SIKU NILIYOKWENDA KUNUNUA MWANAMKE
Kuna siku nilienda sehemu kwajili ya kununua mwanamke si unajua tena haya mambo ya ujana ingawa nilikuwa na mke pamoja na watoto, nikiwa ndani ya gari langu nasogea maeneo yale karibu kabisa nilimuana mzee mmoja hivi.
Nilikutana na yule mzee akiwa amezeeka na amevaa nguo kuu kuu zilizochoka, akaniangalia kwa macho ya kutafakari kisha akaniambia kwa sauti ya upole lakini yenye uzito wa hekima:
“Mwanangu pesa ni kama mvua ya ghafla huja kwa nguvu, lakini ikiisha tu ardhi hubaki kavu. Ukiwa kijana, pesa utakutana nayo kwa njia nyingi, lakini usipojua thamani yake, utaifikia uzeeni ukiwa huna hata kivuli cha kumbukumbu nzuri.”
Akaendelea…
“Niliwahi kuwa kijana kama wewe – nguvu nilikuwa nayo, marafiki walikuwa kibao, pesa zilipita mikononi mwangu kama upepo. Lakini nilikosea. Nilifikiri ujana unadumu, nilidhani pesa hazitaisha. Sikuwekeza, sikusave, niliishi kwa ‘leo ni leo, kesho ni mapenzi ya Mungu.’ Na sasa tazama…”
Akageuza uso wake na kunyoosha mkono kwenye kiatu kilichochanika…
“Leo, nina miaka 76. Sina pensheni, sina biashara, sina hata nyumba ya kupanga iliyo kwenye jina langu. Wale marafiki wa starehe walipotea na pesa ziliisha kabla ya busara kufika.”
Kisha akaniangalia tena machoni:
“Kama uko kijana sasa, jifunze kujiwekea akiba. Wekeza hata kidogo. Jifunze kusema ‘hapana’ kwa anasa na marafiki wa muda mfupi. Pesa ni mtumwa mzuri lakini bwana mbaya sana. Na ujana? Ni kivuli cha jua la asubuhi hakikai!”
Nikanyamaza kimya nilitabasamu kwa huzuni, nikamshukuru kwa hekima yake.
Niliondoka eneo lile taratibu bila hata kugeuka nyuma nilijihisi tofauti nikatafuta sehemu nikakaa ghafla nikaanza kulia na kujiona mkosaji sana.
Nilinyanyua simu yangu nikampigia mke wangu na kumwomba atoke nyumbani aje nilipo ili tuweze kutulia kwa pamoja, nilishindwa hata nimwambie nini kwani alitaka kujua nilichomuitia.
Tangu siku hiyo, nikaanza kuheshimu kila senti ninayopata, maana nilielewa
Ujana ni wa muda, pesa huisha lakini busara huokoa maisha.