsaliti, lakini ilikuwa ni kwa bahati mbaya. Kiukweli kabisa mimi na mke wangu tangu ashike mimba ya pili hatukushiriki tendo kutokana na matatizo yake ya uzazi.
Nilimvumilia kwa miezi mingi lakini mimi kama mwanaume ilifikia hatua nilishindwa, hapo sasa shetani alinishawishi nifanye ujinga ambao leo hii naujutia. Nimekuja hapa kuomba msamaha kwa sababu hili ni kosa langu la kwanza, mke wangu wewe unajua kuwa mimi sio msaliti kwako, ni hiyo mara moja tu ambayo umenifumania ila sijawahi na sitorudia tena.
Naomba rudi nyumbani tulee familia, na kuhusu Rahabu niko tayari nimfukuze kwaajili yako…
Yaani leo hii tukifika nyumbani tu, Rahabu namfukuza”
Aliongea maelezo mengi lakini nilielewa hapo kwenye kumfukuza Rahabu tu. Niliwaza angalau moyo wangu utapata amani endapo
kama Rahabu atafukuzwa. Mama yangu alikuwa mtu wa kwanza kumsamehe mume wangu, baada ya kumsamehe alinishawishi na mimi nimsamehe. Ilikuwa ngumu ila mwisho wa siku nilimsamehe kisha nilichukua begi langu tulirudi nyumbani.
Baada ya kufika nyumbani kama alivyoahidi, alimwambia Rahabu akusanye vitu vyake, alimkabidhi kiasi cha pesa kisha alimfukuza. Nafsi yangu ilitulia, japo walinipitisha kwenye kipindi kigumu lakini kuondoka kwa Rahabu niliamini mume wangu atatulia, ndoa yetu itakuwa salama.
******
Maisha mapya ya Mimi Na mume wangu yalianza vizuri sana. Licha ya majukumu kuwa mengi lakini sikutamani tena kutafuta Dada wa kazi, niliamua kukomaa mwenyewe. Asubuhi nilifanya kazi zote, mume wangu alielekea kazini kakwe na Mimi nilielekea kwangu.
Mwezi mmoja ulikatika sikusikia story yoyote mbaya kutoka kwa mume wangu. Lakini licha ya kutulia, alianza kuonyesha mabadiliko ambayo sikujua yalitokana na nini. Kwanza kila mwisho wa mwezi alilalamika kuwa hana pesa, alishindwa kulipa ada ya mtoto shule, pesa za matumizi nazo zilimshinda. Majukumu yote ya familia aliniachia Mimi. Zile pesa zangu ambazo nilikuwa nawekeza benki; zote nilianza kuzitumia kwaajili ya matumizi ya nyumbani, kulipia mtoto ada na mengineyo. Na kwakuwa Mimi ni mkewe wala sikujali sana kutumia pesa zangu, nilijisikia fahari kuona namsaidia majukumu mume wangu kipenzi.
Bandu bandu humaliza gogo, pesa za benki zilikwisha; nilihamia kwenye pesa za faida. Ilikuwa kila siku nikipata faida, niliitumia kununua vitu vya nyumbani. Faida ilianza kupungua, nilianza kula mtaji, ilifikia hatua duka lilipukutika kabisa, niliongea na mume wangu lakini hakuonekana kushtuka sana. Aliniambia
ni mambo ya kawaida Biashara kufirisika, tulianza kuishi maisha yasiyofanana na status yetu. Mtaani watu walimuona mume wangu ana pesa nyingi, walidhani tunakula milo kamili, lakini haikuwa hivyo! Ndani ya familia tulipitia uvumilivu mwingi tu. Yale mambo ya kila mtu kula kwenye sahani yake yalikwisha, tulianza kula wote kwenye sahani moja.
INAENDELEA