NILIKATAA KUBAKWA, WAKANISHUSHA PORINI, NIKALIWA NA FISI
Mkasa Wa Kweli
Chanzo: BBC
Irene Mbithe mwenye umri wa miaka 27 ni mtoto wa kwanza kati ya watoto sita katika familia yake kutoka Machakos.
Irene ni mmoja wa wale ambao maisha yao yalivurugika alipovamiwa na fisi, ambapo anasimulia jinsi alivyopoteza mkono wake, na jicho katika shambulio baya baada ya madereva wa lori kumshukisha njiani usiku wa manane katika hifadhi ya mbuga ya wanyama alipokataa wamnyanyase kingono.
Wakati huo alikuwa na umri wa miaka 19 na maisha magumu ya nyumbani yalimlazimu kuanza kutafuta ajira na mapema ili awasaidie wazazi wake. Alifanikiwa kupata ajira ya kuuza vitabu.
Lakini baada ya siku kadhaa muajiri wake alimuitisha kitambulisho chake cha kitaifa ambacho hakuwa amejisajili, na kwa sababu ya usalama na kutaka uaminifu wa kazi, muajiri wake Irene alimtuma kurejea nyumbani ili amletee kitambulisho cha mzazi wake.

Irene alisema aliondoka bila muajiri wake kumpa nauli na alipofika njiani na kupumzika kando ya barabara kabla ya kumuomba msaada wa kumbeba na gari mtu asiyemfahamu baada ya kumsimulia masaibu yake ili pate kurudi nyumbani kwao machakos.
“Wakati wa safari, mmoja wa madereva aliniomba nimpe chupa ya maji iliyokuwa pembeni mwangu. Nilimpa maji na kisha akaniomba ninywe maji pia nipunguze uchovu, baada ya kunywa mara moja nikalala,” alisema Irene.
Alilala usingizi mnono na alipoamshwa alikuwa amefika mjini Mombasa badala ya machakosa nyumbani kwao.
Aliposhukishwa Mombasa na dereva wa lorry kumuacha mjini humo ilimlazimu atafute tena gari ya kurudi Machakos na hapo ndipo wasamaria wema walimuombea usaidizi wakati wa saa kumi na mbili jioni.
Waliposafiri kwa saa kadhaa na madereva wa lorry , walisimama kupata chakula cha jioni na kisha baadaye safari ilipoendelea walitaka kumnyanyasa kingono. Irene alipokataa na kuonyesha uwoga mwingi dereva alimpiga.
Katikati ya usiku wenye kiza, walimshukisha na kumtupia mzigo wake njiani na kuondoka. Hapa ndipo Irene Mbithe alipokutana ana kwa ana na fisi aliyemshambulia vibaya, kwa kumtafuna uso upande wa kushoto na kumsababishia ulemavu wa jicho moja ambalo mpaka sasa halioni.
Alipokuwa akishambuliwa na fisi huyo mwanamume mmoja aliyekuwa akipita na gari na kushuhudia hilo alijaribu kumuokoa kwa kupiga honi na kusogea karibu ili fisi amuachilie lakini kwa hasira fisi alimmburuta hadi kichakani na kumtafuna mkono mara tatu huku akisikia lakini alikuwa hana tena nguvu za kupigana na mnyama huyo.
Msamaria mwema huyo alirudi nyuma na akaelekea katika eneo moja ambalo alikuwa amwewaona maafisa wa polisi maili kadhaa kutoka hapo ili wamsaidie Irene.
“ghafla niliskia risasi ikipigwa hewani – risasi iliomshutua fisi na kuniacha na kukimbia” Irene alisema.
Polisi walipofika walijua wazi Irene amefariki kutokana na jinsi hali yake ilivyokuwa. na kuamua kuwapigia simu wahudumu wa shirika la wanyama pori KWS ili waje kuchukua mwili wake.
KWS walipofika walimchukua Irene na kumuweka kwenye kitanda ili wampeleke kwenye chumba cha kuhifadhi maiti na katika harakati za kumfunga funga walimfinya tumbo, akatapika damu iliokuwa imekwama mdomoni na iliokuwa ikimzuia kupumua vizuri.
Na hapo ndipo alikohoa na kutambulika kuwa hajafa, akakimbizwa katika hospitali ya makindu na kisha hospitali ya machakos level 5 ambapo alikopokea matibabu na kusalia huko kwa miezi minne.
Irene alishindwa kujizuia na hisia alipokuwa akisimulia kilichomtokea usiku ule wa giza totoro tarehe 3 mwezi wa 8 mwaka wa 2018 ambapo maisha yake yote yalibadilika na kumwacha na maumivu ya kimwili, kihisia pamoja na ulemavu wa maisha.
Irene Mbithe alipoteza mboni ya jicho la kushoto, na kupata alama za mikwaruzo kwenye kifua chake upande wa kushoto. Vilevile alikatwa mkono wa kushoto mbali na kupata alama za mikwaruzo kwenye miguu yote miwili.
“Nimewasamehe madereva wa lori walioniacha njiani usiku wa manane, nimewaachia Mungu awalipe” alisema Irene kwa huzuni na uchungu mwingi.
Licha ya tukio hilo kubadilisha maisha yake kwa kiasi kikubwa ameendelea kuwapa wanawake wanaopitia changamoto ya aina yoyote moyo wa kuendelea na maisha na kutokata tamaa na kubwa kabisa kujkubali kwani kufanya hivyo kunarahisisha safari ya uponaji.