MWANAUME WA NDOTO ZANGU
SEHEMU YA 41
Nilipagawa. Niliwaza mume wangu alinambia boksa kaisahau gest!! Sasa imekuwajekuwaje niikute chumbani kwa Rahabu???? Nilibaki
mdomo wazi, macho yalinitoka, sura ilinipauka, nilibaki nimeduwaa tu!!! Hata ile hamu ya kusuka iliniisha. Fasta nilimpigia simu Rahabu, simu iliita kisha ilipokelewa.
“We Rahabu, hii boksa ya shemeji yako imefikaje huku chumbani kwako?”
“Boksa? Boksa ipi tena dada?”
“Wewe usijitoe hufahamu, nipo chumbani kwako muda huu. Nimekuta boksa ya mume wangu kwenye kabati lako, nani kaiweka??”
“Oooh nimekumbuka, itakuwa jana wakati naanua nguo zangu nilichanganya na za shemeji. Na sio boksa tu, nadhani ukiangalia kwa makini utaona nguo zake zingine, nilizichanganya kwa bahati mbaya”
Nilichunguza kwa makini ni kweli nilikuta koti la suti la mume wangu, singlendi na suruali moja. Zote zilionekana kuwa zimetoka kufuliwa!
Zilinukia vizurii. Maelezo ya Rahabu niliyaelewa ila sasa nilijiuliza hizo nguo za mume wangu zilifuliwa lini? Na ni nani huyo ambaye alizifua?… Japo sikupata majibu lakini niliamua kukubali tu, nilielekea sebuleni ambako nilisukwa kisha msusi aliondoka.
Usiku nilimuuliza mume wangu kuhusu kuzikuta nguo zake chumbani kwa Rahabu. Alinijibu kuwa yeye mwenyewe ndiye alizifua pamoja na boksa. Angalau nilipata auheni, moyo wangu ulitulia.
*****
Ilikuwa ni siku nyingine, siku ya jumamosi. Familia nzima tulikuwa ndani ya mjengo. Siku hiyo mume wangu alichangamka sana, pia muda wote alikaa karibu yangu hadi nilishangaa!! Nilijiuliza kapatwa na nini lakini sikupata jibu. Mara alinichezea tumbo langu, mara alinibusu, mara alinivuta hadi kitandani alinichombeza kwa maneno matamu.
“Mke wangu hivi unajua nakupenda sana?” “Kweli mume wangu? Hunizidi mimi”
“Nakuzidi… Alafu hii mimba yetu ni ya miezi mingapi?”
“Kwa sasa ina miezi mitano, siku chache zijazo itafikisha miezi sita.”
“Woooow!! Namsubiri sana mtoto wangu wa pili… Nakupenda mnoo”
“Asante mume wangu, mi naomba tu uendelee kunipenda, kunijali, kunivumilia kwa hii hali yangu, husije ukanisaliti baba Masoud”
“Siwezi…. Weee nikusaliti wewe? Kwa uzuri huo? Kwa utamu ulionao? Yaani nikuache wewe niende kwa wanawake wengine wasio na
tumbo wala mgongo??… Aaah hapana, kwanza hiyo haiwezekani, haitokuja kutokea mimi kukusaliti wewe, nakuapia mbele za Mungu” Aliongea kwa msisitizo mkubwa.
Maneno yake yalifanya nijisikie fahari sana, maneno yalikuwa kama tiba moyoni mwangu, nilisahau matukio yote aliyonifanyia siku chache zilizopita. Pia kitendo cha kuapia mbele za Mungu kilizidi kunipa matumaini, imani na kujiamini kwamba hawezi kunisaliti.
Tuliendelea kubebika, kuna muda alininyanyua alinirudisha sebuleni kwenye sofa, alinilaza juu ya mapaja yake kisha tulitazama movie akiwa anachezea nywele zangu. Hadi jioni inafika mume wangu hakuniacha hata kidogo.
Sasa tukiwa bado tumelaliana kwenye sofa mara Rahabu alifika akiwa amependeza vibaya mno. Kama kawaida yake alivaa hijabu na nikabu utasema ni muarabu. Alituaga kuwa anaelekea sokoni kununua mboga ya jioni.
SEHEMU YA 42
“Jamani wapendanao ngoja niwaache muendelee kubebika, mimi naenda sokoni kuwanunulia mboga ili niwapikie”
“Mboga? Mboga gani tena? Mchana zilibaki mboga za kutosha!! Maharage yapo, samaki zipo, mchicha upo, matunda yapo.. Kwahiyo hakuna haja ya kwenda sokoni, pia muda umeenda sana! Pumzika tu” Nilimwambia Rahabu ambaye alikosa pozi, alikosa muelekeo!!
“Muache tu aende akanunue vitafunwa vya
asubuhi” Mume wangu alidakia
“Vitafunwa vipo, kuna viazi, magimbi na mchele upo jikoni” niliendelea kugonga msumari
“Lakini mimi leo nina hamu sana na nyama, hizo samaki zenu nimezichoka. Kwahyo Rahabu kama unaenda sokoni itakuwa vizuri sana!!
Nenda kaninunulie nyama, alafu shika hii pesa kanunue na soda kreti moja tuweke kwenye friji”
Nilijitahidi kuzuia lakini waliniweza. Rahabu alipokea pesa kisha aliondoka alielekea sokoni. Nyumbani tulibaki mimi, mume wangu na mwanangu Masoud ambaye muda mwingi alikuwa bize na masomo yake ya shuleni.
Dakika zilikatika, nusu saa ilipita Rahabu hakurudi. Nilitazama muda nilikuta tayari imetimia saa moja usiku. Mume wangu alisimama alielekea kuoga, alivaa kibukta chake na jezi ya Yanga kisha aliniaga kuwa anaenda kutazama mpira wa yanga.
“Mida ya Mayele hiii, mwendo wa kutetema tuuu.
Mke wangu tutaonana baada ya mpira”
“Lakini baba Masoud mbona leo yanga hachezi?
.. Kwenye ratiba wameandika anacheza Simba na Azam, kwahiyo wewe yanga baki tu nyumbani”
“Aah kumbe anacheza Simba! Sio mbaya, ngoja nikawakere watani wangu”
“Mhh jamani sasa si bora ubaki tuangalie wote hapa hapa, kwani hicho king’amuzi cha Azam tumenunua cha kazi gani?”
“Mpira unanoga mkiwa wengi. Ngoja niende vibanda umiza huwa kunanoga sana”
Niliamua kumuacha aende. Alinipiga mabusu meengi, mabusu ya uongo na ukweli kisha aliondoka. Sasa baada ya kutoka nje kwa bahati mbaya alisahau kufunga mlango. Na kitumbo changu nilisimama nikiwa natabasam kisha nilitembea hadi mlangoni nikitaka kufunga mlango. Lakini kabla sijafunga mlango; macho yangu yaliganda kwenye gari ya mume wangu.
Akiwa amekaa kwenye siti ya mbele nilimuona akizungumza na mtu fulani, mara walikumbatiana kidogo kisha aliondoa gari.
Nilipata mawenge! Nilijiuliza mtu huyo ni nani?? Ni rafiki yake wanaenda kucheki mpira au ni mtu gani? Ni wa kike au wa kiume??. Sikutaka kukubali, nami nilitoka nje kisha niliita boda nilimuambia tuifuatilie gari ya mume wangu.
Safari ilianza, nilidhani ataelekea kwenye mabanda ya mpira lakini mabanda yote aliyapita, aliendesha gari hadi kwenye lodge iliyopo katikati ya mji. Presha yangu ilizidi kupanda, tumbo langu lilipanda joto! Nilihisi kuchanganyikiwa. Walizama na gari ndani ya lodge, mimi na boda boda tulipaki nje. Nilishuka kisha nilipiga hatua za haraka kuelekea ndani; kama mteja vile kumbe nilikuwa nina jambo langu.
Baada ya kuzama ndani nilikuta kashapaki gari kisha mume wangu alitoka nje, alizunguka
upande wa pili alimfungulia mlango mtu ambaye nilitamani kumfahamu. Licha ya kwamba nilisimama mbali lakini nilikuwa makini kwelikweli. Macho yangu yalitua kwa mwanamke ambaye alivaa mavazi ya kiislamu, kuanzia juu hadi chini, japo sikumuona vizuri lakini niliweza kumtambua kuwa mwanamke huyo ni Rahabu. Nikiwa bado nimezubaa mara walishikana mikono kisha walizama ndani kabisa ili wakafanye mambo yao. Aisee nilipagawa, nilivurugwa na nilichanganyikiwa sanaa!!
SEHEMU YA 43
“Dada unafanya nini hapa? Mbona kama unaichunguza sana lodge yetu? Wewe ni mwizi au?” ilikuwa ni sauti ya mlinzi.
“Nani mwizi? Nimekuibia nini?… ” “Sasa unafanya nini hapa?”
“Nilitaka niingie ndani nichukue room ila kuna kitu nimesahau nyumbani”
“Sawa, basi kama umefuata huduma naomba ingia ndani, lakini kama wewe sio mteja naomba ondoka”
Niliwaza kwa sekunde chache nizame ndani au niondoke?… Nilitamani niingie ndani ili nikakichafue huko huko chumbani, lakini nilikumbuka kuwa nje nilimuacha boda boda, kwa hasira na maumivu makubwa niliamua kuondoka, nilikaa kwenye boda kisha nilirudi nyumbani ambako nilifikia kitandani kisha nilianza kulia. Sikuamini kama Rahabu angeweza kuniibia mume wangu. Sikuamini kama naishi nyumba moja na adui yangu.
Nilikumbuka jinsi nilivyokuta boksa ya mume wangu chumbani kwa Rahabu, jinsi walivyokuwa wanafanya usafi pamoja, jinsi mume wangu alivyokuwa anakataa chakula changu kisha anakipenda cha Rahabu!! Aisee niliongeza kilio, nililia hadi nilijionea huruma.
Ilipita saa moja, saa mbili, hadi inafika saa tatu hakuna ambaye alitokea. Nilifuta machozi kisha nilienda kukaa sebuleni, nilitulia kimya nikitazama taarifa za habari.
Nikiwa nimeganda kwenye Tv mara mlango ulifunguliwa, nilidhani angeingia Rahabu lakini hakuwa yeye, alikuwa ni Mume wangu ambaye mkononi alibeba maua meengi, alinitazama usoni kisha alitabasam, alinifuata alinikumbatia kisha alinipiga mabusu ya tumboni, aliniwekea maua tumboni.
“Mke wangu kipenzi si unajua nakupenda sana, nimekuletea zawadi ya mauaa”
“Asante” Nilijibu kwa upole nikiwa sijachangamka, macho yangu bado yaliganda kwenye Tv.
“Vipi mbona kama una mawazo? Kuna tatizo au?”
“Wala hakuna tatizo, nipo kawaida tu”
“Au unahisi njaa? Kwani Rahabu bado hajapika? Yuko wapi aniletee chakula tule pamoja, mana nami nina njaa kali sana!! Hawa simba wameshinda wamenitia njaa. We Rahabu upo wapiii, ebu niletee chakula…… Mke wangu huyu Rahabu hanisikii au? Mbona haniletei chakula?”
“Rahabu? Kwani umemuona Rahabu hapa? Rahabu tangu alivyoenda sokoni, hajarudi”
“Hajarudi?…. Yaani masaa yote hayo bado hajarudi? Huyu ameanza kutupanda kichwani eeh!! Sasa leo atanikoma, nakwambia leo atarudi kwao. Hawezi kutuchezea akili sisi, anaaga anaenda sokoni kumbe anaenda kukutana na wanaume zake, anakukalisha na njaa mke wangu kipenzi ambaye umebeba mtoto wangu… Leo tutatambuana shenzi kabisa”
Mume wangu alikasirika kiasi kwamba alinichanganya. Nilijiuliza ina maana hajui lolote kuhusu Rahabu au ananizuga tu?. Kwa hasira
alianza kujizungusha ndani ya nyumba. Akiwa bado anajizugusha mara Rahabu aliingia akiwa amebeba kapu ambalo lilijaa vitu ambavyo alinunua. Baada ya Rahabu kuingia tu mume wangu alichomoa mkanda kutoka kwenye pensi ambalo alivaa, alimfuata Rahabu alianza kumtandika kwa mkanda. Walikimbizana hadi chumbani kwa Rahabu, kwa mbali nilisikia kilio kutoka chumbani, pia nilisikia puh! Tih! Pah!.
Walizidi kunichanganya, nilijiuliza hivi ni kweli wapo siriazi au ndo walitaka kuniaminisha kuwa hawakuwa pamoja?
Kule chumbani kipigo kiliendelea, pia kilio kiliendelea, niliona wanaweza kuuwana.
Nilisimama niliwafuata huko huko chumbani nilimkuta mume wangu akimtwanga mikanda Rahabu!!
“Mume wangu basi, ebu muache utamuumiza” niliingilia kati
“Hapana, huyu anataka kututawala, ngoja
nimfunze adabu mshenzi huyu”
“Shemeji nisamehe…. Kaka Nasri nisameheee mimi sitarudia tena…. Mi sikuwa kwa wanaume, nilipitia kwa rafiki yangu ambaye alinichelewesha…. Nisameheni jamani Dada
naomba nisaidie ataniua” Rahabu alilalamika.
Nilianza kumuonea huruma Rahabu, nilimshika mume wangu nilimvuta pembeni ili hasiendelee kutoa kipigo. Kwa hasira alifokafoka maneno mengi kisha aliondoka, nilibaki mimi na Rahabu, nilikaa kitandani kisha nilianza kumbembeleza hadi alitulia. Nilitamani nimuulize maswali mengi lakini sikujua nianzie wapi. Pia kutokana na kilichotokea nilishindwa kumuuliza kama yule niliyemuona lodge ni yeye au sio yeye.
Niliwaza nimuache, nimpotezee au nifanyaje?…
Niliona haiwezekani nimuache hivi hivi.
“Alafu mdogo wangu, hivi una uhakika kwamba ulikuwa kwa rafiki yako?”
“Ndiyo dada, nilivyofika kwao aliniambia
nimfumue nywele kisha nimsuke”
“Mh, mbona mimi nilikuona ukiingia lodge na shemeji yako?”
“Mimi? Uliniona mimi?” alishtuka alinikodolea macho
“Ndiyo. Kwani mimi wewe sikufahamu? Nakufahamu sana. Tena ulivaa hivi hivi, mavazi meusi na ushungi mweusi”
“Ah ah ah Dada nawe kwa kuchanganya mambo, hivi ukinitazama kichwani mimi nimevaa ushungi mweusi?” aliongea kwa kujiamini akiwa anacheka. Nilimtazama kichwani nilishagaa kuona amevaa ushungi mweupe badala ya mweusi.
“Mh! Ina maana yule niliyemuona sio wewe??… Niambie ukweli, isije ikawa unanizunguka kwa shemeji yako. Kama sio wewe basi samahani kwa kukufananisha, lakini kama ni wewe naomba acha mara moja kwa sababu nitakufanyia kitu kibaya.”
SEHEMU YA 44
“Dada huo wasiwasi wako tu. Kwanza mimi tangu nizaliwe hao wanaume wenyewe siwajui, na sitaki kuwajua, nasubiri siku nikiolewa ndio nianze mambo ya kikubwa. Yaani mimi na udogo huu, na wembamba huu nitembee na ule mwili wa shemeji kweli… “
“Basi mdogo wangu tusifike mbali, nisamehe. Nikutakie usiku mwema” Niliamua kufunga mjadala kisha nilielekea chumbani kwangu.
Nilimkuta mume wangu kashalala, tena kwa hasira alijifunika shuka hadi kichwani. Nami niliona bora nilale tu!! Nilipanda kitandani nilijilaza pembeni yake.
Macho yangu yaliganda kwake, nilitamani nimfunue shuka tuongee lakini niliogopa. Nilitamani nimkumbatie au nilale kifuani kwake lakini nilimuogopa. Kuna muda nilipandwa na hisia za mapenzi, ni muda mrefu sikufanya tendo hilo. Japo sikuruhusiwa kufanya lakini nilitamani kufanya hata kama huwa napata maumivu. Kwa hofu nilimfunua shuka mume
wangu, alikasirika aligeukia upande wa pili. Nilimsogelea kisha nilimkumbatia, nilimwambia kuwa nina hamu na yeye lakini alinisukuma, aliniambia kuwa amechoka na hajisikii kufanya tendo lolote. Hisia zangu zilikata pale pale, kwa uchungu nami nilijifunika shuka nililala.
*****
Kulikucha asubuhi, mume wangu alikuwa wa kwanza kuamka kisha alitoka nje. Mara nilimsikia akimkoromea Rahabu, alimfokea akimwambia afanye usafi vizuri, mara alimwambia hajui kudeki, ugomvi wao uliniweka njia panda. Kuna muda nilihisi nawasingizia lakini kuna muda niliona wananizuga tu.
Nilisubiri mume wangu aje ili nae nimuulize aniambie ukweli. Baada ya sekunde chache alirudi, alioga kisha alivaa nguo zake kwaajili ya kwenda kazini. Kabla hajaondoka nilimtwanga swali la kwanza.
“Hivi baba Masoud, una uhakika jana ulienda
mpirani kweli?” “Sasa nilienda wapi?”
“Mbona nilikuona ulienda lodge ukiwa na mwanamke? Tena mwanamke mwenyewe ni Rahabu”
“Aah nimekumbuka, si unamzungumzia yule dada aliyevaa mavazi meusi juu hadi chini?”
“Ndiyo”
“Yule sio Rahabu. Mke wangu nawe kumbe plag!! Kwanza ni kweli jana nilivyotoka hapa nilimchukua yule binti nilimpeleka lodge. Yule ni mke wa mtu, ni mke wa rafiki yangu. Nilimpa lift nilimpeleka lodge kisha nilimuacha nilirudi mpirani”
“Lakini mbona niliwaona mkiingia ndani mkiwa mmeshikana mikono? Na mlango wa gari ulimfungulia”
“Kwahiyo unataka kusema mimi natembea na mke wa rafiki yangu si ndio? Yaani kumfungulia
gari mwanamke ina maana unatoka nae si ndio? Alafu ukimshika mtu mkono alafu umsindiize ndani ya lodge ina maana unatoka nae au vipi?…. Sawa nashukuru kwa matusi yako…
Nashukuru sana… We leo si unaamua kunitukana kwamba natembea na wake za watu, sawa mama asante sana….” Alikasirika, alinung’unika kwa hasira
“Basi mume wangu nisamehe, ni wasiwasi wangu tu kwakuwa nakupenda”
“Kunipenda gani huko inafikia hatua unaniambia natoka na Rahabu?…. Huyu Rahabu nimemleta hapa mwenyewe akiwa kadogoo, amekuja hapa hata kuvaa hajui, namlea mwenyewe, kimtu chembamba, shingo ipo kule, kwa kipi alichonacho hadi nitoke nae? Rahabu amekuzidi nini wewe? Au kile kitako chake ndo kinipagawishe mimi? Hivi mke wangu unanichukuliaje?”
“Jamani baba Masoud si yameisha… Nisamehe
SEHEMU YA 45
basi mume wangu kipenzi”
Hakunijibu, aliondoka kwa hasira, nilibaki nimeganda tu, nilijilaumu kwanini nimemchokoza, bora hata ningetulia!!
Kitendo cha kuwahisi vibaya kilisababisha mabadiliko makubwa ndani ya nyumba. Kwanza mume wangu hakuelewana na Rahabu, muda mwingi walikuwa wanapishana tu bila hata kusalimiana. Pia hata kuhusu chakula, mume wangu alikataa vyakula vyote ambavyo vilipikwa na Rahabu. Alafu mwisho wa mwezi hakumlipa mshahara, alimwambia amlipi kama akitaka aondoke. Rahabu alibaki analia tu, alihuzunika lakini hakuondoka. Kuna siku walitibuana kuanzia asubuhi hadi jioni, walijibizana kwa maneno makali, ilifikia hatua ilibidi niingilie kati; niliwatuliza.
Ugomvi wao ulizidi kunithibitishia kwamba hawana mahusiano yoyote ya kimapenzi.
Angalau nilipata amani ya moyo!! Niliamini
kuwa hakuna wa kuniibia mume wangu kipenzi. Japo sikupenda ugomvi wao ila nilifurahi kuona hawaelewani hata kidogo, nilitamani bifu lao liendelee kila siku ili mume wangu anipende Mimi tu.
Siku zilisonga, mimba yangu ilifikisha miezi 6. Mume wangu alizidi kunipenda kiasi kwamba siku ya mpira hakwenda kwenye vibanda umiza, tuliangalizia nyumbani. Kila siku akitoka kazini alirudi moja kwa moja nyumbani. Hata simu yake hakuwa ananinyima kama zamani. Muda mwingi niliishika, nilisoma meseji zake, nae alisoma zangu, tuliaminiana sanaa!!
****
Baada ya ndoa yangu kutulia nakumbuka siku hiyo nikiwa dukani kwangu mara aliingia mkaka flani hivi mweusi, mrefu, ana mwili wastani.
Nilimkaribisha kama mteja lakini aliniambia kuwa yeye sio mteja ila ana mazungumzo na
Mimi.
“Naitwa Genson, kwanza nafurahi nimekukuta upo mwenyewe. Naomba utege sikio unisikilize” Mkaka aliniambia akiwa bado amesimama
“Sawa nakusikiliza, we ongea tu” Nilimjibu nikiwa na shauku ya kutaka kujua.
“Pole Dada” “Pole ya nini?”
“Mimi sio mfuatiliaji wa maisha ya watu lakini kwa muda mrefu nimejikuta nikianza kufuatilia maisha ya familia yako. Kwa akili yako unadhani unaishi kwa raha sana, unajiona ni mtawala wa Mali zako zote!! lakini ukweli ni kwamba unaishi kwenye Giza”
“Giza kivipi tena mbona unazidi kuniachanganya?”
“Naomba leo hii ukifika nyumbani kaage kwamba unasafiri unarudi kijijini kwaajili ya jambo fulani, waambie kuwa utakaa kijijini kwa
wiki moja. Licha ya kuaga lakini usiondoke. Tafuta sehemu jifiche, kesho usiku mida ya saa 1, mbili au tatu usiku hakikisha unarudi nyumbani pasipo wao kujua. Kwa namna yoyote ile ingia ndani kisha jifiche ndani pasipo wao kutambua. Ukifanya hivyo utanishukuru” Alimaliza kuongea kisha aliondoka.
INAENDELEA