Clickable WP Image
JOIN US WHATSAPP CLICK HERE
JOIN US TELEGRAM CLICK HERE

NILIDHANI MGENI, KUMBE MKE MWENZA

(PIGO LA MKE MWENZA)

PART: 01

Kwa majina naitwa Mama Furaha kutoka wilayani karagwe mkoani kagera. Karibu kupata story hii ikiletwa kwako na McLaurian.

Ni mida ya saa 12 hivi na mkanda wake  huku jua likiwa linaanza kuzama kwa mbali , ndipo nilipombeba Furaha kisha nikafungasha vipande vitatu vya kuni pamoja na vyombo ambavyo nilienda navyo shambani.

Bila kuchelewa, nilianza safari ya kurudi nyumbani ili nimpikie mme wangu kipenzi ambaye aliniaga kwenda harimashauri kwa ajili ya kufuatilia pesa za TASAF.

Mwendo wangu ulinifanya nichoke kweli japo sikuwa na namna yoyote mpaka hapo mida ya saa moja hivi nilipowasiri nyumbani.

Nilibwaga mizigo yangu ” puuuh!” Huku kichwa changu nikihisi kama kinawaka moto hivi kutokana na jasho lililotokana na kata iliyotengenezwa kwa kanga yangu.

Baada ya kutua, nilifungua mlango kisha nikaingia ndani ndipo nilipoona viatu vyote vya baba furaha vikiwa ndani.

     ” Hee! Kumbe kasharudi ” nilijiuliza huku nikiwa natabasamu.

Nilikagua kila sehemu kuona kama amemletea Furaha mkate au andazi kutoka wilayani lakini wapi sikuweza kuona chochote kile.

Kwakuwa sikuwa na simu, nilitulia kisha nikabeba panga langu na kuelekea shambani ili kuvuna ndizi kwa ajili ya chakula cha usiku.

Nilitamani kumuacha sebuleni mtoto Furaha lakini niliona panya watamsumbua maana walikuwa wanarukaruka kwa sifa asee utadhani wataishi milele.

Giza kwa mbali lilitanda kwani migomba ilikuwa imeshiba vizuri kiasi cha kutengeneza hali ya kama msitu hivi.

Niliingia shabani huku majani makavu yakitoa sauti ya ” parakacha..!parakacha..!” Japo sikuogopa maana nilishazoega.

Niliendelea kutembea taratibu kwa tahadhari kubwa mpaka kwenye ndizi niliyokuwa nataka kuikata.

Nilitoa nguzo iliyokuwa imeshikilia ndizi hiyo kisha nikaidondosha kwa chini.

Ndani ya sekunde kama 3 hivi, nilisikia na kuona watu wawili wanainuka na kutimua mbio kari kabisa na sehemu niliyokuwepo.

Kwa mshutuko mkubwa nilipiga kelele iliyoishia tumboni kisha nikadondoka chini na alimanusura kidogo nikatwe na panga.

Furaha alianza kulia ndipo niliposhutuka kuwa huenda kaumia lakini bahati nzuri aliweza kutulia.

” Hee!  Maajabu gani haya, yaani watu wazima wanakuwa kama mbwa!. Wanabahati kama angelikuwepo baba Furaha, angeweza kuwakamata au kujua sura hata ya mmoja wao”

Niliongea peke yangu huku nikiwa naelekea sehemu walipokuwa.

Baada ya kufika sehemu hiyo, nilishangaa kukuta kandambili mbili moja ambayo ilikuwa na rangi ya blue kama za mme wangu. Nilichunguza kwa pembeni ndipo nilipokutana na nguo ya kike ya ndani ambayo ina umbo la V iliyokuwa na rangi nyekundu pamoja na viatu vya kike.

Nilibaki kinywa wazi bila kuamini nilichokiona kwa macho yangu.

Nilivikusanya kwa kijiti kisha nikavificha sehemu ya pembeni kidogo ili kesho kukiwa na mwanga, niangalie vizuri na baba Furaha.

Haya niliikata ndizi na kuelekea nyumbani.

Nilianza kuzimenya na ndani ya lisaa limoja, chakula kilikuwa kimeiva.

Kama ulivyokuwa utaratibu, sikupenda kula chakula peke yangu bila mme wangu kipenzi japo ambaye kiukweli hapendi kufanya kazi mpaka nyumba niliyofikia ilikuwa imejengwa kwa matope ikiwa na chumba kimoja na sebule.

Kwasababu jembe halimtupi mkulima, nilipambana mpaka nikajenga nyumba ya tofali yenye vyumba vinne na sebule mbili.

Nilimsuburii..mpaka saa 4 sasa za usiku lakini hakutokea ndipo nilipojawa na hofu kwani licha ya kupenda kunywa na kulewa, hakuwahi kufikisha mda huo.

Nilienda chumbani nikaanza kutandika kitanda ili walau nipoteze mda lakini nilimaliza bila kumuona.

Uvumilivu ulinishinda kabisa kwani nilikuwa na njaa kweli ndipo nilipokua chakwangu kisha nikaanza kula.

Ndani ya dakika 2 hivi mara baada ya kuanza kula, alisikika mtu anagonga mlango ndipo nami niliponyanyuka haraka kuufungua.

Ile nafungua, nilikutana na mme wangu kama nilivyokuwa nawaza huku akiwa na ndala moja mguuni.

“Karibu..”nilimkaribisha.

“‘Asante..” alijibu huku akionesha kuwa na hasira kwa mbali.

” Mbona upo na ndala moja?” Nilimuuliza.

“Ebu nipakulie chakula nile!. Maswali gani unaniuliza!, mimi ni mwanaume! ” alifoka.

“Mbona hivo jamani!,..kwani  nimekukosea nini?”

“Kwanza we mke gani sura yenyewe imekomaa hivyo afu umelegea kweli mpaka unanitia aibu”

“Unasemaje!, kila siku nashinda kwenye jua nalima afu wewe kazi yako kulewa ndo shukrani yako. Hii nyumba kama sio nguvu zangu ungekuwa unaishi wapi?, hata mie sipendi kuwa hivi ila kumbuka hata hao wanatunzwa sio wewe hujawahi kuninunulia hata rosheni.” Machozi yalinitoka huku nikiwa najiuliza kwanini leo kawa hivyo mpaka anaongea maneno makali.

“Wewe ni mbaya bwana shukuru nilikuokoa ungezeekea nyumbani. Maziwa yenyewe yamekushuka kama Mwajuma ndala ndefu mpaka sipati hamu ya kuwa na wewe kabisa. Leo nakwambia ukweli hata kama ni mchungu”

“Nilikulazimisha unioe..!, heee!..lione!.. ” Uchungu uliongezeka mpaka nikaanza kulia kwa sauti ya chini.

“Unaniambia lione!!.nitakubutua mda huu! Eheee ..hunijui wewe!”

“‘Nibutue! …nasema nibutue..! Mi nimekusemesha! Umenikuta zangu nimetulia afu unakuja na mapombe yako ! Kwendraaa huko.”

“‘Pombe umeninulia wewe!..kwa taarifa yako sijalewa wala nini ila leo nimeamua kukwambia ukweli wa moyoni kabisa”

” Basi umeshinda niache na ubaya wangu nipumzike ila..ila…labda sio mimi!” Niliongea kwa uchungu.

Nikiwa naelekea chumbani, gafla ilisikika sauti kama ya kike hivi ikigonga mlango ndipo nilipobaki nimeganda huku nikiligeuza shingo langu huku nikiwa na shauku yakujua nani anagonga usiku huo……

PART: 02

ILIPOISHIA..

Sauti ya kike ilisikika ikibisha hodi huku mlango ukigogongwa bila kujua nani anagonga mlango….

SONGA NAYO…

Nikiwa nimegeuza shingo langu kama mtu aliyepatwa na mshutuko mkubwa sana, nilimuona baba Furaha akinyanyuka taratibu bila wasiwasi wowote kuelekea kufungua mlango.

Nilimtia jicho lakini hakuniangalia ndipo alipofungua mlango.

Baada ya kufungua mlango, aliingia msichana ambaye si mrefu wala mfupi, si mnene wala mwembamba huku rangi yake kama ya kunde hivi japo ilikuwa usiku na mwanga hafifu.

Mkononi alikuwa na begi kubwa kweli ambalo mtoto wa darasa la 5 asingeweza kulibeba.

Kiukweli msichana huyo alikuwa mzuri sana japokuwa nilijikubali lakini kizuri kipe sifa zake.

Kwakuwa sikuwahi muona wala mfahamu, nilitega masikio yangu ili kujua nini kitaendelea .

“Karibu hapa ndo nyumbani” baba Furaha alimwambia huku akimpokea begi lake.

“Asante sana” msichana huyo aliitikia huku akinitazama kwa jicho la chongo kisha anainamisha kichwa.

Kwakuwa alikuwa mgeni, nilienda chumbani nikajifunga kanga kisha kisha nikarudi sebuleni.

” Mgeni karibu..” nilimkaribisha huku nikimtia jicho kujua ni nani

Kabla hajanijibu, baba Furaha alidakia kama kidaka tonge kwa kusema’

” We mwanamke mbona unakiherehere!..unamuuliza nini!, nenda ukalale huko na umbea wako”

“Kwani kumkaribisha nimekosea?, eti dada nimekosea?”

Dada huyo alitabasamu bila kujibu chochote kile huku baba Furaha akiniangalia kwa jicho la ukali.

Licha ya maneno hayo makali mbele ya mgeni, sikusita kumuuliza walau hata jina lake..

” Samahani unaitwa nani?” Nilimuuliza.

“‘Naitwa Joy…” alinijibu.

“‘Ohh kumbe …”

“Ndiyo…”

“‘Sawa mi naitwa mama Furaha”

“Asante..”

Baada ya utambulisho huo, nilitamani kuendelea kumuuliza lakini niliona busara kwa mgeni kumfanyia hivo.

Nilinyanyuka taratibu mpaka chumbani kisha nikajilaza japo usingizi haukupatikana hata kwa sekunde moja.

Nikiwa nimejilaza, niliwasikia wakiendelea na maongezi ambayo yalinicha kinywa wazi.

Nilinyanyua mbavu zangu na kutaka kufungua mlango lakini nikaamua nitulie kwani wakati huwa haudanganyi.

“Hii ndo nyumba yako utakayokuwa unaishi na huyu uliyemuona, ninampango wa kumfukuza maana siwezi kukaa na mke mbaya namna hii” baba Furaha alisikika akimwambia Joy kwa sauti ya chini sana.

“Mhh… “‘

“Mbona waguna”?

“Hamna …”

Nikiwa nimeweka macho yangu wazi, mlango ulifunguliwa kisha baba Furaha akaingia na kuzama uvunguni kisha akavuta godoro na kutoka naro.

Sikumuongelesha chochote maana nilimjua tabia zake.

Ndani ya dakika kama 10 hivi, alikuja tena chumbani kisha akabeba mashuka mawili .

Niliwaza na kuwazua iweje mwanaume aanze kumtandikia mgeni wa kike sehemu ya kulala?.

Swali hilo sikulipatia majibu na badala yake liliniongezea maswali mengine zaidi.

Ukimya ulitawala kisha mwanga wa sebuleni ambao uliokuwa unaangaza, ukapotea gafla.

Nilikaa kimya bila hata kukohoa huku nikiwaza kama ni kweli kilichopo moyoni mwangu, basi naondoka na roho ya mtu.

Wahenga wasema ” chelewa chelewa, utakuta mwana si wako”. Nikiwa nimemsubiria baba Furaha kwa lisaa lizima sasa, nilinyanyuka kitandani kisha nikajifunga kanga iliyoanzia shingoni kushuka mpaka kwenye magoti.

Taratibu nilifungua mlango ili sauti isisikike.

Nilipofika sebuleni, nilishangaa kutokuona mtu yeyote.

“‘Hee! Wameenda wapi?,” nilijiuliza huku nikiangaza huku na kule

Wakati naendelea kuangaza, niliona viatu vya Joy karibu na chumba cha wageni ndipo niliposogeza sikio langu kuona kama kuna mtu ndani.

Haikupita dakika hata 1 hivi, sauti iliyokuwa na mlio kama kinanda ambacho kinalizwa vizuri, zilisikika kutoka chumbani humo ndipo nilipoishiwa nguvu.

“Ina maana amelala na mgeni!..hata kama hanipendi hii ni dharau kubwa sana” kwa hasira kali nilijisemea moyoni huku nikitamani kuvunja mlango kwa meno kama kiboko afanyavyo kwa mitumbwi.

Sikuona haja ya kuishi tena kwani uchungu ulikuwa mkubwa sana.

Niliingia chumbani kisha nikavaa kijunga ( kikaptula) changu kisha nikavaa na Tshirt.

Bila kuchelewa, nilibeba panga lake mkononi huku machozi yakiwa yananitoka kama mtu anayepuliza na kuchochea  moto kwenye kuni mbichi.

Nilipofika kwenye mlango wa chumba walichokuwemo, nilisikia sauti zikiongezeka huku kwa mbali kimvua kikianza kunyesha hali iliyosababisha ubaridi kweli.

Nilisukuma mlango kwa nguvu lakini kumbe ulikuwa umefungwa.

Kitendo cha kufanya hivo, kiliwashutua kidogo maana kelele za kinanda na muungurumo, zilikata gafla kama umeme uliokatika.

Nilisukuma tena kwa nguvu lakini wapi ndipo nilipoamua kwenda nje ili kubeba jiwe kubwa maarufu kama ” FATUMA” ili niligongeshe mlangoni.

Bahati nzuri nilifanikiwa kulipata japo lilikuwa zito sana.

Taratibu nililisogeza mpaka nikafanikiwa kuingia nalo ndani huku nikiwa nahema.

Sasa nilijiandaa kulisukuma jiwe hilo moja kwa moja kwenye mlango wa chumba hicho huku kwa pembeni nikiwa nimeegesha panga langu.

Nilijitutumua kwa kulinyanyua kwa nguvu zote kisha nikahesabu kimoyomoyo 1…2…….

JE MLANGO ULIFUNGUKA?

JE ILIKUWAJE?

JE HUYO NI MGENI KWELI AU LA!?

PART: 03

ILIPOISHIA,

Kwa nguvu nilinyanyua jiwe zito sana kisha nikajiandaa kuligongesha kwenye mlango ili ufunguke.

SONGA NAYO…

Wakati zimebaki sekunde chache sana kabla ya kuliachilia, nilijiwa na wazo moja kwa haraka kichwani mwangu.

   ” Sasa nikivunja mlango si itakuwa hasara?!, lakini haina shida kama ni hasara basi…” Nilijisemea mwenyewe moyoni mwangu huku nikiwa nahema ” twii…twiii..”.

Nilifumba macho yangu kisha nikaachamisha kinywa changu huku nikiwa nimeinama kidogo kama mtu anayetaka kuruka kichura kisha nikalisukumizia jiwe hilo kubwa mojakwa moja kwenye mlango “puuuh…..!.

Asee niliogopa sana mara baada ya kusikia mdada aliyejiita Joy akipiga kelele ” mama..mama!”!.

Kusikia hivo, nilijiweka mkao wa kutimua mbio mithiri ya panya aliyehisi harufu ya paka.

Vile nashangaa tu!, nilijikuta kwenye mikono ya baba Furaha ambaye alikuwa amevaa bukta huku akiwa kifua wazi.

Sura yake ilinitisha sana mpaka nikatamani kukimbia lakini haikuwezekana kwani alikuwa emeniweka kwenye himaya yake.

  ” Unanijua unanisikia!.. nakuuliza wewe mpuuzi” aliongea huku akiwa ananivuta mkono kwa nguvu.

 “Niacheee!..niache!..” Nilitoa sauti kali huku nikiinama ili nimg’ate mkono lakini niliishia kula kofi za mashavuni .

 ” Dharau uliyoionesha siku ya leo!, utanitambua. Sidhani kama utaliona jua kuanzia sasa! Umechezea pabaya sana, utajua kama mafunzo yangu ya mgambo yalikuwa na faida au la!” Alizidi kunivuta mkono huku akitaka anifunge mikono kwa kamba ya katani ambayo ilikuwa imefungwa kwenye gunia la karanga.

”  Dharau! …dharau ipi unasema! Unapata wapi ujasiri kuleta malaya wako kwenye nyumba ambayo nimeitolea jasho tena unadiliki kulala naye kabisa. Siogopi chochote hata unieue lakini kitachimbika”

“‘Ohh unasema huyo malaya!, sasa ndo mke wangu kuanzia sasa kama ulikuwa hujui. Huwezi kunilazimisha nikupende na sura yako ya bibi kizee mpuuzi wewe”

“Lione .., nendeni mnakojua ila sio kwenye nyumba niliyotoa jasho langu.”

Baada ya kumwambia hivo, alivimba kama nyoka anayetaka kutema mate ya sumu .

Aliniangalia kisha akanipiga mtama nikadondoka chini kama mtoto mdogo.

Asee nilihisi kuona viluwiluwi mara baada ya kudondoka chini.

“Mama..mama..nakufa!!..,nakufa..” nilipiga kelele.

” Kuna mama yako hapa!..hee! Nasema kuna mama yako?!, sasa leo ukilala bila kupoteza maisha labda sio mimi”

Aliniviringisha kisha akaniziba mdomo ili nisitoa sautin

Baada ya kufanya hivo, nilishindwa kupumua vizuri mpaka nikajikuta nataka kupasuka kabisa.

Nilitamani kupata hata mtu wa kunipa msaada lakini hakupatikana kwa mda huo.

Kwa mbali, nilianza kuwaona wajuba wakiwa wanataka kunichukua ndipo niliogopa sana tena sana.

Ndani ya dakika kama 10 hivi, aliniachilia kwa mda ndipo nilipopumua kwa haraka mithiri ya maji yaliyozuiwa yavunjavyo daraja.

“Haaah!..haah!..haaah!..heeeh…heeeh!” Niliendelea kupumua kwa kasi.

” Utarudia tena wewe mpuuzi!, utarudia tena?” Akiwa ananitikisa kichwa changu mithiri ya mama amwambiavyo mtoto aliyevunja chupa ya chai.

“Sirudii tena mme wangu..hooh!..hooh!.sirudii tena nisamehe..”

“Sasa ndo uelewe kwanini naitwa mwanaume”

“Lala hapo nikuchape bakora tano..!”

Asee kwa hali niliyokuwa nayo kwa mda huo, nililala huku nikiwa nimegeuza shingo langu juu na kumuangalia kwa macho ya huruma.

“Baki hapohapo wala usijitingishe!” Alifoka kisha akaenda akatafuta fimbo ambayo ilikuwa pembeni mwa ukuta.

Katika vitu naviogopa ni viboko lakini sikuwa na namna maana bila kufanya hivo, wajuba angeweza kunitoa uhai na wajuba kunichukua.

“Usiniangalie!..angalia chini!, ukiweka mkono kwenye makalio hiyo nafuta”

Alisema kisha nakajaribu kuangalia chini lakini uvumilivu ulinishind maana nilikuwa nimevaa bukta laini tu.

“‘Mme wangu nisamehe nakuomba!..nakuomba.”

“Fumba mdomo huo!, hilo jiwe umerusha kama sio uimara wangu mda huu tungekuwa tunasema mambo mengine”

“Ni hasira tu ila sitorudia kabisa mme wangu”

Wakati naendelea kumbembeleza, Joy alitoka chumbani humo akiwa amejifunga kanga mpaka sehemu niliyokuwepo.

Niliona aibu kulia mbele yake lakini sikuwa na namna. Nilimchungulia na japo kwa hofu lakini kiukweli uzuri wake ulikuwa unatisha mpaka nikazidi kupandwa na presha

“‘Mme wangu naomba umsamehe kama ni kosa lishatendeka. Itoshe kusema muache usije kujitafutia matatizo mengine” Joy alimwambia baba Furaha.

“Anadharau sana, anapaswa kunyooshwa ili aache kunichezea..”

“Mhh ni hasira tu, kwani ulikuwa hujamwambia kabla kuwa una mke ?”

” Analijua maana nina zaidi ya wiki 3 sijamuomba …na sina hamu naye”

“Mhh makubwa. Mimi huko sipo ila usimpige tafadhari kama wataka kumpiga basi namimi naondoka mda huu nitajua wapi pakulala”

Maneno hayo yalimpunguza nguvu kabisa mpaka akajikuta fimbo alokuwa ameushika mkononi inadondoka yenyewe.

Moyoni mwangu nilifarijika kwa hali hiyo lakini kiukweli nilikuwa na hasira hata za kula nyama ya mtu mbichimbichi.

Aliondoka bila kuongea chochote kisha akafungua mlango na kutoka nje.

Ndani ya sekunde kadhaa, nilinyanyuka chini kwa haraka sana kisha nikafunga mlango ili asiingie.

Uzuri wa milango ya nyumba hiyo, ni imara sana kiasi kwamba ili uufungue labda utumie mashine ya kukatia vyuma.

“Hee mbona umemfungia?” Joy aliniambia

“Nyamaza wewe! Unajua uchungu nilionao!, sasa leo we ni halali yangu. Ame nife mimi au ufe wewe ila lazima mmoja apotee!” Nilimwambia kwa hasira.

“Hee! nimekukosea nini?!, yamekuwa hayo tena!”

Wakati anamalizia kuongea hivo, baba furaha alisikika akigonga mlango lakini wapi ndipo nilipowahi kushika kisu kilichokuwa kinatumika kukatia nanasi.

“Si umejifanya mjanja!, ingia ndani sasa tuone, Malaya wako huyu utamkuta vipandevipande kama unamuuza bucha, mwandae aje abebe nyama…”

Nilimwambia kisha nikamsogelea Joy kwa hasira sana huku naye akisogea nyuma….

PART: 04

ILIPOISHIA,

Nilimfungia mlango baba furaha kisha nikamfata Joy aliyekuwa ndani huku nikiwa nimeshika kisu kikali mkononi..

SONGA NAYO…

Baada ya kuanza kumsogelea Joy, alipiga kelele kwa sauti kubwa sana mithiri ya mtu aliyemwagikiwa na uji wa maziwa.

Kwakuwa ilikuwa usiku uliotulia tuli, nilihisi hata majirani kusikia sauti hiyo ndipo nilipomkanya mara moja.

” Fumba mdomo wako mara moja!” Nilimwambia huku baba Furaha akigonga mlango kwa nguvu bila mafanikio.

“Ndiyo nanyamaza..nanyamaza usinichome ” Joy aliitikia huku akiwa anatetemeka.

“Kaa chini..!'” Nilimuamrisha huku nikiwaza kumchoma kisu shingoni.

Hakuwa na ubabe wowote ule na badala yake alitii kila nilichomwambia.

“Ebu niambie umefikaje hapa!”

“Tulipanga tangu mda mrefu mara baada ya kunipa ujauzito akasema atanioa siku ya leo”.

“‘Hee! Una mimba .!:

“Ndiyo ya miezi 6..”

“‘Wakati mnafanya ujinga wako hukujua kama ni mme wa mtu?”

 ( Joy alikaa kimya tuli)

“Nakuuliza wewe na masikio kama ya popo!, hukujua kama anafamilia?”

“‘Ali..alinifata mwenyewe kisha akasema mmetengana hivo anataka mke wa kuishi naye”

“‘Ilikuwa lini hiyo!”

“Sikumbuki ila ni mda sasa…”

“‘Ndo nyienyie kazi kuvunja ndoa za watu!, kwanza umri wako naye hamringani kabisa ..malaya wewe”

 ( Joy kimya akiwa ameinamisha kichwa chake chini)

“Sasa chagua kati ya kufia hapa au kuondoka hapa!, nimeheshimu mtoto aliyeko tumboni laa sivyo mda huu ungekuwa nyama zilizotapakaa damu”

Wakati namwambia hivo, baba furaha alionekana akipitisha kichwa  kwenye dirisha kama kibaka fulani hivi.

Nilishutuka mno kwani kuingia kwake angeweza kuniua kabisa.

Nilipiga hatua ya gafla kisha nikashika fimbo nakuanza kumponda kichwa kama nyoka.

“Rudisha kichwa hicho..!., unikome tangu leo,..jiheshimu..” nilimponda kweli.

Baada ya kupokea kipondo, alicharibu kurudisha kichwa chake, lakini chakushangaza na kuchekesha, kiling’ang’ania dirishani hapo na kila akijaribu kukitoa nafasi inakuwa haitoshi.

“Ukome si umeingia mwenyewe!, ongea sasa kama wewe mwanaume”

Nilimuacha akitapatapa kujinasua lakini bado kisha nikamfata Joy.

“‘Sasa nakuomba kwa heshima zako, ondoka nyumbani kwangu. Sikukatazi kuwa na Malaya wako lakini ni marufuku kukanyaga kwenye nyumba niliyoijenga kwa jasho langu.”

“‘Sina pa kwenda maana nyumbani nimepakimbia ili wasijue maana baba ni mkali sana anaweza kuniua”

“Unasema!..hivi unanijua au unanisikia!, ngoja nikuoneshe kazi sasa”

Nilimsogelea kisha nikamlamba kofi moja zito kwenye shavu lake la kulia.

“Hii…hiii!..! mme , naondoka!  …naondoka” alisalimu amri huku akitoa sauti ya kilio.

Nilimvuta kisha nikaingia naye mpaka chumbani walipokuwa.

Kuingia tu, nilikutana na harufu fulani sijui niisemeje huku mashuka yakiwa yamejichora ramani kama ya Afrika au Amerika na wino uliokuwa haujakauka vizuri.

Hali hiyo iliniumiza kweli maana nilikuwa na mda wa wiki kama hivi bila kupata haki yangu ya kuvaa pete huku baba Furaha akisingizia kuwa anakuwa anachoka ilihali huwa anashinda bila kazi.

Chozi lilinitoka hisia zangu zikanipanda mpaka magotini bila kupata mtu wakunituliza.

Kwa hasira kali, nilirusha begi lake sebuleni kisha nikamtagert kumchoma walau mkononi lakini alinikwepesha mkono.

Nilinyanyua kutaka kumchoma tena maana alikuwa mdada fulani hivi asiye na nguvu hata kunifikia nusu yangu.

Wakati nataka kufanya hivo, niliogopa hasa suala la mimba ndipo nilipomsukuma akaangukia sebuleni.

“Utarudia tena kukanyaga nyumbani hapa!?” Nilimuuliza kwa ukali huku nikiwa nimemnyooshea kidole cha kati karibu na jicho lake.

“‘Hapana sitorudi tena naomba nifungulie niondoke” alinijibu huku akihema kama temba anayefukuzwa na jogoo ili apewe uzao.

“Nikikuona hapa nikufanyeje!?”

 ( Joy kimya)

“Hunisikii!?, au dharau..”

“Utakavyoamua wewe .”

” Haya umeongea mwenyewe ole wako ulete miguu yako tena. Hutoamini kitakacho kukuta..”

Baada ya kumwambia hivo, nilimchungulia baba Furaha lakini uzuri kichwa chake bado kilikuwa kimeng’anga’ani kwenye nondo ya dirisha huku akianza kutokwa na machozi.

“Mke wangu nisaidie nakufa..nisaidie tafadhari..” aliongea kwa sauti ya huruma”

“Leo ndo umeniona wa thamani eeh!., aku!..pambana na hali yako. Umejiingiza mwenyewe na utajitoa mwenyewe au ufie hapohapo .”

“Nilikuwa nakutania mke wangu. Nakunda sana na siwezi kukuacha .Wewe ndo malkia wa moyo wangu. Nakupenda sana.”

“Unadhani mie mtoto mdogo?, kama wanipenda umeniletea nini hii!, sidanganyiki. Una roho ngumu sana mpaka na huna shukrani”

“‘Nisamehe nilikosea sitorudia tena.., nisaidie au kawaite watu maana nakufa hapa!” Baba Furaha aliongea kwa huruma huku akichuruzika chozi.

Baada ya maneno hayo ya huruma, niliinamisha kichwa changu huku nikiwaza nini nimfanyie ….

PART: 05

ILIPOISHIA

Baba Furaha aliendelea kuomba nimsaidie kumnasua kwa maneno ya huruma kabisa huku nikibaki njia panda …

SONGA NAYO..

Niinamisha kichwa changu chini mithili ya kobe anayetunga sheria kisha nikajawa na roho ya huruma moyoni mwangu iliyoambatana na hofu kubwa sana.

Nilimtizama baba Furaha kisha nikatabasamu kwa kejeli huku nikitikisa kichwa changu.

Baada ya kuona maji yanakaribia kuzidi unga, nilimshika mkono Joy kisha nikamfungulia mlango .

Nilimsukumiza kwa nje akiwa na begi lake pamoja na meneno juu yake kama ishara ya kumtisha ili asirudie tena.

“Nimekusamehe sasa ole wako nikuone umeleta fimbo zako za miguu hapa nitazivunjavunja”

Joy hakuongea chochote badala yake alipengà kamasi laini huku akionekana mwenye huzuni kubwa sana..

Niliingia ndani kisha nikaanza kufunga mlango. Kabla ya kumaliza kufunga mlango, gafla mlango ulisukumwa kwa nguvu sana mpaka nikashangaa.

Bahati nzuri nilifanikiwa kuweka komea kisha nikaegeshea na madumu ya maji ya lita 20.

Niliangaza moja kwa moja mpaka dirishani lakini sikuweza kumuona tena baba Furaha.

” Fungua mlango huo! ” sauti kali ilisikika kwa nje.

” Nani akufungulie!, lala huko nje ” nilimjibu.

” Unasema?!”

” Nasema nini kwani hunisikii?

” Sasa ngoja nikuoneshe kuwa mi mwanaume”

“Huuna aibu kulilia nyumba ya mwanamke!, “

Baada ya kauli hiyo, mlango uligongwa kwa kitu kizito sana mpaka ukatoa sauti  ” Puuh!”

Nilishutuka na kuanguka chini kisha nikainuka huku nikiwa nahema.

Madumu yote yalidondoka chini ndipo nikaanza kuyaweka tena.

” Unafungua hufungui!?” Alisikika akisema kwa nje

” Sifungui!” Nilimjibu kwa hasira.

” Sawa ila nikikuweka kwenye anga zangu, walahi nakunyonga na kukula mzimamzima ukiwa mbichi”

” Na umechelewa njoo hata sasa hivi. Unadhani nakupopa!”

” Sawa we endelea kusema hivo ila nakwambia hutoamini nitakachokufanyia”

Baada ya mazungumzo hayo, ukimya kidogo ulitawala huku nikiwa nimejibanza kwenye mlango.

Kwa mbali nilianza kusikia minong’ono kutoka kwa Joy akimlalamikia baba Furaha.

” Mi naondoka, siwezi kukaa hapa hata siku moja . Kama unanipenda basi kanijengee nyumba yangu mjini”

” Kwanini!?, hapa ni nyumbani kwangu na huyu kichaa namuondoa hapa mda si mrefu”

” Mhh amesema akiniona tu ananivunja miguu yangu..”

” Akuvunje yeye ni nani!?, anakutisha tu . Usiogope chochote na wala usiende sehemu yoyote . Jisikise huru hapa ni kwako.

” Lakini mbona anasema nyumba hii ni yake?”

” Nyumba yake ameijenga hapa ni kwao?, “

” Haya mme wangu ila namuogopa sana”

” Usimuogope hana lolote na hana chochote”

Waliondelea kuongea kwa sauti ya chini huku nikiwa nawasikiliza.

Niliangua kicheko cha kejeli .

    “” Hahahha!! Hahahah!…hahahaha”

” Hee! Kumbe ametusikia ?”

Joy alisilika akiongea.

” Hana lolote huyo”

Hawakuongeza neno lolote lile ndipo lipoenda chumbani kulala .

Baada ya dakika kama 10 hivi, nilizinduka mara baada ya kusikia sauti ya mtu akiwa akiwa anachimba hivi.

” Nini hiki!” Nilishutuka

” Nakaribia kutoboa…”Sauti ya baba Furaha ilisikika.

” Eboo! ” nilijifunga kanga huku nikihaha wapi pa kukimbilia.

Ama kweli nilianza kuona kama nazama kwenye bahari yenye kina kirefu ambayo imejaa samaki wakubwa sana wala watu.

Niliangaza huku na huko lakini sikupata jibu kipi nikifanye kwa wakati huo.

” Leta jiwe hilo!, bado kidogo nimekaribia kubomoa” sauti ya baba Furaha ilisikika.

” Hee! hivi huyu mwanaume ni kichaa au?, sasa atanikuta humu kama ananiua aniuwe basi ila sitoki”Nilijisemea mwenyewe huku moyo kwa upande mwingine ukiniambia ” kimbia”..

JE ILIKUWAJE?….

PART: 06

ILIPOISHIA,

Baba Furaha alisikika akiongea na Joy kuwa amekaribia kutoboa ukuta..

SONGA NAYO..

Nikiwa nimetega masikio yangu kama ungo la kunasia wawimbi, nilikuta napata wakati mgumu sana.

Nilijifunga kanga yangu vizuri kwa ajili ya lolote. Ndani ya dakika 1 tu, mapigo ya moyo wangu yaliongezeka huku sauti ndani mwangu ikiniambia,

  ” Kimbia..kuishi ni mara moja tu!”

Bila kupingana na sauti hiyo, nilitembea kwa kunyata taratibu mpaka mlango wa nyuma kisha nikaufungua huku nikichungulia kama kuna mtu.

Bahati nzuri nilifanikiwa kutoka salama salimini.

Kwakuwa giza lilikuwa nene, nilijibanza kwenye migomba huku nikiwachungulia.

Baba furaha miguu tu ndo ilionekana na baada ya mda alizama ndani mzima.

Haikuchukua hata dakika 1, mlango ulifunguliwa kisha Joy naye akaingia ndani.

“Funga mlago asije akatoroka!, leo ni leo yaani ananifungia!” Alisikika akibweka kweli kwa sauti ya juu.

Baada ya kusikia maneno hayo, nilisogea nyuma kidogo huku nikihofia usalama wangu.

” Uko wapi wewe ! Leo nakuchinja..!” Alizidi kupiga kelele.

Baada ya mda, niliona niondoke sehemu hiyo lakini nilikumbuka kitu,

“Ohh .. nimemsahau mwanagu Furaha!”

Nilisikitika sana kwani nilimpenda sana mwanangu wa pekee. Nilitamani kuingia ndani lakini niliogopa.

Kwa uchungu mkubwa huku nikiwa naogopa kweli hasa giza, niliamua kwenda kwa mwenyekiti wa serikali za mitaa ili anipe msaada.

Nikiwa njiani kuelekea kwake, gafla niliona mtu kama amejibanza kwenye mgomba huku akitikisa kichwa. Nilipiga kelele kwa nguvu,

“Mama..mama..mama”

Nilitimua mbio kama kibaka aliyenusurika kwenye kiberiti.

Nikiwa nahema kwelikweli, nilikutana na vijana wawili wakiwa wameshika rungu.

Bila kuchelewa, nilitimua mbio huku nikidhani ni miujiza niliyoona kwa mbele.

Kitendo cha kukimbia, walianza kunifukuza ndipo nilipoongeza kasi ambayo ndani ya dakika 1 ilikata kabisa mara baada ya kudondoka chini.

Walinirukia kisha wakanikamata. Asee walikuwa na nguvu kwelikweli. Kwa bahati mbaya, hakuna niliyeweza kumtambua kwani walikuwa wamevaa mask.

“Unatoka wapi usiku huu!, nyie ndo wezi wa ndizi mtaa huu. Kila siku watu wanalalamika kumbe wewe ndo mwizi eeh!, sasa leo utaongea” walinifokea huku wakitaka kunifunga mikono kama mwizi.

“Hapana mimi siyo mwizi..mimi siyo mwizi subiri niwambie sasa..”

Kabla sijamalizia kuongea, walidakia kwa pamoja

” Kama siyo mwizi kwanini umekimbia?”

“Nilifikiri ni mtu niliyemuona kwa mbele hapo ambaye alikuwa amejibanza huku akirusha mikono..”

“Hee unasema!? mtu yupi huyo…”

“Njoo niwapeleke..”

“Oya..anazingua sana. Anatupeleka wapi?”

“Ebu muache atupeleke..”

Tuliongozana huku wakiwa wamenishika mkono mpaka sehemu hiyo.

Baada ya kufika, nilishangaa kuona ni jani la mgomba huku likiwa limening’inia.

“Hee! tuoneshe sasa..Huyo mtu yuko wapi?” Waliniuliza.

Asee nilikosa chakuwajibu.

“Hutaki kuongea eeh..!”

“‘Hapana niliona kama mtu lakini sasa hivi simuoni huenda ameondoka”

Baada ya kuwambia hivo, hawakunielewa kabisa mpaka wakaanza kuniambia nisiongee chochote.

” Una chochòte hapo tukuachie..?” Waliniuliza.

“Chochote kipi..?” Niliwajibu huku nikitetemeka.

“Ina maana huelewi au?”

“Sijaelewa..”

“Ohh utaelewa tu.”

Walianza kutembea na mimi kuelekea shamba la mikahawa lililokuwa na giza kwelikweli.

“Mnanipeleka wapi na kwa kosa lipi?” Niliwauliza.

“‘We tulia si umejifanya huelewi basi tunaenda kukufundisha.”

“Kwani kosa langu lipi?, basi nipelekeni kwa mwenyekiti”

“Usitupangie na hutufundishi kazi, fumba mdomo wako.”

Nilikaa kimya mpaka walipofika kwenye sehemu hiyo .

Walinikalisha chini mnamo mida ya saa nane kasoro hivi za usiku.

” Sasa unatakiwa kuwa muwazi .Tumekwambia huna chochote tukuachie lakini unajibu hovyo”

“‘Sasa mimi nina nini?, sina chochote nipo kama mnavyoniona hapa.” Niliongea kwa sauti ya upole.

” Sawa sasa tunakupenda sana na tunathamini utu wako. Tunaomba uwe mpole na usithubutu kunyanyua kinywa chako . Ukikiuka hilo, kitakachokupata usitulaumu”

“‘Lakini kwanini hivyo, nisikilizeni basi niwambie shida zangu.”

” Bwana eeh hatuna mda wa kukusikiliza “

Hasira kali zilinipanda huku nikiwa sijui nini wanawaza juu yangu. Nilimkumbuka mwanangu Furaha pamoja na nyumba kutoka kwenye jasho langu.

Nikiwa nawaza na kuwazua, walinishika mikono yangu kisha mmoja akaniziba mdomo.

Niliogopa sana na kupiga kelele lakini hazikuweza kusikika kwani nilikuwa nimezibwa mdomo.

Walianza kunikagua kwenye nguo zangu lakini hawakupata kitu.

“‘Oyaa amevaa kaptula kwa ndani. Ebu mtoe hiyo kanga”

Nilirusharusha miguu kama samaki aliyetolewa majini kisha na kuwekwa nchi kavu.

Kwenye nguo yangu ya ndani, nilikuwa nineweka elfu 18 ndipo nilipoona maji yamenifikia shingoni.

Ndani ya mda mfupi, walianza kunipapasa kila sehemu wakitafuta pesa mpaka wakanivua kaptula langu.

Baada ya kufanya hivo, nilimuona mmoja akimnong’oneza mwenziye kwa sauti ya chini huku wakionesha sura ya tabasamu…..

Share.
Leave A Reply

error: Content is protected !!