NEBUKADNEZA: MBABE WA VITA, MUABUDU SANAMU ALIYEKULA MAJANI KAMA NG’OMBE
Kuna huyu mwamba wa kuitwa Nebukadneza. Unapowazungumzia wafalme waliokuwa na nguvu kubwa, basi bila shaka hutoweza kulisahau jina la mwamba mmoja hivi wa kuitwa Nebukadneza.
Huyu jamaa alikuwa mtawala kipindi kile cha akina Daniel. Nenda kasome Daniel sura ya 1 mpaka ya 4, imemuelezea sana mfalme huyu kwa namna alivyokuwa na nguvu, Mungu alikuwa anamuonyesha mambo yajayo kwa kupitia ndoto, halafu Daniel ndiye akawa mtafsiri.
Tuje sasa. Huyu jamaa ametoka wapi?
Baba wa mfalme huyu aliitwa Nabopolaan. Huyu alikuwa mfalme wa 65 wa nchi iitwayo Babiloni ambayo ilikuwa na mji wake uitwao Babiloni. Sasa miaka hiyo mfalme huyu alikuwa kwenye mapigano makali ya Misri, kwa nini? Walikuwa wanagombania milki ya Ashuru, yaani kama leo hii Morocco na Algeria wasivyopatana kisa tu kuna maeneo Morocco anayatawala kimabavu na Algeria wakiamini hayo ni maeneo yao.
Sasa baba yake alipofariki dunia, Nebukadneza akaanza kutawala Babiloni na kuingia kwenye vita yake ya kwanza na Misri, vita hivyo vilikwenda kupiganiwa huko Eufrate katika utawala wa mwisho wa baba yake, hiyo ilikuwa ni mwaka 605 Kabla ya Kristo.
Wakati huo Misri ilikuwa na mfalme wao, Farao-Neto lakini alijikuta yeye na majeshi yake wakiangukia pua kwa kuchakazwa vibaya sana na Babiloni.
Hiyo vita haikupiganiwa Eufrate tu bali walihama na kwenda kupigania sehemu nyingine iitwayo Karkemishi katika mto Eufrate. Unaweza kusoma kitabu cha Yeremia 46:2.
Sasa hapa nakupa mambo mawili, historia kulingana na Biblia, halafu historia kulingana na vitabu vya darasani. Hapa inabidi nicheze kotekote ili muelewe vizuri.
Sasa kwa nini Babiloni iliamua kumpiga Misri? Hii ilikuwa ni adhabu ya Mungu, yaani aliona kulikuwa na maovu mengi sana Misri (Hawa jamaa wamepinda tangu zamani), akaamua kumpeleka Nebukadneza kwenda kupigana huko. Soma Yeremia kuanzia sura ya 46.
Lakini sababu ya pili ni kwamba Misri aliitaka miji ya Shamu na Palestina, kwa nini? Miji hiyo ilikuwa karibu na Babiloni na kwa sababu waliona majamaa wanaitawala dunia, basi ingekuwa kazi nyepesi sana kupambana nao kama tu wangeipata miji hiyo.
Sasa naye Babiloni hawakutaka kuona hilo linatokea. Wakapambana vilivyo mpaka kushinda vita hivyo. Wakati Nebukadneza anapambana kwenye vita ndipo akapokea taarifa kwamba mshua wake amekufa hivyo ilikuwa ni lazima kurudi nyumbani na kusimikwa kuwa mfalme.
Nebukadneza alikuwa mjanja sana. Yaani alikuwa akipambana na Wamisri ili wasichukue Palestina na Shamu lakini wakati huohuo alikuwa akipigana na watu wa mji huo ili awatawale.
Alifanikiwa kwa kiasi kikubwa sana, na baada ya hapo, sasa akaamua kwenda huko Yuda ili kupigana na mfalme Yehoyakimu. Unaposema taifa la Yuda, inamaana ya Israel. Akaona hiyo haitoshi, akaufuata mji wa Siria (Syria) na kuupiga na miaka minne baadaye akarudi kupigana na Wamisri.
Hii vita hakushinda, na hata Wamisri hawakushinda. Sasa hilo likawapa viburi watu wengine na kuona mbona kama na sisi tunamuweza jamaa? Kwa nini tusimfuate na kumkung’uta?
Mtu wa kwanza kuwa kimbelembele na kuonyeshwa mfano alikuwa Yuda (Israel) alipoleta kukukakara zake, akapigwa vibaya mno na wakamteka mfalme Yehoyakimu, halafu pale akampandikiza mfalme aliyemtaka yeye aliyeitwa Sedekia. Najua kwa Wakristo hata majina si mageni kwenu.
Miaka ilikwenda mbele, mataifa yalitaka kujitoa katika utawala wa Babeli lakini walishindwa kwa sababu majamaa walikuwa hatari wa vita.
Watu wakapitisha ndogondogo kwa mfalme wa Yuda, Sedekia na kumwambia mbona alijisahau? Kwa nini ulipe ushuru mkubwa kwa Babeli na wakati hata wewe unaweza kujinasua! Sedekia akaona poa, acha nimtwange, kuingia vitani tu, akapigwa yeye.
Mji wa Yerusalemu ukawa under attack, jamaa akaingia hekaluni, akachukua vyombo vya dhahabu vya humo ambavyo Wayuda walikuwa wakivitumia kwenye ibada zao (Hivi vyombo vilimletea shida sana mfalme Belshaza ambaye ni mtoto wa Nebukadneza). Akawateka watu, akamuua Sedekia, halafu nchi ya Yuda akaifanya kuwa mkoa na si nchi tena.
Sasa miongoni mwa mateka waliochukuliwa ndiyo walikuwepo akina Daniel, Shadraki na Abedenego
Sijui unapata picha hapo.
Yaani ukisoma Bible, halafu ukasoma na haya masomo ya darasani ya historia, unaanza kupata mambo mengi zaidi.
Tuendelee.
Baada ya Mfalme Sedekia kuuawa, sasa Yehoyakimu akachukua nafasi hiyo ya kuiongoza Yuda (Israel). Hapa kuna kitu ambacho watu wanatakiwa kufahamu. Tuliona kulikuwa na mataifa mengine yaliyokuwa yakipingana na Babiloni chini ya Nebukadneza.
Mataifa hayo yalikuwa mengi lakini yakiwemo Syria na Palestina. So hapo unaona kulikuwa na nchi iitwayo Palestina na pia kulikuwa n Yuda ambao ndiyo Waisrael. Na wote hao walikung’utwa na Nebukadneza na kufanywa mateka.
Hapa naomba nifafanue kitu. Kama nilivyowaambia huko nyuma kwamba Nabii Issa siyo Yesu, Abraham wa kwenye Biblia si wa kwenye Kurani. Hao ni watu tofauti kabisa kwa sababu Nabii Issa hakufa msalabani, Yesu alikufa msalabani. Abraham wa kwenye Kurani ana baba mwingine na wa kwenye Biblia ana baba mwingine. So tukiwazungumzia hawa watu, tujue tunawazungumzia watu tofauti.
Hiyo napo imetokeza kwa Nebukadneza. Ukisoma kitabu cha Biblia na vya historia vingine vimemtambua kama Nebukadneza lakini ukisoma vitabu vingine vya dini, kuna mtu anajulikana kama Nabonido. Sasa wengi wanahisi kwamba huyu Nabonido ndiye Nebukadneza, hapana. Ni watu wawili tofauti waliokuwa na maisha ya kufanana tu.
Nebukadneza alikuwa mbabe wa vita, baada ya kuona ameishambulia Yuda, Palestina, Syria na mataifa mengine, sasa akaondoka na kwenda kupigana vita na mfalme Tiro huko Foenike. Vita hivyo vilipiganwa kwa miaka 13 (Soma kitabu cha Ezekiel 29:18 wamemzungumzia sana Tiro mpaka kupigwa kwake na Nebukadneza).
Hapa najua unaweza kujiuliza kwamba kwa nini huyu Nebukadneza alikuwa na nguvu kubwa? Jibu ni moja tu kwamba Yuda walikuwa wanaadhibiwa kwa mambo yote waliyokuwa wameyafanya.
Kulikuwa na sababu zilizomfanya Mungu kuwaadhibu kupitia Nebukadneza. Kwanza ilikuwa ni kutokumuamini tena yeye, watu wakachonga masanamu na kuanza kuyaabudu.
Ngono ikasambaa kila kona, yaani watu walikuwa wakizini mpaka vibarazani, watu walifanya uzinzi mpaka na ndugu zao. Pia watu waliwafanyia matambiko watoto wao wa kuwazaa, kwa hiyo Yuda na Samaria zote zikanajisiwa, sasa Mungu akamuinua Nebukadneza ili kuwaadhibu.
Nebukadneza ambaye alitoka katika taifa la waabudu masanamu, akawa na nguvu kubwa kuliko hata Yuda.
Ukisoma Biblia hasa kitabu cha Ezekiel, ni kama kwa kipindi hiki silaha kubwa ya Mungu dhidi ya mataifa mengine yalikuwa ni Nebukadneza! Kwa nini? Sababu ni kwamba Tiro alipigwa kwa kuwa tu waliucheka mji wa Yerusalemu.
Waliukejeli mji ule, waliutolea maneno machafu na hivyo Mungu akampa roho Nebikadneza kuona ni sahihi kwenda kupambana na Tiro. Haikuwa vita ya kawaida, ilidumu kwa miaka hiyo 13.
Huyu Nebukadneza, kutokana na maguvu aliyokuwa amepewa na Mungu, hata naye alimuita mfalme wa wafalme, mfalme aliyetawala watu mpaka wanyama.
Ukiachana na hayo kama nchi lakini pia huyu mfalme Tiro alikuwa na makosa yake kemkem, soma Ezekiel 28. Alilaaniwa na kuambiwa angepigwa sana mpaka kusikia aibu. Mwisho wa vita, mfalme huyo alitekwa na kuuawa mbele za watu, kilikuwa ni kifo cha aibu sana kwa mfalme.
Nebukadneza alijulikana kama mfalme mwenye nguvu, aliijenga Babiloni kwa kutumia kodi za mataifa ambayo yalikuwa chini yake yakiwemo Yuda na Palestina.
Alirudisha na kukarabati mahekalu ya kale katika majiji ya Babuloni ili kupata utegemezo wa makuhani wa Babiloni. Pia alitayarisha umwagiliaji wa kawaida wa nchi za Babiloni kupitia mtandao mzima wa mifereji iliyounganishwa na Eufrati. Katika utawala wake ufalme wa Babeli mamboleo ulifikia kilele cha ukuu wake.
Katika vitabu vingine vya historia vilimtaja Nebukadneza kuwa katili kupitilia. Alikuwa anamchukua sungura, anamchuna ngozi na kumla hivyohivyo akiwa na uhai wake.
Ukiachana na hilo, pia zile falme ambazo alizitawala, aliwalazimisha wafalme kuwa machoko. Watawala wa Kirumi kama Tito na wengine walijikuta wakiingia katika suala lake hilo la uchoko.
Pamoja na kuweka wafalme wengi na kuwamaliza, pia mwisho wa siku akaamua kumuua mfalme wa Yuda, Yehoyakimu na mwili wake kuwatupia mbwa.
Hayo yote aliona kama hayatoshi, akawalazimisha watu wamuite Mungu. Wakati akimuweka Sedekia kuwa mfalme wa Yuda, aliwataka wafalme watano wawe chini ya Sedekia. Kuna kipindi wafalme hao walipanga njama za kummaliza Nebukadneza lakini walishindwa kwa kuwa Sedekia alikwenda kuwachoma kwa Nebukadneza.
Kwa hasira, akawachukua wafalme hao watano na kuzifunga nywele zao kwenye mikia ya farasi na kuwaamuru wakimbie kutoka Yuda mpaka Lida, umbali wa zaidi ya kilometa 35.
Pamoja na ujinga wake mwingi lakini Nebukadneza alikuwa akiwaheshimu Wayahudi kwa kuwa aliamini Mungu wao alikuwa wa kweli.
Aliwachukua Daniel, Shadraki na Abednego kwa kuwa alitambua nguvu za Mungu wao, akawaweka karibu naye kwa ajili ya kutafsiri ndoto na maono yake.
Alipewa nguvu na kila kitu ila siku moja baada ya kukaa katika paa la nyumba yake, aliiangalia Babiloni jinsi ilivyopendeza, hapo akajisifia, akasema utukufu wote na uwe kwake. Hilo likamkasirisha Mungu na hivyo kumtupa mbali kabisa, akakosa watu, akaishi porini na kuanza kula majani kama ng’ombe kwa miaka saba.
Baadaye akaangalia mbinguni, kwa mara ya kwanza akamuomba Mungu wa kweli, hiyo ikawa almanusura yake, akarudishwa na kuendelea na maisha yake kama kawaida.
Hakuna marefu yasiyo na ncha. Wanajeshi wa Babiloni wakapigwa na Euphrates huko Zazana. Nebukadneza akakimbia kurudi Babiloni na baadhi ya wanajeshi wake. Huko, akakutana na mtu aitwaye Darius ambaye akamteka na kumchinja kama kuku.
Ukawa mwisho wake. Alikufa akiwa anamjua Mungu wa kweli ni yupi baada ya kuabudu sana masanamu.
Habari yake zaidi inapatikana kwenye kitabu cha Daniel na Ezekiel.