MWANAUME WA NDOTO ZANGU
SEHEMU YA 11
Kitendo cha mimi kufeli hovyo kiliwasikitisha na kiliwakasirisha walimu, hawakupenda mwenendo wa masomo yangu kwa sababu shule ile ni kubwa na ilizoea kufaulisha kwa kiwangi cha juu. Walishangaa kuona sina akili.
Hapo sasa walianza kupambana na mimi, walinikomalia, walinibana sana, japo nilibadilika
kidogo lakini matokeo yangu hayakuridhisha.
Shule ile ilikuwa ina sheria zake, ili upande darasa linalofuata basi ni lazma ufaulu mitihani ya mwisho ya darasa ulilopo. Na ikitokea umefeli masomo yote, unafukuzwa kabisa.
Ikitokea umepa
ta four, unarudia darasa. Kwa bahati mbaya matokeo yangu ya kumalizia kidato cha tatu nilifeli, nilipata D 1 na F kama zote. Hapo sasa walimu walinichoka, mkuu wa shule hakupendezwa, ilibidi kaka Nasri aitwe ili aambiwe kuhusu matokeo yangu, niliogopa, nilitamani ardhi ititie kisha kihama kifike, niliwaza atayapokeaje matokeo yangu?
Akiambiwa nimefeli itakuwaje? Aisee nilivurugwa. Ni kweli kaka Nasri aliitwa kisha kikao kifupi kiliwekwa, mazungumzo yalikuwa kama ifuatavyo.
“Huyu binti ni mwanao?” mkuu wa shule alimuiliza kaka Nasri
“Hapana, ni mdogo wangu”
“Amefeli mitihani yake ya kidato cha tatu, amefeli kiasi kwamba tunamuogopa, huyu hafai kabisa kubaki hapa, hasije akaidhalilisha shule yetu. Hivyo basi kwa mujibu wa sheria; tunamfuta kwenye shule hii, na kuanzia leo Gensuda sio mwanafunzi wetu.”
Wee nilishtuka!! Mshtuko nilioupata ulifanya nizimie. Sikujua kilichofuata ila tu ghafla nilijikuta nipo hospitali. Nilizungusha macho sikumuona mtu hata mmoja. Niliinuka nilikaa kitandani kisha niliendelea kusubiri. Mara mlango ulifunguliwa, aliingia Matroni wa shule yetu akiwa ameongozana na Kaka Nasri; Nilimtazama kaka usoni nilimuona kavimba kwelikweli, alishindwa hata kunitazama usoni, moyoni nilisema kumekucha. Nilihisi huo ndio mwisho wangu wa masomo.
“Tayari ameamka, mizigo yake ile pale pembeni. Gensu ebu nenda kakague kama vitu vyako
vyote vipo kwenye begi.” Matroni aliniambia. Taratibu nilshuka chini nilielekea kwenye kona yaliko mabegi yangu. Nilikagua vitu vyangu vyote nilikuta vipo sawa.
“Vyote viko sawa?” Matroni aliendelea kuniuliza “Ndiyo”
“Sawa!! mimi naomba niwaage nirudi shule nikaendelee na majukumu yangu. Barua yake ya kufutwa shule hii hapa, niwatakie safari njema” Matroni aliongea akiwa anamkabidhi Kaka barua yangu ya kufutwa shule.
Matroni aligeuka nyuma aliondoka zake. Ndani ya chumba nilibaki mimi na Kaka, kwa mara ya kwanza aliinua uso alinipiga jicho lisilo na mchezo, uso wake ulikunja ndita za hasira.
Jamani niliogopa mimi hadi sio poa. Nilitamani nilie au nikimbie nikurupuke nitokomee vichakani. Kwa hasira hakufungua mdomo wake wala hakunipa ishara yoyote, aligeuka kisha alipiga hatua kuelekea nje. Niliona
nikizubaa naweza achwa kwenye mataa, fasta nilibeba mabegi yangu kisha nilimfuata, niliwaza nikamuombe msamaha, kama kunipiga makofi akanipige ilimradi tu hasira zake ziishe pia hasitufukuze nyumbani kwake.
Tulifika nje, nilimuona akiingia kwenye gari lake. Nami bila kuchelewa nilifungua mlango wa nyuma niliweka mabegi kisha nilizama ndani nilikaa. Nilidhani angeondoa gari lakini hakuondoka, alilala juu ya usukani wa gari yake, kitendo hicho kilifanya niamini kwamba ameumizwa sana na matokeo yangu ya kufeli.
“Kaka Nasri…” Nilimuita kwa upole lakini hakuitika wala hakunitazama. Aliendelea kulalia usukani, pia kwa mbali nilisikia kwikwi na pumzi za kilio, ghafla nilimuona akifuta machozi!!
Aisee nilichanganyikiwa mimi jamaniii.
“Ka-ka Nasri Ni-samehe…” Hapo sasa hata mimi niliongea nikiwa nalia
“Nimekosa mimi, nimekosa mimi, nimekosa
SEHEMU YA 12
sana” niliendelea kulalamika kwa uchungu
“Kaka… Nitazame basi hata kidogo. Mimi sio kwamba nilifeli makusudi, ni bahati mbaya tu. Changamoto nilizopitia kwenye maisha zilifanya nipoteze akili zangu za darasani, nilihisi elimu ni kama mzigo tu, wenzangu wakiwa wanasoma mimi niliwakimbia, darasani sikutaka kuwazingatia walimu, nilikuwa sijui nilitendalo, nilikuwa sijitambui, nilikuwa sielewi umuhimu wa ada zako, nilikuwa nachukulia kawaida tu, fikra zangu kielimu zilikuwa ndogo”
“Ina maana kwa sasa fikra zako ni kubwa? Unajitambua? Umeshajua umuhimu wa elimu?” aliniuliza pasipo kunitazama
“Ndiyo, sasa najua kwanini ulinipeleka shule. Pia sasa najua kwanini unaumia mimi kufeli. “
Baada ya jibu langu aliwasha gari kisha aliondoa kwa kasi ya ajabu. Moyoni niliwaza tuaelekea nyumbani lakini ghafla nilishangaa tunarudi shuleni. Sikujua tunaenda shule
kufanya nini, pia sikujua kama kaka Nasri amenisamehe au bado ana hasira na mimi. Sikutaka kumsemesha, nilimuacha tu nione kwanini tunarudi shule.
Baada ya dakika chache tulifika shuleni. Alipaki gari kisha tulishuka. Tulipiga hatua kuelekea ofisini kwa mwalimu mkuu. Mimi nilikaa nje kwenye benchi, Kaka alizama ndani kwa mkuu wa shule. Sijui walikuwa wanazungumza kuhusu kitu gani, ila tu mazungumzo yao yalianza saa 7 mchana hadi saa 11 jioni bado walikuwa wanaongea. Mida ya saa 12 walimaliza, hapo sasa nami niliitwa. Nilizama ndani niliwekwa katikati;
“Gensu” Mkuu wa shule aliniita “Abee”
“Mshukuru sana huyu kaka yako, anapambana sana kwaajili yako. Laiti kama isingekuwa huyu, laiti kama hasingekupigania, sidhani kama ungeendelea kubaki kwenye shule hii”
“Ina maana naendelea na masomo?” niliuliza nikiwa nimekodoa macho.
“Yeah. Kaka yako ameniambia kwamba una mzazi mmoja tu ambaye hajiwezi, ameniambia kwamba hana undugu na wewe lakini anakulea na anakusomesha kama mdogo wake. Anataka wewe ufanikiwe ili uje kumlea mama yako.
Huyu kaka yako muda huu ametoa zaidi ya million kutushawishi tukuache uendelee na kidato cha nne. Japo hairuhusiwi, japo hiyo ni kama rushwa lakini tumekubali sio kwa sababu ya fedha ila kwa sababu hata sisi tunakuonea huruma kutokana na hali ya umaskini katika familia yako. Hivyo basi tumekupatia nafasi nyingine, kwa sasa wenzio wanarudi likizo, wewe utabaki na wanafunzi wachache ambao wanaishi mbali, pia utabaki na wenzio ambao wamejiunga na tuition ya kidato cha nne. Kaka yako anaondoka, wewe utakuwa na sisi hapa… Ila tunataka usome”
“Sawa, nawaahidi kila mtihani wa kidato cha
nne nitakuwa mwanafuzi wa kwanza. Pia mtihani wa mwisho wa kidato cha nne nitapata division one”
“Woooow!!” Mkuu wa shule alihamaki kwa furaha, alitabasam kwa raha.
“Mbele ya mkuu wa shule, naahidi kama Gensu ataongoza mitihani na akipata division one; yeye na mama yake nitawajengea nyumba, nitamsomesha chuo na kuhusu ajira nitashughulikia mimi hadi aajiriwe” Hapo sasa kaka Nasri aliongea furaha za ajabu akiwa amesimama, alianza kujizungusha ndani ya ofisi akiwa anarukaruka.
SEHEMU YA 13
Mkuu wa shule alibaki amekenua meno tu, aliushangaa upendo wa Kaka Nasri juu yangu. Kiukweli kabisa katika hii dunia ni ngumu sana mtu baki kuwa na roho nzuri kama ya kaka Nasri. Watu wengi hawapendi mafanikio ya
wenzao. Sikuhizi hata ndugu wenyewe hawapendani, ukoo haupendani, familia nyingi hazipendani, lakini Kaka Nasri alikuwa ana roho ya pekeyake, alinipenda kama mdogo wake na kubwa zaidi alitamani sana nifanikiwe.
Baada ya kikao hicho mimi na kaka tulitoka nje tulielekea kwenye gari yake, nilichukua mabegi yangu, alichomoa wallet alitoa pesa za matumizi alinikabidhi, alinisisitiza nisome kwa bidii kisha tuliagana. Yeye alirudi nyumbani, mimi nilielekea hosteli.
*****
Hatimaye kwa mara nyingine nilianza maisha mapya shuleni. Kutokana na likizo tulibaki wanafunzi wachache, wengi walirudi nyumbani kwao. Kitu cha kwanza ambacho nilikifanya ni kutafuta marafiki wenye akili nyingi ili wawe wananifundisha. Pia nilitafuta wale wanaopenda kusoma mara kwa mara ili niwe nasoma nao. Nilihakikisha nasoma asubuhi,
mchana, jioni, usiku kabla ya kulala na alfajiri kuanzia saa 10 au 11. Masaa yangu ya kulala yalikuwa ni sita tu, kula chakula saa 1, masaa mengine yote ni kujisomea, kuingia kwenye vipindi vya tuition, kuingia library na mazoezi ya viungo muda ya jioni.
Mkuu wa shule hakuwa mbali na Mimi, pia aliwaambia walimu wanipe ushirikiano wa kutosha. Taratibu nilianza kubadilika, niliwaomba walimu wawe wananitungia mitihani yangu pekeyangu. Mwanzo nilipata 40 ya 100, 67 ya 100, 80 ya 100 na hatimaye
nilipata 100 ya 100.
Mtihani wa mwisho wa wanafunzi tuliokuwa tunasoma tuition, Mimi ndiye niliongoza.
Mwalimu mkuu alifurahi kiasi kwamba alitamani shule zifungue haraka ili aone kama nitaongoza darasa zima au lah. Wale wanafunzi waliokuwa wananifundisha mwisho wa siku walikuwa wananiomba niwafundishe. Nilianza kupata wafuasi kama wote, kila mtu alitamani
atengeneze urafiki na Mimi. Nilikiwa lulu kwao, hata baadhi ya wanafunzi wa vidato vya chini walikuwa wananiomba niwafundishe, niliwafundisha.
Muda wa kufungua shule ulifika, wanafunzi walirudi shuleni, baadhi walishangaa kunikuta, hasa hasa wale wenye akili walishtuka kuona kilaza nikiwa bize na masomo, alafu sikujali wala nini, nilikuwa bize na kutimiza malengo yangu.
“Mmh! Nyie huyu si alifeli huyu? Sasa mbona tumemkuta?” Wakali wa darasa walianza kunikalia vikao
“Eti alisamahewa”
“Kah hii shule nayo kumbe ina mambo ya ajabu, Tangu miaka ya zamani shule yetu haijawai kufelisha kidato cha NNE, ila mwaka huu naona huyu Gensu atatutia aibu”
“Umeona eeeh, eti mwanafunzi anapiga F-F-F-F, Huyo ni mwanafunzi au ushuzi, aondoke
akajambe mbele huko. Hasije akatutia gundu bure”
Walinisengenya pasipo kujua kwamba nimebadilika. Hawakujua kwamba nimepigwa tuition ya nguvu. Niliwacha waropoke, moyoni niliapa kwamba nitawakomesha. Masomo na vipindi rasmi vya kidato cha NNE vilianza.
Ulikuwa ni mwaka wa heka heka, kama mnavyojua kidato cha NNE, muda wote ni darasani tu, muda wote ni pilikapilika, Mara tuingia maabara (labalatory), Mara tuingie maktaba, hata muda wa michezo tulipunguziwa. Masuala ya mipira, debate, yalikuwa yanafanywa na vidato vya chini, sisi form four tuliwekwa kwenye kundi la watu wakubwa.
Mwezi wa kwanza ulikatika, mwezi wa tatu tulifanya mtihani wa kwanza ambao NILIONGOZA. Hapo sasa wengi walishtuka, wale waliokuwa wananisimanga walitengeneza makundi ya kunikomoa kimasomo, walishirikiana kimya kimya ili waniongoze lakini
SEHEMU YA 14
hata kwenye mitihani ya ngazi za wilaya niliwaongoza, Waliona cha kufia nini?
Waliungana na Mimi.
Ni mwaka mmoja ulitimia pasipo Mimi kurudi nyumbani wala kumuona mama yangu, nilimmiss sana. Pia ni miezi sita ilikatika pasipo kuonana na kaka Nasri, tangu sikuile ameniombea msamaha hakuwai kurudi tena, mara nyingi tulikuwa tunaongea kwenye simu, alinitumia pesa za matumizi, matokeo yangu aliyapata kupitia mwalimu mkuu, alifurahi sana kusikia kwamba mimi ndiye kiongozi wa mitihani yote ya kidato cha nne.
***
Hatimaye ulifika mwezi wa tano, mwezi ambao tulifanya mtihani wa Mock mkoa. Kwa upande wangu mitihani ilikuwa mirahisi sana, malengo yangu yalikuwa ni kuongoza mkoa mzima wa Tanga, hivyo basi nilikuwa makini sana katika
kujibu mitihani yangu. Mitihani ya Mock ilimalizika mwanzoni mwa mwezi wa sita. Na nakumbuka tulipewa likizo ya wiki 1 tu kisha tulitakiwa turudi shule kwaajili ya maandalizi ya mtihani wa mwisho wa kumaliza kidato cha nne (NECTA). Kwakuwa tulipewa muda mfupi wa mapumziko wenzangu wengi waliondoka haraka, kama kawaida shuleni nilibaki mimi na wengineo wachache ambao wanaishi mbali.
Kutokana na malengo ambayo nilijiwekea sikutaka kurudi nyumbani, nilitaka nitumie likizo hiyo fupi kwaajili ya kujisomea zaidi. Kule nyumbani Kaka Nasri alipata taarifa kwamba tumefunga shule. Bila kuchelewa alinipigia simu;
“Hallo mdogo wangu” “Naam kaka, shikamoo”
“Marahaba!! Naona mpo likizo, japo umetumiss lakini naomba husirudi nyumbani hadi umalize kidato cha nne. Mana huku mtaani sio kuzuri sana, fujo ni nyingi, unaweza ukaja alafu
ukajisahau bila kusoma, pia bora ukae huko ambako hakuna fujo za wanaume waharibifu”
“Sawa kaka nimekuelewa. Pia Mimi mwenyewe nimeamua nibaki huku nijisomee, si unajua kuwa nataka nongoze mtihani wa taifa”
“Wewe usiniambiee, yaani unataka uwe T.O (Tanzania one)?”
“Ndiyo kaka”
“Mungu akubariki sana Mdogo wangu, kama nilivyokuambia kwamba ikitokea umepata division one; nakununulia nyumba. Pia ukifaulu kidato cha sita nakupeleka chuo nje za nchi na kuhusu ajira yako Mimi ndiye nitasimamia”
“Sawa kaka. Pia msalimie mama na Rahabu, mwambie mama nampenda sana.”
“Mama yako anakusikia hapa, anasema amemiss kukuona. Ebu mtumie picha yako. Nenda pale ofisini kwa mwalimu mkuu, mwambie akupige picha ukiwa umevaa sare,
picha hiyo aitume kwenye WhatsApp yangu ili nimuonyeshe mama yako ambaye ni muda mrefu hajakuona”
“Sawa kaka, muda si mrefu mama ataiona picha yangu. Ila mwambie hasije akanishangaa mana nimebadilika sana, mwambie nimekuwa malkia wa shule ah ah ah” Niliwatania
“Ah ah ah! Ebu tutumie hiyo picha tukuone kwanza, isije ikawa umebongeka”
Tuliongea mambo mengi sana, pia niliongea na mama yangu, tulicheka, tulifurahi, na mwisho baada ya kukata simu nilienda ofisini kwa mwalimu mkuu, alinipiga picha nzuri kupitia simu yake ya IPHONE kisha alimtumia kaka Nasri kupitia WhatsApp. Baada ya kutuma picha hazikupita dakika nyingi mama yangu alinipigia, alinisifia kuwa nimekuwa mkubwa na nimekuwa nzuri kupita kiasi. Alinisisitiza niendelee kujitunza, nisikubali kurubuniwa na wanaume.
SEHEMU YA 15
“Huo uzuri wako usiufanye kama soko la kujipatia fedha kwa wanaume, utajiharibia sifa zako za kuolewa. Pia utatumika vibaya.
Naomba uniahidi kuwa hutojihusisha na wanaume hadi muda wa ndoa”
“Mh mama kwani una wasiwasi na Mimi?”
“Sio wasiwasi, naomba uapie… Apia kwa Mungu nikiwa nakusikia”
“Nakuahidi mama yangu, Mwenyezi Mungu akiwa ananisikia. Kama niliweza kujitunza katika kile kipindi cha shida, hakuna mwanaume atakayeweza kunirubuni wala kunilaghai, nitajitunza hadi nihitimu masomo yangu, nipate kazi, kisha nitaolewa”
“Wow mwanangu nikutakie masomo mema”
“Sawa mama, nakupenda mama yangu, tutakutana nikimaliza form four”
Sikuwa na mashaka juu ya hilo, kwa ufupi ni kwamba sikumuona mwanaume wa kuweza
kuniharibia maisha yangu, mwanaume huyo hayupo, hata kwa uchawi hawaniwezi. Baada ya kuongea na mama nilielekea hostel, nilikaa kitandani kisha nilianza kujisomea. Nilisoma nikiwa natabasam, upendo wa mama yangu ulifanya nivimbe!! Hata kama sikuwa na baba lakini uwepo wa mama kwangu ilikuwa raha tupu. Pia msaada wa kaka Nasri huo ndio ulinipa nguvu na confidence kama zote, nilisoma nikiwa nawaza kwamba hakuna wa kunibabaisha kifedha kwa sababu kaka Nasri yupo.
***
Kumbuka kwamba tulifunga shule kwa wiki moja tu. Siku ya kwanza ilipita, Siku ya pili ilipita, siku ya tatu ilisepa, zilibaki Siku NNE likizo iishe. Kwakuwa nilikuwa napenda kusoma niliona siku zinachelewa, nilitamani wanafunzi wenzangu warudi haraka ili tuanze maandalizi
ya NECTA. Sasa siku hiyo usiku, nikiwa nimelala, nikiwa sina hili wala lile mara kiswaswadu
changu kiliita. Kwenye simu yangu kuna namba za watu wanne tu. Mama, kaka Nasri, mwalimu mkuu na Rahabu. Sikujua kati yao ni nani amenipigia, niliamka kutoka usingizini, nilichukua simu nilitazama nilikuta ni KAKA NASRI, fasta nilipokea;
“Hallo kaka, samahani nimechelewa kupokea, nililala”
“Ooh usijali, pia nisamehe nimekuharibia usingizi wako”
“Haina shida kaka….” Nilitaka niendelee kuongea ila sikujua naongea nini. bila shaka nilitaka nimuulize kwanini amenipigia usiku wa manane. Sio kawaida yake. Hata hivyo niliogopa kumuiliza. Wote wawili tulikaa kimya, nilishangaa kuona haongei chochote, simu ilikuwa hewani, nilisubiri sana lakini hakuongea kitu.
“Kaka..” “Kakaa”
“Kaka Nasri”
“Naam… Naam… Mzima wewe lakini”
“Ndiyo, Mimi ni mzima, naendelea vizuri, pia najiandaa na mitihani ya mwisho”
“Sawa ni vizuri… Lakini Gensu..” “Abee kaka”
“Hivi ile picha uliyoituma ni yako kweli au ulidownlod google?”
INAENDELEA