BIBI HARUSI KIKOJOZI
Salvatory alikuwa akikatiza kwenye Korido ndefu ya bweni la Mango,shule ya sekondari ya watakatifu Rufino na Rinaldo iliyoko wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma.Alisimama ghafla,uso wake ulimvimba kwa gadhabu.Jasho jembamba lilimchuruzika katika paji lake la uso,japo hakukuwa na joto kali kiasi la kusababisha jasho kumtiririka usoni kama bomba la kijiji.Chanzo cha yote hayo!Ni hasira alizonazo dhidi ya kijana aliyekuwa amekutana naye uso kwa uso koridoni.
“Nimetoka chumbani sasa hivi,lakini haujanifulia shuka langu moja!Una akili kweli wewe?”
“Hapana kaka,sio kwamba sikufulii.Nilichukua shuka lako moja nikufulie,halafu lingine nimalizie muda huu maana hata mimi nilikuwa na lundo la nguo zangu nyingi.Hivyo basi sasa hivi ndiyo naenda kulichukua nikalifue,nisamehe sana kaka!”Kijana yule mwenye umri mkubwa takribani miaka ishirini alijitetea.
“Nikusamehe nini!.Kwanini ulinikojolea?Hebu toa uso wako boya wewe,kubwa zima linajikojolea si useng* huo.Sitakusamehe mpaka naingia kaburini…”Salvatory alifoka,akamtukana matusi ya kila aina kijana pekee mwenye umri mkubwa shuleni hapo.Salvatory alikuwa na kila sababu ya kumuita kaka kijana huyo kwani ndio kwanza alikuwa na miaka kumi na saba,lakini hakufanya hivyo na aliapa kutofanya hivyo mpaka watakapo maliza shule na kuondoka shuleni hapo.Hakumuona kijana yule kama kaka yake bali kikojozi mkubwa sana duniani tena wa kimataifa!
Robinsoni alibaki mnyonge sana,chozi lilimdondoka.Akaanza kujuta na kumlaumu Mungu kwa jinsi alivyomuumba.Alijiona tofauti sana na wenzake na hakujua chanzo cha yote ni nini.Wazazi wake walimpeleka hospitali za kila aina,walitumia miti shamba ya kila aina na isitoshe walimpeleka mpaka Kanisani kuombewa lakini tabia yake ya kujikojolea ilibaki palepale.Tangu azaliwe mpaka umri huu wa miaka ishirini alikuwa bado anajikojolea kitandani jambo ambalo lilimgombanisha na wanafunzi wenzake walioishi chumba kimoja kipindi chote cha masomo ya sekondari.
“Mungu nimekukosea nini mimi?Kwanini najikojolea?”Tangu utoto wangu mpaka sasa mimi ni kijana mkubwa,tafadhari nakuomba Mungu fanya kila njia nisizeeke na kufa katika mateso haya.Niko chini ya miguu yako nakuomba uniondolee aibu hii….”Robinsoni alipiga magoti huku akilia,aliivua rozali yake na kufanya sala fupi lakini hakuna aliyemjali na huzuni yake.Kila mwanafunzi alimpita na kumuona mtu asiyefaa shuleni hapo kwani aliyafanya mabweni yao ya kiume kunuka mikojo jambo ambalo lilipelekea bweni lao liwe la mwisho kila shindano la usafi mabwenini liwekwapo mezani.Aliwatia sana aibu,walimchukia sana..
Hakuliona kosa lake la kumkojolea Salvatory usiku uliopita kwani Salvatory ndiye aliyemuomba Robinsoni alale kitanda chake cha juu na yeye ashushe godoro lake kitanda cha chini.Licha ya Robinsoni kukataa katu katu kutokana na hali yake hiyo lakini Salvatoiry alimbembeleza sana na kujikuta anakubali.Wakabadirishana,Salvatory akashusha godoro lake kitanda cha chini baada ya kukisafisha na kukipulizia pafyumu kuhakikisha hakinuki mikojo na Robinsoni akahamishia godoro lake kitanda cha juu.Wasomi wanakwambia Vice Versa is true!.Yaliyomkuta Salvatory akiwa amelala Mungu ndiye anajua,akiwa katikati ya usingizi mzito.Alihisi kinywaji cha moto chenye radha ya chumvi chumvi kikipenya taratibu katika mdomo wake.Mwanzoni alihisi alikuwa ndotoni kumbe sivyo!Alikuwa akinywa mkojo wa Robinsoni kutoka kitanda cha juu ambao ulikuwa ukidondoka matone matone kama hautaki vile kumbe ndo hivyoo kuna mtu alikuwa anakipata cha mtema kuni.Salvatory alikurupuka kitandani kama mwendawazimu,nguo zake zililowa kama vile amenyeshewa na mnvua.Hakuna aliyemuhurumia zaidi ya kumcheka tu na kumkejeli baada ya wote kustushwa na kelele zake,isipokuwa Robinsoni aliyekuwa akiomba msamaha huku akilia.Tabia yake hiyo ya kujikojolea ilimfanya siku zote ajidharau na kujiona hana thamani mbele ya mtu yoyote yule duniani.
Akiwa anayakumbuka yote yaliyopita usiku,alisimama mahali alipokuwa amepiga magoti koridoni,akaelekea chumbani kuchukua shuka la Salvatory ili aweze kulifua na kulisafisha jina lake mbele ya mwanafunzi mwenzake huyo wa kidato cha nne.Baada ya kufanya yote hayo,alienda kwa Salvatory,Robinsoni akapiga magoti na kuomba msamaha lakini hakuna kilichobadilika.Aliapa katu katu kutomsamehe mpaka anaingia kaburini.
BAADA YA KUMALIZA SHULE.
Salvatory alikuwa ameketi sebuleni pamoja na mchumba wake Joanitha majira ya saa mbili usiku.Alimpenda sana Joanitha msichana pekee aliyetokea kuzishikilia hisia za moyo wake.Weupe wake wa Kinyaturu kutokea kule Singida uliong’arishwa kwa mafuta ya Alizeti ulimfanya Joanitha aonekane mzuri na mrembo mithili ya Malaika mbele ya macho ya Salvatory.Salvatory hakusema chochote mbele ya Joanitha,kama kupatikana alikuwa amepatikana kwelikweli na kama kunasa basi alikuwa amenaswa kama vile vipande vya chuma visogezwapo karibu na Sumaku.
“Joanitha ameshakufanya taahira.Siku ukimuoa nazani hatafanya chochote kile!Kwa jinsi unavyompenda basi hata nguo za ndani utamfulia.Si hivyo tu hata maji ya kuoga utamchemshia,wewe utakuwa kama vile ndio umeolewa na si yeye.”Salvatory alicheka sana baada ya kukumbuka maeneno ya rafiki yake kipenzi na mfanyabiashara mkubwa wa Kitanzania anayeishi kule Uingereza,bwana Hakika Jonathan.Maneno hayo aliambiwa pale tu alipompelekea kadi ya harusi na kumwelezea hisia zake alizonazo juu ya msichana huyo ambaye walikuwa wanatarajia kufunga ndoa hivi karibuni.Hawakuwahi kugusana,hata busu hawajawahi kupigana huku kila mmoja akimuahidi mwenzake usiku baada ya kufunga ndoa basi watafanya kila kitu ambacho walipaswa kufanya kama wanandoa.Licha ya uhunu wa Salvatory,aliahidi kuvumilia kutolionja tunda la katikati kama vijana wa sasa wanavyoliiita mpaka siku ya harusi yao.
Sasa ulikuwa ni usiku wa mwisho kabla ya harusi yao,siku inayofuata Salvatory na Joanitha wangefunga pingu zao za maisha na kuanza kuishi kama mke na mme.Joanitha ilibidi afike nyumbani kwa mchumba wake huyo ili wamalizie kuzungumza kuhusu mipango ya mavazi yao siku ya harusi wakiwa wamebakiwa na masaa takribani kumi na manne tu.Wakiwa katikati ya mazungumzo mvua kubwa ilianza kunyesha,radi zikapiga,upepo mkali ukavuma.Haikuwa mnvua ya mchezo mchezo kwani ilisheheni upepo mkali pamoja na barafu iliyotanda angani.Baridi hiyo ilisababisha baridi kali sana,baridi ambayo ilisababisha kila mmoja atetemeke.Licha ya kufunga madirisha,kuvaa makoti lakini baridi iliendelea kuwaadhibu vikali sana.Katika harakati za kujinasua katika baridi kali,walijikuta wamekumbatiana na kutupana kwenye sofa.Salvatory hakuwaza kingine bali ngono tu!Alijitahidi kutumia nguvu zake na ujanja wake kama mwanaume lakini Joanitha hakuwa tayari tunda lake la katikati kuliwa kabla ya ndoa.Alikuwa mwanamke mwenye msimamo kwelikweli.Kwa vile Salvatory alikuwa amekufa ameoza,ilibidi avumilie kwani siku moja haikuwa kubwa sana kuvumilia.Ikabidi avumilie.Mvua iliendelea kunyesha,Joanitha alisubili ikatike arudi nyumbani lakini haikuwezekana na wote kwa pamoja walijikuta wakipitiwa na usingizi mzito sana.Wote kwa pamoja wakakoroma kama ng’ombe huku wakiwa wamekumbatiana juu ya sofa sebuleni kwa Salvatory..
Hatimaye kulipambazuka,jua lilichomoza,siku mpya ilikuwa imeanza.Salvatory aliamka kutoka usingizini,harufu kali ya mkojo iliyopenya katika matundu mawili ya pua yake ndiyo iliyomuamsha kutoka usingizini.Hakuamini alichokiona,mkojo ulikuwa umetapakaa sebuleni.Haukutokea sehemu yoyote ile bali kwa Joanitha,msichana pakee aliyezigusa hisia za Salvatory.Sketi ya Joanitha ilikuwa imelowa,jambo ambalo lilipelekea anuke mikojo kama choo cha stendi au sokoni.Salvatory hakuamini alichokiona,ama kweli malipo ni hapa hapa duniani.Siku zote aliwacheka sana vikojozi,hakujua kwamba mtu kukojoa ukubwani wakati mwingine ni ugonjwa na hakuna anayepinda hali hiyo.Yeye aliwachukia sana watu hao,jambo la ajabu alishindwa kumsamehe hata Robinsoni waliyekuwa wakisoma naye sekondari kule Kigoma miaka mingi iliyopita.Salvatory alikumbuka kila kitu na kujikuta akianza kulia kwa kwikwi.
“Mungu najua una makusudi na mimi!Nampenda sana Joanitha,siwezi kumuacha na nitahakikisha mpaka anapona,nitafanya kila njia mpaka aepuke aibu hii.Nampenda sana Joanitha siwezi kumuachaa!Robinsoni popote ulipo nimekusamehe na nina juta kauli yangu niliyokutamkia miaka mingi iliyopita. Leo hii Mungu ameniadhibu kwa matendo na kauli yangu dhidi yako.Nimekusamehe Robsinsoni..”Salvatory alilia sana huku akimkumbatia mchumba wake Joanitha,Joanitha akakubali kukumbatiwa kwa aibu baada ya kugundua kile alichokifanya lakini maneno ya Salvatory yalimfariji na hakuhofia kuachwa.Siku zote hakutaka kulala na Salvatory kitanda kimoja si kwamba aliilinda bikra yake,hapana!Aliogopa siri yake kuvuja na yeye kukosa bahati hiyo ya kuolewa.Aliamini ndoa pekee ndiyo ingemuepusha asije akaachwa kutokana na tabia yake hiyo ya kukojoa kitandani.Kama kawaida yangu Hakika Jonathan baada ya kisa hiki kunijia katika fikra zangu,nikachukua Laptop na kuandika kama kumbukumbu ili iwe fundisho kwa wengine.
MALIPO NI HAPAHAPA DUNIANI,KILA JAMBO MUNGU ANAMAKUSUDI KATIKA MAISHA YAKO USIMLAUMU WALA KUMDHARAU KIUMBE KAMA WEWE ALIYEUMBWA NA MUNGU.